Na Mary Gwera, Mahakama-Morogoro
Watumishi wa Mahakama mpya za Wilaya 18 zilizozinduliwa
hivi karibuni wanaendelea kupatiwa mada mbalimbali za kuboresha utendaji kazi
wao katika Mafunzo yanayoendelea kutolewa kwenye Ukumbi wa Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki (IJC) Morogoro.
Ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo hayo, leo tarehe 29 Novemba,
2022 mada zilizotolewa ni pamoja na; Wajibu na Majukumu ya Mahakama za Wilaya, Utunzaji
na matumizi sahihi ya Kumbukumbu na matumizi ya ofisi mtandao ‘e-office’, Mradi
wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama.
Akiwasilisha Mada ya Wajibu na Majukumu ya Mahakama ya Wilaya,
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt amewataka
Watumishi wa Mahakama hizo kuwathamini wananchi ambao ndio wateja
wanaosababisha wao kuwa kazi, hivyo huduma zitakazotolewa ziwe za viwango.
“Nadhani hapa wote mnafahamu majukumu ya Mahakama
mnazofanyia kazi, hivyo tuko hapa kwa ajili ya kukumbushana ili kutoa huduma bora
zaidi, ni matumaini yangu na Mahakama kwa ujumla kuwa mtaboreshaji utendaji
kazi wenu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza jukumu kuu la Mahakama la
kutoa haki,” amesema Mhe. Sarwatt.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu-
Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula amewaasa Watumishi hao kuzingatia
utunzaji sahihi wa nyaraka mbalimbali za ofisi na kuwaasa kutunza siri za ofisi
na za wateja.
Akiwasilisha mada ya Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za
Mahakama, naye Mchumi Mwandamizi kutoka Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Bi. Felister Fatukubonye amewaeleza washiriki wa Mafunzo hayo kuwa Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango
Mkakati wake wa mwaka 2020/2021-2024-2025, ambapo amewaeleza Watumishi hao kuwa Mahakama ya Tanzania bado inaendelea na uboreshaji wa huduma mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji haki inamfikia mwananchi kwa urahisi.
Aidha, Bi. Felister amesema kuwa, ili jitihada za Mahakama, Serikali na Wafadhili ziweze kuzaa matunda kunahitajika ushirikiano wa pamoja ikiwemo watumishi kubadili mtazamo na fikra ili uboreshaji za miundombinu na kadhalika viweze kwenda sambamba na utoaji huduma bora kwa wananchi.
Mafunzo haya ya Huduma kwa mteja yanaendelea kutolewa na Watumishi hao mpaka tarehe 02 Desemba, 2022
na mada nyingine zitatolewa ikiwemo Jinsi ya kukabiliana na msongo (Stress
Management) na kadhalika.
Washiriki wakimsikiliza mtoa mada (hayupo katika picha).
Mkurugenzi Msaidizi kutoka Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania, Bw. Daniel Msangi akichangia mada ya Mradi wa uboreshaji wa huduma za Mahakama iliyotolewa na Bi. Felister.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni