Na Faustine Kapama – Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma amewasihi wadau mbalimbali wa haki jinai duniani
kuunganisha juhudi na nguvu kitaifa, kikanda na kimataifa ili kupambana kikamilifu
na uhalifu wa kifedha, hususani katika makosa dhidi ya wanyamapori, ugaidi na utakatishaji
fedha.
Mhe. Mruma ametoa wito huo leo tarehe 7 Novemba, 2022
alipokuwa anafungua mafunzo kuhusu makosa ya kifedha ya siku tano ambayo yanawaleta
pamoja Majaji 14 na Mahakimu Wakazi 26 ili waweze kubadilishana
uzoefu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za
biashara haramu kwenye makosa hayo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo ambayo yameandaliwa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kikundi
cha Kupambana na Utakatishaji Fedha cha Mashariki na Kusini mwa Afrika-The Eastern
and Southern Africa Anti-Money Laundering Group (ESAAMLG) na Shirika la
Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Jaji Mfawidhi huyo alibainisha kuwa utakatishaji
fedha, ufadhili wa ugaidi na biashara haramu ya wanyamapori ni makosa makubwa yanayohusisha
makundi ya wahalifu waliojipanga.
"Hakuna nchi ambayo haijaguswa na uhalifu huu,
ambao unaathiri bioanuwai, afya ya binadamu, usalama wa taifa, ongezeko
lisiloelezeka la mahitaji ya bidhaa na huduma, uadilifu wa mfumo wa kifedha na
maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku ukiboresha vikundi vya uhalifu. Ni
kupitia utakatishaji fedha ambapo shughuli haramu ya fedha inahalalishwa.
Mafunzo haya yanafanyika kwani yanaongeza kiwango cha uelewa miongoni mwetu
maafisa wa Mahakama, ni matumaini yangu wadau wengi wa sekta ya haki
watafikiwa,” alisema.
Jaji Mruma alibainisha pia kuwa ongezeko la haraka la utandawazi
na shughuli huria za kifedha bila shaka umefanya utakatishaji fedha kuwa
mojawapo ya migogoro ya kimataifa. Amesema hali hiyo imepelekea umuhimu wa uwepo
wa mikakati na juhudi za pamoja kwa ajili ya vita dhidi ya utakatishaji fedha,
hivyo akasisitiza nchi lazima zishiriki katika vita hiyo.
Alisema kwa kutambua ukweli huo mashirika kadhaa ya
kimataifa, ambayo ni mashuhuri zaidi katika mapambano dhidi ya utakatishaji
fedha na ufadhili wa kigaidi duniani (The Financial Action Task Force (FATF), yameandaa
mapendekezo na mbinu bora ili kusaidia nchi zote kuimarisha juhudi zao katika
mapambano hayo.
Aliipongeza ESAAMLG katika kupambana na utakatishaji fedha
kwa kutekeleza mapendekezo ya FATF. Jaji huyo alidokeza kuwa ESAAMLG imekuwa
ikishirikiana na mashirika mengine ya kimataifa yanayohusika na kupambana na
utakatishaji fedha, kuendeleza uwezo wa kitaasisi na rasilimali watu na
kuratibu usaidizi wa kiufundi pale inapobidi.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Mahakama ya Tanzania
inafanya kazi kwa bidii katika kutoa huduma kwa gharama nafuu na kwa ufanisi
ambao utaleta maendeleo endelevu kwa taifa letu. Vile vile tunawashukuru
ESAAMLG na GIZ kwa kukubali ombi letu la kuendesha mafunzo haya kwa Majaji na
Mahakimu na hasa utayari wao wa kusaidia mafunzo katika awamu mbili, moja kwa
Mahakimu 40 na haya yanayoanza leo,” alisema.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba
ya Mkuu wa Chuo cha IJA, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Mratibu
wa Mafunzo ya Mahakama IJA, Mhe. Eliya Baya alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo
hayo ni muendelezo mwingine kama hayo yaliyotolewa kwa kundi la kwanza la
Mahakimu 40 mwezi Septemba mwaha huu.
Alipendekeza IJA, GIZ na ESAAMLG kuandaa na kuratibu
mafunzo zaidi kwa maafisa wengine wa Mahakama na wadau wa haki jinai katika
siku za usoni ili kujenga uelewa kuhusu tishio linalosababishwa na wahalifu
wanaojihusisha na uhalifu, kutenda makosa yanayohusu utakatishaji fedha,
ufadhili wa ugaidi, biashara haramu ya wanyamapori na uhalifu mwingine
unaohusiana na hayo.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Wizara ya Maliasili na
Utalii, wawezeshaji kutoka Mamlaka za Wanyamapori za baadhi ya nchi barani
Afrika na wawezeshaji wabobevu kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Katika mafunzo hayo washiriki watapitishwa kwenye
maeneo mbalimbali, ikiwemo sheria za kitaifa na kimataifa zihusuzo makosa dhidi ya wanyamapori, ugaidi na utakatishaji fedha;
madhara ya makosa hayo katika taifa na dunia; urejeshaji wa mali zilizopatikana
kutokana na makosa hayo na wajibu wa maafisa wa Mahakama, wapelelezi na
waendesha mashtaka katika uendeshaji wa mashauri yanayohusu makosa hayo.
Mratibu wa Mafunzo ya Mahakama IJA, Mhe. Eliya Baya akieleza jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma akiwasili katika ukumbi wa mkutano katika hoteli ya Ramada yanapofanyikia mafunzo hayo.












Hakuna maoni:
Chapisha Maoni