·Shangwe kila kona Mahakama ikichanja mbuga kutekeleza Mpango Mkakati
Na Faustine Kapama-Mahakama, Busega
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 25 Novemba, 2022
amezindua Mahakama za Wilaya 18 kwa mpigo, hatua ambayo inaenda kumaliza kabisa
kero iliyokuwa inawakabili wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za
utoaji wa haki katika maeneo mbalimbali nchini.
Uzinduzi
huo ambao umefanyika katika Mahakama ya Wilaya ya Busega ili kuwakilisha
Mahakama zingine 17 ambazo zimejengwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa
Benki ya Dunia katika Mikoa tofauti umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama,
Bunge, Mkoa wa Simiyu na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi za
Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Bi. Preeti Arora.
Wananchi
waliohudhuria uzinduzi huo katika viwanja vya Mahakama hiyo na wengine
waliokuwa wanafuatilia tukio hilo lililokuwa linaonyeshwa mubashara na
Televisheni ya Taifa walilipuka kwa furaha mara baada ya Jaji Mkuu kutamka “Majengo
mapya 18 ya Mahakama za Wilaya za Busega, Itilima, Butiama, Rorya, Songwe,
Gairo, Mkinga, Mbogwe, Nyang’hwale, Kyerwa, Missenyi, Kaliua, Uvinza, Buhigwe,
Kakonko, Tanganyika, Kilombero na Mvomero yamezinduliwa”.
Mhe.
Prof. Juma aliwashukuru wananchi katika Wilaya hizo 18 kwa kuwa na uvumilivu wa
kusubiri miaka mingi baada ya Wilaya zao za kiutawala kuanzishwa hadi leo walipokabidhiwa
rasmi majengo ya kisasa ya Mahakama za Wilaya. Amebainisha kuwa kiutawala,
Wilaya za Mkinga, Rorya na Missenyi zilianzishwa mwaka 2007, miaka 17 iliyopita,
ambapo Wilaya za Butiama; Gairo; Mbogwe; Nyang’hwale; Kyerwa; Kaliua; Uvinza;
Buhigwe; Kakonko; Itilima na Busega zilizoanzishwa mwaka 2013, huku Wilaya za Tanganyika
na Songwe zikianzishwa mwaka 2016, miaka sita iliyopita.
Mhe.
Prof. Juma alitumia nafasi hiyo kuwajulisha wananchi wa Wilaya hizo 18 ambazo
zimepata majengo mapya ya Mahakama za Wilaya kuwa majengo hayo ni zaidi ya
majengo ambayo yanakuja na uboreshaji wote uliokuwa ukitekelezwa chini ya Awamu
za Kwanza na Pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama (Judiciary Strategic Plan) na
Programu ya Maboresho (Citizen-Centric Judiciary Modernisation Justice Delivery
Project) inayofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mkopo wa Benki ya
Dunia.
“Tarajieni
kupata huduma zilizo bora kutoka kwa watumishi ambao Mpango Mkakati wa Mahakama
na Programu ya Maboresho imewabadili fikra na mitazamo yao katika utoaji wa
huduma. Katika majengo haya tegemeeni kuona watumishi wenye kutoa huduma
zinazomnufaisha mwananchi, zilisogezwa karibu na mwananchi. Wananchi
hakikisheni kuwa huduma zinawaridhisha na endapo mtaona kasoro au mapungufu
msilalamike kimya kimya pigeni simu kwenda CALL CENTRE inayofanya kazi kwa saa
24 kupitia Namba 0752 500 400,”
alisema.
Alimtaka
kila mtumishi wa Mahakama kuvaa beji yenye jina lake ili kukusaidia mwananchi
kumtambua yule ambaye anatoa huduma isiyoridhisha. Alisema kuwa huduma kutoka
ndani ya majengo hayo isiishie tu kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, bali
itimize matarajio ya makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Benki ya
Dunia.
Baadhi
ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameupongeza uongozi wa Mahakama ya
Tanzania chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa uboreshaji wa
kuridhisha wa huduma za kimahakama na kusogeza huduma za utoaji haki karibu na
wananchi, hususani katika kujenga Mahakama za Wilaya 18 ambazo zimeziduliwa
leo.
“Tunaishukuru
Mahakama ya Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kazi
nzuri inayofanya ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi. Ama kweli ndoto
imegeuka kuwa kweli, ni vigumu kuamini, lakini ndiyo imetokea. Wale wanaobeza
mafanikio kama haya wajiangalie upya,” alisema mkazi mmoja wa Busega aliyejitambulisha
kwa majina ya Maduhu Nyanda.
Jaji
Mkuu aliyekuwa ameongozana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha aliwasili katika viwanja vya Mahakama hiyo majira ya saa 3.15 hivi asubuhi
kwa ajili ya ufunguzi wa Mahakama hizo na kupokelewa na viongozi mbalimbali,
akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi, Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka
Kanda ya Shinyanga, Mwanza na Musoma, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Wilbert Chuma na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel.
Kabla
ya kupanda katika jukwaa kuu, Mhe. Prof. Juma alipata nafasi ya kusalimiana na
viongozi, kukagua jengo la Mahakama ya Wilaya Busega na baadaye kukata utepe
maalum kama ishara ya kuzindua Mahakama hizo 18 za Wilaya. Baada ya kupanda
katika jukwaa kuu, Wimbo wa Taifa ulipigwa na baadaye Jaji Mkuu alipokea salamu
kutoka kwa viongozi mbalimbali kabla ya kuongea na Watanzania.
Akiwasilisha
salamu za Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda aliwakumbusha maafisa
wa Mahakama watakaohudumu katika Mahakama hizo za Wilaya kuzingatia utendaji
kazi kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Kanuni za Maadili za Maafisa wa Mahakama kwa kutekelza wajibu wao bila
kujali hali ya kijamii au kiuchumi ya mhusika, kutokuchelewesha haki bila
sababu za msingi, kutoa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria nan kutoa haki bila
kufungwa na ufundiwa kisheria ambao unaweza kukosesha haki kwa wahusika.
Kadhalika,
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa Mahakama, wakiwemo Jeshi
la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa
Kujitegemea, Jeshi la Magereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili mashauri yaweze kumalizika kwa wakati.
“Niwaombe
wananchi kutumia huduma za Mahakama mnapokuwa na migogoro badala ya kuchukua
sheria mkononi. Wananchi mtakapokuwa na malalamiko kuhusu Mahakimu
muwasilishe katika Kamati ya Maafisa wa Mahakama ya Mkoa na Wilaya,” alisema.
Mhe. Dkt. Nawanda aliahidi kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ili
iweze kutekeleza jukumu lake kikamilifu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni