Jumanne, 29 Novemba 2022

RUSHWA NI KANSA, HAIKUBALIKI: JAJI NGWEMBE

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka watumishi wa Mahakama, hususani katika Wilaya ya Gairo na Kilombero kuitumikia jamii kwa uadilifu usio na mashaka na kujiepusha na rushwa ambayo ni kansa isiyokubalika hata kidogo mahakamani.

Mhe. Ngwembe alitoa wito huo hivi karibuni katika mahojiano maalum siku chache kabla ya uzinduzi wa majengo mapya ya Mahakama za Wilaya 18, ikiwemo Gairo na Kilombero zilizopo katika Mkoa wa Morogoro.

Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza watumishi katika Mahakama hizo kuhakikisha wanayatumia majengo hayo kama kichocheo cha upatikanaji wa haki na si vinginevyo. Aidha, aliwasisitiza kuyatunza majengo hayo ili yaweze kuhudumia wananchi kwa kipindi kirefu kama inavyotarajiwa.

“Majengo haya ni mapya na mazuri, hivyo ni wajibu wetu kuyatunza kama mboni ya jicho, tuyalinde, sio mategemeo yetu kuona yanapoteza ubora wake ndani ya miaka miwili au mitatu” alisisitiza Mhe. Ngwembe.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo aliwasihi wananchi kuzitumia Mahakama hizo kutatua migogoro yao na sio kujichukulia sheria mikononi, jambo linaloweza kuwaingiza katika matatizo makubwa. Vilevile aliwasisitiza kutilia mkazo elimu ya sheria inayotolewa mahakamani na katika vyombo vya habari kama sehemu ya kujifunzia masuala mbalimbali ya msingi yahusuyo sheria.

Aliongeza kuwa ujenzi wa majengo hayo uliofadhiliwa na Benki ya Dunia umemaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa Mahakama ya Wilaya Gairo ambapo hapo awali wananchi hao walilazimika kuifuata huduma hiyo umbali mrefu.

“Tunategemea Mahakama ya Wilaya ya Gairo itakuwa mkombozi kwa wananchi waliokuwa wanakwama kupeleka mashauri katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa kwa kukwepa umbali” alisema.

Hivyo akaishukuru Benki ya Dunia kupitia Mhimili wa Mahakama na Serikali kwa kutoa fedha zilizowezesha kujengwa kwa Mahakama ya Wilaya Gairo na kuboresha Mahakama za Wilaya Mvomero na Kilombelo, hatua ambayo imeweka mazingira wezeshi ya utoaji haki kwa wananchi.

Ujenzi wa Mahakama hizo za Wilaya ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano wa 2020/21- 2024/25 katika nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe.
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni