Jumatano, 30 Novemba 2022

MTENDAJI MKUU WA MAHAKAMA ASISITIZA MARIDHIANO KATIKA KUTATUA MIGOGORO

·Amwaga vifungu vya Biblia, Quoran mbele ya viongozi wa dini

Na Faustine Kapama-Mahakama

Mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa dini kuhusu masuala ya usuluhishi na maridhiano yaliyokuwa yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania yamehitimishwa leo tarehe 30 Novemba, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Kutuo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam, Prof. Ole Gabriel aliwaomba viongozi hao kuwahimiza waumini katika Makanisa na Misikitini kutatua migogoro yao kwa njia ya usuluhishi.

“Nawaomba mfanye kila manaloweza kuwahimiza waumini wenu kufuata miongozo iliyowekwa katika Biblia na Quran Tukufu kufikia maridhiano kwenye migogoro mbalimbali kabla ya kukimbilia mahakamani,” alisema.

Mtendaji Mkuu huyo alibainisha kuwa pamoja na Mahakama ya Tanzania kuanzisha Kituo maalumu cha Usuluhishi, bado anaamini viongozi wa dini ni chombo muhimu katika kuwasidia wananchi kutatua migogoro inayowakabili kwa maridhiano, njia ambayo ina manufaa makubwa katika jamii, ikiwemo kuoiarisha undugu.

Aliwapitisha viongozi hao wa dini pamoja na Kamati za Amani na Jumuiya za Maridhiano Tanzania kwenye Quran Tukufu ambayo inaeleza, “Hakika si vinginevyo waumini wote ni ndugu, basi tengenezeni katika udugu wenu.” Hivyo akasema kinachoaminika kwenye maandiko hayo matakatifu ni wananchi kutengeneza mambo yao katika undugu.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel aliwapitisha viongozi hao katika Biblia, Matayo 18:15-17, ambayo inasema “Na ndugu yako akikukosa enenda ukamuonye, wewe na yeye pekee yenu, akikusikia umempata nduguyo.

“La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao liambie Kanisa na asipolisikia Kanisa pia na awe kwako mtu wa mataifa na Mtoza ushuru.”

Hivyo, amewasihi viongozi hao kutengeneza mifumo ya kuwaelimisha watu katika Makanisa na Misikitini ili kuwa na maridhiano kuanzia ngazi ya familia. “Tusipofanya hivyo tutakuwa tumetenda kosa kubwa na migogoro itatufuata mpaka Misikitini na Makanisani,” amesema.

Mtendaji Mkuu alitoa mfano katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia ambacho kilianza kutoa huduma za utoaji haki Octoba 2021 ambapo hadi hivi sasa kimeshasajili mashauli 2,906 ambayo asilimia 98 ya wahusika wana dini zao.

Hivyo akataka kujua viongozi wa dini kama waliwahi kuwaelimisha waumini hao kufuata taratibu kama zilivyoainishwa katika maandiko matakatifu hayo kabla ya kukimbilia mahakamani.

Prof. Ole Gabriel amewahakikishia viongozi hao kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha mashauri mengi yanamalizika kwa njia ya usuluhishi kwa kuzingatia Jumuisha hiyo ya Maridhiano ni nguzo muhimu ambayo itasaidia kuimarisha mahusiano mema katika ya jamii.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewasihi pia viongozi hao kukemea maovu bila kuogopa na kuwasaidia waumini wao kupitia mahubiri wanayoyatoa kubadili fikra hatua itakayosaidia kubadilisha uchumi wa nchi, watu kujitambua na kumwogopa Mungu.

“Nyinyi viongozi wa dini mna nafasi kubwa ya kufanya mageuzi ya kifikra na Mahakama ipo tayari kushirikiana na nyinyi mpaka tufanikishe hayo malengo yetu,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti wa Kamati za Amani na Jumuiya za Maridhiano Tanzania, Alhaji Musa Salum ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewawezesha kujifunza mambo mengi, ikiwemo kujua kuwa Mahakama haipo kwa ajili ya kufunga watu bali ni mahali salama ambapo wananchi hupatiwa haki zao.

“Tumepata faida nyingi sana, tumepata uelewa kuhusu Mahakama. Tumepata kujua namna ambavyo tunaweza kushirikiana na Mahakama. Kutokana na mafunzo haya, tunaahidi kuyafanyia kazi yale yote tuliyojifunza,” amesema.

Akiwasilisha neno la utangulizi kabla ya kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu- Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick alimweleza Mtendaji Mkuu kuwa viongozi hao wamepitishwa katika mada mbalimbali, zikiwemo kufahamu majukumu ya Mahakama kikatiba katika kulinda amani ya nchi na Sheria ya uendeshaji wa Mahakama, Mpango Mkakati wa Mahakama na Maboresho katika Mahakama, mafanikio na changamoto.

Mada zingine zilizowasilishwa kwenye mafunzo hayo ni Biashara haramu ya utumwa wa kisasa, madawa ya kulevya na madhara kwa jamii; Imani zenye misimamo mikali na athari katika jamii na Utamaduni wa Kiafrika au Kitanzania na ujio wa dini, Uhusiano wa Mihimili ya nchi na namna inavyofanya kazi na dhana ya Serikali na Utawala bora na Rushwa katika Tanzania na changamoto za Rushwa kwa Mahakama.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati anafunga mafunzo ya siku mbili leo tarehe 30 Novemba, 2022 ambayo yaliandaliwa kuwajengea uelewa viongozi wa dini katika masuala mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kamati za Amani na Jumuiya za Maridhiano Tanzania, Alhaji Musa Salum akiwasilisha neno la shukrani kwa niaba ya viongozi wenzake waliohudhuria mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu- Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick akiwasilisha salamu kabla ya kuhitimishwa mafunzo hayo.
Meza kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa dini (juu na chini) waliohudhuria mafunzo hayo.

Meza kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya viongozi wa dini (juu na chini) waliohudhuria mafunzo hayo.


Meza kuu ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama waliokuwa wanaratibu mafunzo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni