Jumatatu, 28 Novemba 2022

MKUU WA MKOA DODOMA ATEMBELEA UJENZI MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA

 

·Aisifu Mahakama kwa kuboresha huduma na kupunguza malalamiko

Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule hivi karibuni alitembelea mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania unaoendelea kutekelezwa na kupongeza jitihadi zinazofanywa na Mhimili huo katika kuboresha huduma za utoaji haki nchini.

Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mhe. Senyamule alisema kuwa kumekuwepo na uboreshaji wa miundombinu ya majengo, ujenzi wa Mahakama mpya ambazo zinasaidia kusogeza huduma za kimahakama kwa wananchi na namna Mhimili huo ulivyojikita kwenye matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma zake kwa wananchi.

Alisisitiza katika ziara yake ya kutembelea miradi yote ya kimkakati inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Dodoma kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya dhati kwa Mhimili wa Mahakama katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za haki kwa wakati.

“Tumeshuhudia uboreshaji mkubwa wa huduma zinazotolewa katika Kituo Jumuishi na kwa kweli kwa upande wetu tunakiri kuwa huduma hizo zimepekelea malalamiko mengi tuliyokuwa tukiyapokea kutoka kwa wananchi kupungua,” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.

Akiwa katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo utakaogharimu fedha za kitanzania billioni 129.7 pamoja na kodi hadi kukamilika kwake. Mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 75 ya utekelezwaji na aliweza kujionea maendeleo yaliyofikiwa.

 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akiwasili katika eneo unapotekelezwa mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama.
Mwonekano wa mbali wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama lililopo Mkoani Dodoma.
Mwakilishi wa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo akitoa ufafanuzi kuhusiana na mradi huo.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti (aliyesimama mwenye suti ya kijivu) akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe walioshiriki ziara hiyo.


Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti (aliyesimama mwenye suti ya kijivu) akitoa neno la ukaribisho kwa wajumbe walioshiriki ziara hiyo.



Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Senyamule akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) walioshiriki kikao kifupi kabla ya ziara ya kutembelea jengo la Makao Makuu.


Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Fatmah Khalfan akitoa neno la ufunguzi katika kikao hicho; aliyeketi kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Suleiman Hassan.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Fatmah akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mpango Mkakati wa Mahakama na gazeti la Mahakama kwa ajili ya uelewa wa pamoja wa mwelekeo wa Mahakama ya Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni