Jumatatu, 28 Novemba 2022

HUDUMA MNAZOTOA ZIAKISI UBORA WA MAJENGO; JAJI NGWEMBE

Na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka Watumishi wa Mahakama za Wilaya 18 zilizopata majengo mapya kutoa huduma bora kwa weledi na uaminifu ili kuendana na uzuri na hadhi ya majengo hayo yaliyozinduliwa na Jaji Mkuu hivi karibuni.

Akizungumza na Watumishi hao mapema leo tarehe 28 Novemba, 2022 alipokuwa akifungua Mafunzo ya Huduma kwa Mteja kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya 18 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki- Morogoro, na Washiriki wengine kutoka vituo vingine vya Kigoma, Bukoba na Musoma walioshiriki kwa njia ya mtandao (virtually), Mhe. Ngwembe amesema kuwa, ni matarajio ya Mahakama ya Tanzania kuwa uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama utakwenda sambamba na utoaji huduma bora kwa wananchi.

“Ni matarajio yangu na ya Mahakama kwa ujumla kwamba, baada ya mafunzo haya kila mshiriki atakuwa ameiva kwa kubadilika kifikra, kimtazamo na weledi na hivyo kuachana na utendaji wa kimazoea ambao ulichangia wananchi kukosa imani dhidi ya huduma zetu,” amesema Jaji Ngwembe.

Mhe. Ngwembe ameongeza kuwa, kila Mtumishi wa Mahakama ana wajibu na jukumu la kuunga mkono jitihada kubwa zinazochukuliwa na Mahakama katika kuboresha utendaji unaozingatia matokeo katika majengo mapya na mifumo ya TEHAMA iliyosimikwa kwenye miundombinu hiyo ya kisasa.

“Kwa kipindi kirefu mtakumbuka, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya majengo, ukosefu wa majengo mapya, sambamba na uchakavu mkubwa wa miundombinu ya majengo ya Mahakama iliyopo sasa katika ngazi mbalimbali kote nchini. Ni kutokana na sababu hizo, ndio maana Mahakama imejiwekea utaratibu wa kujenga majengo mapya na kukarabati majengo yaliyopo kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama Kuu, kwa kutumia vizuri fedha tunazopata kutoka Serikalini na mikopo ya Wafadhili,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.

Mhe. Ngwembe amesema kwamba, mafunzo hayo ni moja ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025 pamoja na Mpango maalumu wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/2022 – 2025/2026.

Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Bi. Beatrice Patrick amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha na kuwawezesha Watumishi wa Mahakama hizo namna bora ya kutoa huduma nzuri kwa wateja wanaofika kupata huduma katika Mahakama hizo.

“Kama unavyofahamu tumezindua Mahakama za Wilaya 18, na kutokana na uzinduzi huo, na kwa kuwa tuna majengo mapya ilionekana ni vema kuwa na mafunzo maalum kwa watumishi wanaokwenda kuzihudumia Mahakama hizo. Vituo hivi vimekusanya watumishi ambao kwa mantiki ya mafunzo tunawaita washiriki kutoka katika Mahakama za jirani kwa lengo la kurahisisha utoaji wa mafunzo kwa muda mfupi kwa Mahakama mpya zote 18,” amesema Bi. Beatrice.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo; Mafunzo haya yamepangwa kufanyika katika Vituo vyetu vinne (4) ambavyo vinajumuisha Mahakama zilizozinduliwa na zipo karibu karibu ili kupunguza gharama ya kutokulazimika kufika kila kituo. Hivyo, Vituo vitakavyoendesha mafunzo haya ni Morogoro IJC, Kigoma, Musoma na Bukoba.

Mafunzo haya yatachukua siku 20 kuanzia leo tarehe 28 Novemba,2022 hadi tarehe 23 Desemba, 2022 ambapo katika kila Kituo mafunzo yataendeshwa kwa muda wa siku tano (5) na wawezeshaji kutoka ndani na nje ya Mahakama. Mada; mada zitakazotolewa ni pamoja na Maadili ya kimahakama, majukumu/wajibu wa Mahakama za Wilaya, Mila na Desturi za kimahakama, mada ya huduma kwa mteja ‘customer service’ na kadhalika.

Akiwasilisha Mada kadhaa katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewasihi Watumishi hao kuzingatia maadili na miiko ya kimahakama, kuwa wabunifu na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.

Tarehe 25 Novemba, 2022 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alizindua Mahakama ya Wilaya Busega iliyowakilisha Mahakama nyingine mpya za Wilaya mpya 17, Mahakama hizo zilizojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ni pamoja na; Butiama, Rorya, Songwe, Gairo, Mkinga, Mvomero, Kilombero, Mbogwe, Nyang'hwale, Kyerwa, Itilima, Missenyi, Kaliua, Uvinza, Buhingwe, Kakonko na Tanganyika.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya mpya 18 alipokuwa akifungua Mafunzo ya Huduma kwa Mteja kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya hizo (hawapo katika picha) yaliyoanza kutolewa leo tarehe 28 Novemba, 2022  kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki- Morogoro. Washiriki wengine  kutoka vituo vingine vya Kigoma, Bukoba na Musoma wameshiriki hafla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo kwa njia ya mtandao (virtually).

Sehemu ya Washiriki pamoja na Wadau wa Mahakama wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya Huduma kwa Mteja kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya 18 zilizozinduliwa hivi karibuni iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (hayupo katika picha). Hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo hayo kwa Watumishi wote wa Mahakama hizo mpya imefanyika kwenye Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Morogoro.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Beatrice Patrick akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya 18.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Bw. Ahmed Ng'eni akiongoza hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya 18.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (katikati) pamoja na Majaji wa Kanda hiyo walioshiriki katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo wakifuatilia/wakimsikiliza Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki aliyekuwa akizungumza  kutoka Kigoma kwa njia ya mtandao. Katika 'screen' ni sehemu ya Watumishi wa Wilaya mpya kutoka Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi. Aliyeketi kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba na kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Morogoro, Mhe. Gabriel Malata.
Washiriki wa Mafunzo kutoka Kigoma, Bukoba na Musoma wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo. 


Washiriki wa Mafunzo wakifuatilia kwa makini.

Ufuatiliaji makini wa kinachoendelea katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama za Wilaya mpya 18. Wa kwanza kutoka kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, wa pili ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Japhet Manyama, anayefuata ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick na wa mwisho ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo-Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu. 




















   

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni