Jumamosi, 12 Novemba 2022

UHALIFU HAULIPI: JAJI MFAWIDHI DAR ES SALAAM

Na Faustine Kapama – Mahakama

Mafunzo ya siku tano kuhusu makosa ya kifedha yaliyowaleta pamoja washiriki 39 wakiwemo Majaji 14 wa Mahakama Kuu ya Tanzania kubadilishana uzoefu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo sheria za kimataifa na kitaifa za biashara haramu kwenye makosa hayo, yamehitimishwa jana tarehe 11 Novemba, 2022.

Akihitimisha mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma alitoa wito kwa jamii kuacha kujihusisha na makosa ya kifedha, ikiwemo uhalifu dhidi ya wanyamapori, ugaidi na utakatishaji fedha kwani uhalifu kwa namna yoyote ile haulipi.

“Katika kutekeleza majukumu yetu, lazima tutume ujumbe mmoja mzito kwa jamii nzima kwamba uhalifu haulipi. Watu lazima wawe na njia halali za kupata kipato iwe kutoka ofisi au ajira, biashara au uwekezaji. Mwamko wa jamii ni muhimu sana kutufanya tushinde vita hivi,” alisema.

Alieleza kuwa wanyamapori wanahitaji kulindwa na hivyo kuwe na hapana kubwa kwa biashara haramu ya wanyamapori, huku utakatishaji wa fedha ushughulikiwe ipasavyo na ufadhili wa ugaidi ukatishwe tamaa kwa gharama yoyote ile.

Jaji huyo aliwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa biashara haramu ya wanyamapori imefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa, kwa kiasi fulani kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kutoka kwa walaji na kwa kiasi uhalifu huo unatishia amani, usalama, maisha na viumbe hai.

“Biashara ya wanyamapori inazidi kuwa tishio, wakati idadi inayoongezeka ni kinyume cha sheria na isiyo endelevu inayotishia maisha ya viumbe wengi porini. Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yametuonyesha umuhimu wa wanyamapori na madhara ya biashara haramu ya wanyamapori na nini tunatakiwa kufanya ili kukabiliana na makosa ya aina hii,” alisema.

Aidha, Mhe. Mruma alidokeza kuwa makundi ya kigaidi yanahitaji fedha ili kujiendeleza na kutekeleza vitendo vya kigaidi na kwamba ufadhili wa kigaidi unajumuisha njia na mbinu zinazotumiwa na mashirika ya kigaidi kufadhili shughuli zao.

"Fedha hizi zinaweza kutoka kwenye vyanzo halali, kwa mfano kutokana na faida kwenye biashara na mashirika ya hisani. Lakini vikundi vya kigaidi vinaweza pia kupata ufadhili wao kutokana na shughuli haramu kama vile usafirishaji wa silaha, dawa za kulevya au watu, au utekaji nyara ili kupata fidia,” Jaji Mruma alisema.

Alisisitiza kuwa uwezo wa maafisa wa haki jinai na watekelezaji wa sheria katika kuchunguza, kushtaki na kuhukumu ufadhili wa ugaidi, kupitia utoaji wa mafunzo maalumu kwenye masuala yanayohusu mbinu za kiuchunguzi, kukamata na kutaifisha mali za ugaidi na pia kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa dhidi ya ufadhili wa ugaidi bado, unahitaji kujengwa.

Jaji Mfawidhi huyo alibainisha kuwa haiwezekani kutenganisha utakatishaji wa fedha na uhalifu wa kifedha kwa sababu karibu uhalifu wote wa kifedha unalazimika kusababisha fedha kuibiwa au mapato kupatikana, ambayo yatalazimika kutakatishwa pamoja na ukweli kwamba utakatishaji fedha ni uhalifu wa kifedha wenyewe.

"Vyanzo vya fedha vinavyoingizwa kwenye miradi ya utakatishaji fedha vinajulikana kisheria kama makosa tangulizi ambayo ni biashara ya dawa za kulevya, wizi, biashara ya ndani, ujambazi na kila kitu ambacho kitawaletea wahalifu fedha," alisema.

Hivyo ni matumaini yake kwamba washiriki wa mafunzo hayo watatekeleza kwa vitendo kile walichojifunza na kusambaza maarifa na ujuzi walioupata kwa maafisa wengine wa Mahakama ambao hawakuweza kuhudhuria mafunzo hayo.

 “Nawasihi, kama maafisa wa Mahakama, kuendelea kujikumbusha mfumo wa kisheria na masuala ya kiutendaji kuhusu utakatishaji fedha, ufadhili wa kigaidi na biashara haramu ya Wanyamapori na kusaidia taifa letu na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla katika kukomesha uhalifu huu wa kimataifa. Mafunzo haya yametufungua macho na hivyo ni lazima tuendelee kujikumbusha mara kwa mara kwani kujifunza ni mchakato wa maisha,” alisema.

Kwa mara nyingine tena alilishukuru Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na Kikundi cha Kupambana na Utakatishaji Fedha cha Mashariki na Kusini mwa Afrika-The Eastern and Southern Africa Anti-Money Laundering Group (ESAAMLG) kwa msaada wao wa kiufundi na kifedha kuelekea kutoa mafunzo hayo, ambayo yaliandaliwa kwa pamoja na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Alibainisha kuwa ushirikiano wao na IJA umezaa matunda kwa kuendesha mafunzo Septemba 2022 kwa kundi la awali la Mahakimu Wakazi 40 jijini Dodoma na sasa mafunzo hayo kwa washiriki 39 yaliyojumuisha Majaji 13 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakimu Wakazi 24 , Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya mmoja na Msaidizi wa Sheria ya Jaji mmoja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amiri Mruma akitoa hotuba ya kufunga mafunzo hayo.
Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo ya Kimahakama kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Elia Y. Baha akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwelo wakati wa kufunga mafunzo ya namna ya kushughulikia mashauri ya makosa ya kifedha.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo (aliyeshika kipaza sauti), akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wote (baadhi hawapo pichani).
Sehemu ya washiriki wa mafunzo wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo.
Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo.

 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni