Na Faustine Kapama-Mahakama, Busega
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameielezea Benki ya Dunia kama mdau muhimu katika
uboreshaji wa huduma zinazoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania katika
maeneo mbalimbali hapa nchini.
Akizungumza na Watanzania
katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama za Wilaya 18 iliyofanyika katika viwanja
vya Mahakama ya Wilaya Busega leo tarehe 25 Novemba, 2022, Mhe. Prof. Juma alisema
kuwa Benki
ya Dunia iliikopesha Serikali ya Tanzania fedha ambazo zimetumiwa na Mahakama
ya Tanzania kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano kupitia Programu ya
Maboresho (Tanzania Citizen-Centric Judicial Modernisation And Justice Delivery
Project).
Amesema kuwa ujenzi
wa majengo mapya ya Mahakama na ukarabati wa majengo mbalimbali umewezekana kwa
sababu Serikali ya Tanzania imetambua kuwa Mhimili wa Mahakama ulihitaji kiasi
kikubwa cha fedha nje ya bajeti ya kawaida ya Mahakama, hivyo ikaamua kufikia
makubaliano na Benki ya Dunia.
“Kwa kutambua kuwa huduma
za utoaji haki ni muhimu katika ukuaji wa uchumi, kuondoa umasikini, kuweka
mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji, kuweka mazingira ya uwazi; kuweka
usawa katika jamii na kulinda amani na utulivu, Serikali ya Tanzania ilichukua
mkopo mkubwa wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia ili kupunguza
changamoto ambazo zinazuia Mahakama kupeleka huduma za utoaji haki karibu na
wananchi,” Jaji Mkuu amesema.
Amesema kuwa kwa Benki ya
Dunia uboreshaji wa huduma za Mahakama una faida kubwa kwa uchumi ambapo kwa mtazamo
wake, fedha za mradi wa Uboreshaji wa Mahakama katika awamu ya kwanza kwa 2015-2020 na awamu ya nyongeza kwa 2020-2025
zinalenga kupunguza umasikini, kuchangamsha ukuaji wa uchumi, kuwasaidia
wanawake, watoto na wanaoishi mbali na Mahakama au katika mazingira hatarishi
kupata huduma za Mahakama sawa na wananchi wengine.
“Nawaomba wananchi wa
Wilaya ya Busega na Wilaya zingine 17 ambazo zinapata majengo mapya ya Mahakama
ya Wilaya watambue kuwa majengo haya ni vielelezo vya dhana ya kusogeza huduma karibu
na wananchi inayotambuliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Dunia,”
Mhe. Prof. Juma alisema katika hafla hiyo iliyokuwa inarushwa mubashara na
Televisheni ya Taifa.
Jaji Mkuu ameshukuru
mchango mkubwa wa Serikali ya Tanzania ambayo imetambua changamoto ya ukosefu
na uchakavu wa miundombinu katika ngazi mbalimbali kote nchini na kuweka
mipango ya ujenzi na ukarabati katika Mpango wa Serikali wa Maendeleo wa Miaka
mitano mitano.
“Serikali ya Tanzania
inatambua kuwa bajeti inayotoa kwa Mahakama isingeweza kuondoa changamoto kubwa
ya uhaba na uchakavu. Hali hii iliilazimu Serikali kutafuta fedha za ziada nje
ya nchi ili kuondoa changamoto ya mahitaji ya majengo,” alisema.
Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa kwa muda mrefu tangu Tanzania imepata uhuru zaidi ya miaka 61
iliyopita, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto
kubwa ya uhaba na uchakavu wa majengo katika ngazi zote za Mahakama.
Amesema kuwa kufuatia
hali hiyo, mwaka 2015 uongozi wa Mahakama uliona kuwa bila kuweka Mpango
Mkakati maalum wa kukabiliana na uhaba na uchakavu wa majengo, Mahakama
itaendelea kuwa na changamoto hiyo na kila ziara inayofanywa na viongozi hukumbana
na maswali mengi kutoka kwa Wabunge kuhusu upungufu na uchakavu wa majengo ya
Mahakama.
“Mwaka 2016 Mahakama ya
Tanzania ilifanya tathmini ya kina kuhusu uhaba na uchakavu wa majengo nchi
nzima na kuandaa ripoti ya hali halisi. Tathmini hii iliainisha kuwa jumla ya
Wilaya 104 kati ya Wilaya 139 zilizopo Tanzania Bara zilikuwa zinahitaji
majengo mapya ya Mahakama za Wilaya kwa sababu ya kutokuwa na majengo kabisa au
kuwa na majengo yaliyokuwa machakavu na yasiyofaa kwa matumizi,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
jumla ya Wilaya 24 zilikuwa na majengo ya Mahakama za Wilaya zilizohitaji ukarabati
mkubwa ambapo ni Wilaya 11 tu ndizo zilikuwa na majengo ya Mahakama ya Wilaya
yenye hali nzuri.
Amesema baada ya Mahakama
kutayarisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2016-2021), uamuzi ukafikiwa wa
kutayarisha pia Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (2016/2017 -
2020/2021) ili kupanga, kuchagua na kuweka vipaumbele na vigezo mahsusi vya
kuhakikisha kuwa changamoto ya upungufu wa majengo na ukarabati mkubwa
inapatiwa ufumbuzi endelevu.
“Mpango wa Miaka Mitano
wa Maendeleo ya Miundombinu ni Andiko Maalum lenye kuainisha uhaba na uchakavu
wa majengo katika ngazi zote za Mahakama, andiko ambalo linatoa Dira ya ujenzi
na ukarabati wa majengo ya Mahakama. Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya
Miundombinu uliandaliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya utoaji huduma za
haki na kusogeza huduma za utoaji haki ili ziwe karibu zaidi na wananchi katika
ngazi zote za Mahakama,” alisema.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mwakilishi
Mkazi wa Benki ya Dunia, Bi. Preeti Arora aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa
kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ambao umeleta mafanikio makubwa
katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kupunguza mlundikano wa mashauri, uharakishwaji
wa usikilizaji wa mashari katika Mahakama na kuanzisha kwa Mahakama
Inayotembea.
Amesema kutokana na
mafanikio hayo, Benki ya Dunia iliidhinisha kiasi cha ziada cha Dola za
Kimarekani millioni 90, hivyo kufanya jumla ya mkopo wa masharti nafuu uliotolewa
kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuboresha huduma mahakamani kufikia dola
za Kimarekani millioni 150.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni