- Mufti wa Kenya mambo safi
Na
Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Kituo
Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta amewaomba viongozi wa
dini na Kamati ya Amani ya Jumuiya ya Maridhiano Tanzania kushirikiana na Mahakama
ya Tanzania katika kurejesha maadili, kujenga taswila njema na kukuza imani kwa
wananchi.
Akizungumza wakati
anafungua mafunzo ya siku mbili ya wajumbe wa Kamati hiyo leo tarehe 29
Novemba, 2022 katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Kituo hicho Jumuishi jijini Dar es Salaam,
Mhe. Mugeta amesema kuwa Mahakama inawashirikisha viongozi hao kwa kutambua
mchango wao katika kujenga mtangamano wa kijamii.
“Mahakama ya Tanzania inaamini
kuwa mkiwezesha jamii kutanzua migogoro kwa usuluhishi, kesi mahakamani
zitapungua na itaishi kwa amani zaidi. Kazi na wajibu wenu wa kuhakikisha jamii
inaishi kwa usuluhishi na maridhiano ni muhimu sana kwani utatuzi wa migogoro
kwa njia hizo ni ishara ya kuwa na jamii iliyostaarabika,” alisema.
Jaji Mfawidhi huyo
amewaambia viongozi hao kuwa kwa kufundisha na kuhimiza maisha yanayozingatia maadili
miongoni mwa waamini wao kutatokomeza vitendo vya ufisadi nchini ambavyo
huathiri sana shughuli za utoaji huduma na haki katika jamii.
Aidha, amewaomba
wafuatilie kwa makini mada zikazowasilishwa katika mafunzo hayo ili waweze
kufahamu majukumu ya Mahakama kikatiba katika kulinda amani ya nchi na Sheria
ya uendeshaji wa Mahakama, Mpango Mkakati wa Mahakama na Maboresho katika
Mahakama, mafanikio na changamoto.
Mhe. Mugeta amezitaja
mada zingine zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, ikiwemo Biashara haramu ya
utumwa wa kisasa, madawa ya kulevya na
madhara kwa jamii; Imani zenye misimamo mikali na athari katika jamii na
Utamaduni wa Kiafrika au Kitanzania na ujio wa dini.
Mada zingine ni Uhusiano
wa Mihimili ya nchi na namna inavyofanya kazi na dhana ya Serikali na Utawala
bora na Rushwa katika Tanzania na changamoto za Rushwa kwa Mahakama.
Mhe. Mugeta amesema kuwa
ni imani yake baada ya mafunzo hayo, viongozi hao wataifahamu vyema Mahakama na
utendaji wake, hivyo kuwa mabalozi wake kwa kuwaelezea waumini wao mambo mazuri
yanayofanywa na Mahakama katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa
maendeleo ya nchi.
“Tunatamani wananchi
wafahamu kuwa Mahakama ni sehemu ya utatuzi wa migogoro kinyume na taswira
iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya wanajamii kwamba Mahakama ni mahali pa
kufunga watu,” amesema.
Amewahakikishia viongozi
hao kuwa Mahakama inawaona kama wadau muhimu na inathamini mchango wao katika
utekelezaji wa majukumu yake. Amesema Mahakama itaendea kutoa ushirikiano kwa
viongozi hao pale watakapouhitaji.
“Milango iko wazi,
tunawakaribisheni muda wowote kwa ajili ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo
ya kuboresha utoaji wa haki na utatuzi wa migogoro nchini,” amesema.
Akizungumza katika
ufunguzi huo, Mufti wa Kenya Omar Aboubakar alisema kuwa Mahakama zinahitaji
ushirikiano wa karibu na viongozi wa kidini ambao huchangia kwa kiasi kikubwa
katika kurejesha maadili kwa wananchi, hivyo
kupunguza au uondosha kwa kiasi kikubwa madhara mbalimbali katika jamii.
Amesema ushirikiano huo
utaondoa hofu kwa wananchi kwamba mahakamani ni mahali panapoogofya, jambo
ambalo sio kweli. “Mahakamani ni mahala pa zuri na salama, ambapo mtu atapata
haki yake, atapata usawa na haki na usawa vikiwepo vitaleta amani katika
jamii,” alisema.
Akitoa neno la
utangulizi, Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia
Ngungulu amesema Mahakama imeona ni vema kuwashirikisha viongozi hao ambao ni
sehemu muhimu kwa jamii kwani kwa kupitia wao ujumbe utafika kwa waamini
wanaowahudumia kwa kuwaelimisha kuhusiana na mmomonyoko wa maadili katika
jamii.
“Ni rahisi watu
wakaelimishwa wakiwa Makanisani au Misikitini kuhusu ubaya wa utendaji wa
makosa kama ubakaji, utumiaji wa madawa ya kulevya, mauaji, unyang’anyi na
mengine na wakaweza kubadilika kimienendo na kifikira na hatimae kuwa na jamii
nzuri na kupungua kwa matendo hayo kama si kumalizika kabisa,” amesema.
Sehemu ya viongozi wa dini wanaohudhuria mafunzo hayo.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa Kamati ya Amani ya Jumuiya ya Maridhiano Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni