Na Angel Meela-Mahakama, Arusha
Chama cha
Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kimeandaa mafunzo ya siku tatu kwa
ajili ya kuwapika wakufunzi wa kitabu cha masuala ya kijinsia ya wanawake na
watoto watakaozunguka nchi nzima kutoa mafunzo kuhusu kitabu hicho.
Mafunzo
hayo yaliyoanza jana tarehe 11 Novemba, 2022 jijini hapa ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika
Bagamoyo hapo awali na pia ni utelekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa alipokua akizindua
kitabu hicho tarehe 20 Octoba, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kitabu
hiki chenye jina "TANZANIA GENDER BENCH BOOK ON WOMEN’S RIGHTS” ambacho
kimeandikwa na timu wa wanachama wa TAWJA na kufadhiliwa na UN Women kupitia
Ubalozi wa Sweden kimeandaliwa mahususi kitumike kama nyenzo kwa watoa uamuzi
na wadau wa haki wakati wa rejea za mashauri yenye mtazamo wa kijinsia.
Akifungua
mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim
Tiganga alisema kuwa anafahamu hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo Rais wa Tanzania
yenye nia ya kufikisha injili hiyo ya haki kwa watanzania na wadau wengi zaidi.
“Ninafarijika
na kufurahishwa na kazi mbalimbali za kitaaluma na kijamii wanazozifanya
wanachama wa TAWJA, licha ya ratiba ngumu sana na nafasi nyeti walizonazo
katika tasnina ya utoaji haki kitaifa na kimataifa bado wanapata muda wa
kufanya shughuli za kitaaluma na kijamii,” alisema.
Mhe.
Tiganga alisema kuwa wameshuhudia kwa upana na unyeti wake wanachama wa TAWJA
wakiwa mahiri kuhakikisha haki sawa kwa wote inapatikana na kukuza utawala wa
sheria kwa takribani miaka 22 tangu kuundwa kwa chama hicho 2000.
“Niwapongeze
na kuwataarifu kuwa mnastahili kujivunia juhudi na mafanikio hayo, kwani si
rahisi kuelewa ni jinsi gani mnaweza kufanya yote haya bila kuathiri majukumu
yenu ya utoaji haki kitaifa na kimataifa, ikizingatiwa kuwa hata Rais wa
Makakama ya Afrika ya ya Haki za Binadamu na Watu ni zao la umoja huu,"
alisema.
Sambamba
na hilo, Jaji Mfawidhi huyo alisisitiza kuwa anatambua jitihada za
kubadilishana uzoefu kitaaluma miongoni mwao katika kazi ya utoaji haki
wanayoifanya TAWJA ambapo katika juhudi hizo wanaume hawajaachwa nyuma, na
ndiyo maana hata katika orodha ya washiriki na wawezeshaji wapo wanaume wa
kutosha.
Aidha,
aliwaeleza kuwa haki za kijinsia si kwa wanawake na watoto pekee, wapo wanaume
wengi nao wanapitia magumu katika maeneo mbalimbali na tayari baadhi yao wamefunguka
na wameunda chama chao kinaitwa “Chama cha Wanaume Wanaopigwa na Wake zao
Majumbani (CHAWAWAWAMA)”
“Rais wao
amejitambulisha kuwa anaitwa Bw. Ernest Josephat Komba, ambaye anapatikana
U-tube. Huduma na mafunzo mtakayo kwenda kuyatoa ni vyema pia yakazingatia
kundi hili ambalo kwa muda mrefu limekuwa halina msaada matokeo yake ni taarifa
nyingi tunazosikia za wanaume kujinyonga," alisema.
Mhe.
Tiganga aliwapongeza wanachama wa TAWJA kwa juhudi kubwa wanazozifanya na amewaasa
kuendelea kazi vizuri zaidi na kuyatumia mafunzo hayo kama chachu ya mabadiliko
ya kumpatia mwanamke na mtoto haki na heshima anayostahiki katika jamii ya
kitanzania.
Alisema kuwa kufanyika kwa mafuzo hayo ni sawa na kuwasha Mwenge ambao utafika kila kijiji ukiwamulikia wanaohitaji elimu ya haki ambayo walengwa wote wataipata ili iwaweke huru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni