Na Lordgard Kilala – Kituo Jumuishi Temeke
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kimesaini hati
ya makubaliano na Chama cha Mabenki Tanzania (Tanzania Banking Association) ili
kuharakisha utoaji haki kwenye mashauri yanayohusu mirathi na ndoa.
Makubaliano hayo yaliingiwa hivi karibuni wakati wa kikao
cha kawaida cha kusukuma mashauri ya madai kilichohusisha wadau wa haki madai
ya mirathi na ndoa kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi.
Wadau wengine waliohudhuria kikao hicho ni Taasisi za Kifedha,
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Mtandao
wa Watoa Msaada wa Kisheria Tanzania (TANLAP), Chama cha Mawakili wa
Tanganyika, Chama cha Mabenki Tanzania, Mawakili na wenyeji kutoka Mahakama.
Makubaliano hayo ni matokeo ya majadiliano yaliyoanza tarehe
23 Septemba 2022 kuhusu namna bora ya kuharakisha utekelezaji wa hukumu ya haki
mirathi kwa kupunguza vigezo vinavyohitajika na mabenki kwenye kufunga akaunti
ya marehemu na kuhamisha fedha kwenda kwenye akaunti ya amana ya mirathi.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya uwepo wa taasisi kama mabenki
zinazohusika kwenye mnyororo wa malipo ya mirathi ambapo Mahakama haina
udhibiti wa moja kwa moja katika shughuli zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Kituo
hicho, Mhe. Ilvin Mugeta alieleza changamoto ambayo Mahakama hukabiliana nayo
katika kushughulikia mashauri ya masuala ya familia, ikiwemo Mahakama kutokuwa
na uthibiti wa moja kwa moja kwenye shughuli za kibenki.
"Kama hakuna pingamizi la kupinga msimamizi wa mirathi
au uhalali wa wosia, shauri halizidi miezi sita kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi
Mahakama Kuu. Baada ya hapo, michakato inayofuata kuhakikisha msimamizi wa
mirathi anatekeleza majukumu yake inahusisha taasisi zingine ambazo Mahakama
haina udhibiti nazo."
Jaji Mugeta alitoa mifano baadhi ya changamoto hizo kama muda
unaotumika kuhamisha umiliki wa ardhi kutoka kwa marehemu kwenda kwa msimamizi
wa mirathi na kisha kwenda kwa warithi, muda wa kukamilisha malipo ya michango
ya waajiri au waajiriwa kwa marehemu kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja
na uchelewaji wa matangazo magazetini.
“Hapo kuna changamoto ambazo kama zisipodhibitiwa au
kuwekewa utaratibu hata kituo hiki kitaingia kwenye orodha ya Mahakama
zinazochelewesha mashauri. Hizo changamoto haziwezi kutatuliwa kama wadau
hatukutani, kukaa na kuzungumza kutafuta suluhu inayokusudiwa. Kwa kuwa muda
ambao Mahakama imejiwekea kufunga shauri siyo lazima uwe muda ambao taasisi
hizo zimejiwekea kuhudumia wateja wao.” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Chama cha Mabenki Tanzania (Tanzania
Banking Association), Bi Tusekelege Joune, akiwasilisha salamu za taasisi hiyo
kabla ya zoezi la utiaji saini hati ya makubaliano alisema, “Kama Taasisi ya
Mabenki tunaahidi ushirikiano kwani hili jambo linagusa maisha ya kila Mtanzania
na wateja wetu.”
Akifafanua kuhusu makubaliano yatakayowezesha kasi ya huduma
za kibenki kwenye mashauri ya mirathi, Bi. Joune aliendelea kusema, “Sisi kama
sekta ya mabenki hatutaki kuwa kikwazo kumpa haki anayestahili, hivyo tutajidhatiti
kutekeleza mambo tuliyokubaliana wala hatutegemei kupishana katika utekelezaji
kwa kuwa makubaliano haya tunayaelewa na tulishiriki kuyaandaa.”
Akielezea hali iliyopo kwa sasa katika usikilizaji wa mashauri
katika Kituo Jumuishi hicho, Naibu Msajili Martha Mpaze alisema kuwa kasi ya
uondoshaji inaridhisha kwani tangu
huduma ilipoanza tarehe 25 Mwezi Octoba, 2021 hadi tarehe 17 Novemba,
2022, jumla ya mashauri 8,330 kwa aina zote yalifunguliwa ambapo mashauri 6,465
yameshatolewa uamuzi, sawa na asilimia 78, huku mengine 1,865 yakiwa bado
yanaendelea kusikilizwa, ambayo ni sawa na asilimia 22.
Mhe. Mpaze hakuacha kuzungumza kuhusu hali ya mlundikano
ambapo alisema katika Kituo hicho siyo changamoto ukilinganisha na Mahakama
nyingine. Amesema kwa mujibu wa utaratibu wa ndani wa kujipima, viwango
walivyojiwekea vipo juu kuliko vilivyowekwa na Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni