Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Elimu ya usalama
barabarani iliyoanza kutolewa kwa wateja wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Morogoro kuanzia tarehe 1 Novemba, 2022 imeitimishwa jana tarehe 3
Novemba, 2022.
Mahakama ya Tanzania kupitia
vipindi vya elimu ya sheria kwa wananchi wiki hii walitoa mualiko kwa jeshi la
Polisi mkoani hapa kutoa mafunzo ya siku tatu kwa wananchi ili kujilinda na masuala
mbalimbali ya usalama wawapo barabarani.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo maalum, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe alisema kuwa Mahakama mkoani hapo haitosimama
peke yake katika kuwapatiwa wananchi elimu, bali itashirikiana na taasisi
mbalimbali ambazo ni wadau wa Mahakama ili kumsaidia mwananchi awe salama.
“Hatutasimama Mahakama
peke yetu kwani Serikali ina mkono mrefu, hivyo tutawatumia wataalamu toka
taasisi zingine kuwafikia wananchi hawa, ndio maana tunapoelekea mwisho wa
mwaka tumewaalika jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani watufundishe
ili tuendelee kuwa salama na tumepanga kuwafikia wananchi zaidi ya mia tano
ndani ya hizi siku tatu.” aliongeza.
Aidha Mhe. Ngwembe
alieleza kuwa baada ya Mahakama kuanza kutoa elimu hiyo kumekuwa na mabadiliko
makubwa kwa wananchi wa Mkoa huo ambapo kesi zinazopelekwa mahakamani ni zile
zenye mantiki, kwa kuwa jamii imeelimishwa na kuepuka kutenda makosa kwa
makusudi. Amesema elimu hiyo pia imepunguza malalamiko mengi kwani sasa
wananchi wanauelewa katika masuala mbalimbali.
Akitoa elimu kwa
wananchi, Mratibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Zauda Mohamedi
alisema kuwa Jeshi la Polisi lipo tayari kushirikiana na raia wema wote ili
kuhakikisha usalama unadumu, huku akipongeza jitihada za uongozi wa Mahakama
kwa mkakati wake wa elimu na kuahidi kutoa ushirikiano kila mara
watakapohitajika kufanya hivyo.
Kwa muda wa siku tatu
wananchi walifundishwa mambo mbalimbali ikiwemo haki za abiria, umuhimu wa kuwa
na bima, usalama barabarani na ulinzi wa mtoto, ambapo waelimishaji mbalimbali
kutoka Jeshi la Polisi walikuwepo kutoa elimu hiyo, akiwemo Mkaguzi Msaidizi wa
Jeshi la Polisi mkoani hapa Emmanuel Kaboja pamoja na Inspekta Victoria Godrich
kutoka Stendi Kuu ya Mabasi.
Naye mteja aliyefika
mahakamani hapo, Bw. Rashid Omary kutoka Malinyi alitoa shukurani zake kwa
uongozi wa Mahakama kwa kuwa na maono ya mbali ya kuwapatia elimu hiyo kwani
inawasaidia kuepuka kutenda makosa na kuendelea kufanya shuguli za kuwapatia
kipato.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe
Chaba aliwakaribisha wananchi waendelee kufika siku zijazo kwani wataalam
mbalimbali watendelea kuja kutoa elimu. Kadhalika, Mhe. Chaba alilishukuru Jeshi
la Polisi kwa ushirikiano waliouonyesha na kuomba wasisite tena kufika
watakapoombwa kufanya hivyo.
Tokea kuanzishwa kwa
elimu ya sheria kwa wananchi katika kituo hicho mwezi Machi 2022 kumekuwa na
muitikio mkubwa wa wananchi ambao wengine hufika kwa ajili ya kusikiliza
vipindi hivyo tu na mpaka sasa tathimini inaonesha wananchi zaidi ya 20,000
wamepata elimu hiyo, huku takwimu zikionyesha wananchi 150 mpaka 200 hufikiwa
na elimu hiyo kwa siku.
Jaji wa Mahakama kuu ya
Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba akiongea na wananchi wakati wa
kuhitimisha elimu ya usalama barabarani iliyotolewa na Jeshi la Polisi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni