Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kuhakikisha
wanawashirikisha wananchi kwenye mnyororo mzima wa utoaji haki.
Ametoa kauli hiyo leo
tarehe 15 Novemba, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo mawili ya
Mahakama ya Wilaya ya Mwanga na Mahakama ya Wilaya ya Same.
Mhe. Prof. Juma alisema
kuwa faida ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama itakuwa na tija ikiwa
utoaji haki utawashirikisha ipasavyo wadau na wananchi kwenye kujenga ubora,
ufanisi na uwazi.
“Mathalan, Mahakama
haitafanikiwa katika wajibu wake wa utoaji wa haki kwa wakati iwapo, kwa mfano Jeshi
la Polisi halitaweza kupeleleza mashauri ya jinai kwa haraka,” alisisitiza.
Aidha, Mhe. Prof Juma
alisema anaunga mkono mabadiliko ya sheria yaliyofanywa hivi karibuni kuzuia
Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwazuia watuhumiwa kabla ya upelelezi
kukamilika.
Jaji Mkuu alisema
marekebisho hayo yakitekelezwa ipasavyo suala la kuwepo kwa mlundikano wa
Mahabusu wanaosubiri upelelezi wa kesi zao kukamilika utaisha.
Aidha, Jaji Mkuu huyo
alisema mbinu ya kutumia usuluhishi katika kutatua migogoro ina faida ya kudumisha
udugu pamoja na kurudisha mahusiano ya kijamii na hata ya kibiashara.
Aliwataka viongozi wa
Mahakama za Wilaya za Mwanga na Same kuhakikisha kuwa huduma zao zinajumuisha
usuluhishi, utoaji wa elimu ya sheria na utaratibu wa kimahakama.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro Nurdin Babu aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa
miundombinu inayoendelea hapa nchini ambayo imetoa mazingira mazuri kwa
watumishi wake kutekeleza majumuku yao kwa ufanisi.
Aliwataka Wabunge
kuendelea kuiombea Mahakama kuongezewa bajeti yake ili iweze kuendelea na
jukumu lake la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya upatikanaji haki katika
mazingira ya karibu na rafiki.
Katika hatua nyingine,
Jaji Mkuu wa Tanzania ameishukuru Serikali kwa uwezeshaji ambao umewasaidia kwenye
tekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano uliboresha miundombinu ya
Mahakama mbalimbali hapa nchini.
“Leo hii tunashuhudia
matunda ya uwezeshwaji uliofanywa na Serikali, usimamizi na utekelezaji wa
Mpango wa Miaka Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu wa Mahakama
uliofanywa na watumishi wa Mahakama ya Tanzania,”alisema.
Alisema katika
utekelezaji wa Mpango Mkakati huo kwa ngazi ya Mahakama Kuu majengo mapya ya
Mahakama Kuu Musoma na Kigoma, kukamilika kwa ukarabati wa Mahakama Kuu Mbeya
na Mahakama Kuu Sumbawanga umefanyika.
Mhe. Prof. Juma alisema
katika kipindi cha 2016 hadi 2021 cha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka
Mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu wa Mahakama, Mahakama za Hakimu
Mkazi saba, Mahakama za Wilaya 28 na Mahakama
za Mwanzo 25 zilijengwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa majengo mawili ya Mahakama ya Wilaya ya Mwanga na Mahakama ya Wilaya ya Same. Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 15 Novemba, 2022 katika jengo la Mahakama ya Wilaya Mwanga. Viongozi wengine walioshuhudia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda( watatu kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu (wa pili kulia), Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Juliana Masabo (wa pili kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Ganriel (aliyeshika kipaza sauti).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni