Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Jumla ya shilingi bilioni
18 za Kitanzania zimetumika katika ujenzi wa majengo 18 ya Mahakama za Wilaya
nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo
tarehe 25 Novemba, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwenye halfa
fupi ya uzinduzi wa Mahakama hizo ambao umefanyika katika viwanja vya Mahakama
ya Wilaya ya Busega, mkoani Simiyu.
Akiziwasiliisha taarifa
yake, Mtendaji Mkuu alimwambia Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, wananchi waliofurika katika
viwanja hivyo pamoja na Watanzania waliokuwa wanafuatilia tukio hilo kupitia
Televisheni ya Taifa kuwa ujenzi wa majengo hayo jumla ya shilingi bilioni 2.7
zimetumika kununulia samani kwa ajili ya ofisi mbalimbali za Mahakama hizo.
Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel,
majengo 18 ya Mahakama za Wilaya yaliyozinduliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania yamejengwa
kwa ufadhili wa mkopo nafuu uliotolewa na Benki ya Dunia kwa Serikali ya
Tanzania.
Alisema kukamilika kwa
majengo hayo kumesaidia kuboresha miundombinu ya Mahakama ambapo kati miradi
hiyo 18, miradi 15 ni Mahakama mpya za Wilaya ambazo hazikuwa na huduma za
Mahakama ya wilaya na tatu ni Mahakama za Wilaya zilizokuwa na majengo chakavu.
Prof. Gabriel alizitaja
Mahakama za Wilaya zilizozinduliwa ni Nyang’ale, Mbongwe, Kaliua, Uvinza,
Kakonko, Buhigwe, Kyerwa, Misenyi, Kilombero, Mvomero, Gairo, Songwe, Butiama,
Rorya, Tanganyika, Itilima, Busega na Mkinga.
Alisema ujenzi wa miradi
hiyo ambayo imetekelezwa na Wakandarasi wazawa ipo katika Mikoa tofauti hapa
nchini na imezingatia mahitaji ya kisasa kwa wadau wa mnyororo wa utoaji haki
ambapo zipo ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii ambapo watu
wenye mahitaji maalum na watoto wamewekewa vyumba vya kutumia wakiwa mahakamani
hapo.
Mtendaji Mkuu aliongeza
kuwa kuzinduliwa kwa majengo hayo katika Wilaya hizo 18 kutaongeza ufanisi na
utoaji huduma kwa wananchi kwani majengo hayo yana mzingira rafiki ya utoaji wa
huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia.
Alisema ujenzi wa miradi
hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano (5)
wa 2020/21-2024/25 nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji
wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.
Viongozi wa Mahakama na Taasisi mbalimbali wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa majengo 18 ya Mahakama za Wilaya ilifanyika leo katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Busega, mkaoni Simiyu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni