Jumatatu, 14 Novemba 2022

JAJI MKUU KUZINDUA MAHAKAMA ZA WILAYA MWANGA, SAME

Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma tarehe 15 Novemba, 2022 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla za uzinduzi wa Mahakama ya Wilaya ya Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Hafla hiyo itakaofanyika katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Mwanga ni mwanzo wa uzinduzi wa miradi mingine 24 ya Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya itakayozinduliwa mwezi huu wa Novemba na mwezi Disemba mwaka huu wa 2022.

Majengo ya Mahakama hizi mbili yaliyopo mkoani Kilimanjaro yameanza kutumika na inatarajiwa kuwezesha watumishi wa Wilaya hizo kuwa katika mzingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi  kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia.

Ujenzi wa miradi hii imezingatia mahitaji ya kisasa ya wadau wa mnyororo wa utoaji haki ambapo kutakuwa na ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii na watu wenye mahitaji maalum huku watoto wakiwekewa vyumba maalumu vya kutumia wakiwa mahakamani hapo.

Kukamilika kwa majengo ya Mahakama za Wilaya Mwanga na Same yataongeza ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi.

Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka Mitano (5) wa 2020/21-2024/25 katika nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

Hafla ya uzinduzi inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Mahakama na Serikali wakiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumaro, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu na Wabunge toka majimbo ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Wananchi wa Wilaya ya Mwanga na Same wanaombwa kujitokeza katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Mwanga kushuhudia uzinduzi huo ambao ni ishara ya kuwepo mabadiliko makubwa ya uboreshaji wa utoaji huduma za Mahakama nchini.

Halikadhalika wananchi wa maeneo mbalimbali nchini wanaweza kushuhudia tukio hilo kupitia Televisheni ya Taifa (TBC) itakayoonyesha tukio mubashara kutoka katika Mahakama ya Wilaya Mwanga.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni