Na Angel Meela-Mahakama, Arusha
Kanda mpya
ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Manyara iliyoanzishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kupitia Tangazo la Serikali Namba 632, 2022 ili kusogeza
huduma karibu na wananchi imeanza kufanya kazi rasmi na itatoa huduma zake ikiwa
katika jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara.
Makabidhiano
ya rasilimali watu na vitu yalifanyika jana terehe 15 Novemba, 2022 kati ya Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Joachim Tiganga na
Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo mpya, Mhe. John Kahyoza ambaye awali alikuwa Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza.
Kabla ya
kuanza kwa Kanda ya Manyara, kulifunguliwa Masjala ndogo katika Kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki Arusha ambayo ilikuwa chini ya Mhe. Tiganga. Tayari Masijala hiyo
imeshapokea mashauri 16 tangu ilipoanzishwa ambapo mashauri matano kati ya hayo
yamekwisha sajiliwa kwa njia ya kielektroniki na yataanza kusikilizwa, huku mengine
yakisubiri uwasilishwaji wa nyaraka ngumu na malipo.
Akizungumza
katika hafla ya makabidhiano hayo, Mhe. Tiganga alimkaribisha Jaji Mfawidhi Kahyoza
pamoja na Jaji mwingine wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Gladys Barthy ambaye
atahudumu katika Kanda ya Manyara ambapo ameahidi kuendelea kuwapa ushirikiano
na wakutosha pindi watakapohitaji.
Jaji
Mafawidhi huyo wa Arusha aliungana na Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda
hiyo, Mhe. Judith Kamala kuwapongeza Mahakimu wote wa Manyara kwa kazi nzuri ya
uondoshaji wa mashauri yaliyosajiliwa katika kipindi cha mwezi Agosti na
Octoba, 2022 kwa takribani asilimia 99 katika Mahakama zao. Aliwaomba watumishi
hao kuendelea kuongeza kasi katika utendaji kazi kama walivyokubaliana kwenye
kikao walichokifanya mwezi Julai jijini Arusha.
Mhe.
Tiganga akiwakabidhi wanachama wote wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania
(JMAT) Mkoa wa Manyara ambao alikuwa mlezi wao kwa Jaji Mfawidhi mpya ambapo
amewaeleza kuwa kama yeye alikuwa Paroko, basi sasa amewaacha kwenye mikono ya
Askofu kwani Jaji Khayoza ndiyo atakuwa mlezi wao mpya.
Katika
hafla hiyo, viongozi hao walipokea taarifa ya utendaji, rasilimali watu na vitu
ya Mahakama zote za Mkoa wa Manyara kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Mhe. Mariam Lusewa ambaye,
pamoja na mambo mengine, alisema wamejipanga kikamilifu kutoa ushirikiano kwa Majaji
hao na wanafurahi kuanza kupata huduma za Mahakama Kuu.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali kutoka ofisi ya Mwendesha
Mashtaka, Usatwi wa Jamii na Mawakili wa Kujitegemea katika makabidhiano hayo,
Mhe. Kahyoza aliwasihi kila mmoja wao kuwajibika katika maeneo yao ya kazi na
kuwa na lengo moja la kumhudumia wananchi ili waweze kupata haki zao kwa wakati.
"Watu
wenye lengo moja wakikaa pamoja hakuna jambo linaloharibika, lengo letu hapa
sote ni moja, kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki na wanaipata kwa wakati.
Sote tupo kwenye basi moja na tunasafiri safari moja, sasa abiria ni wale wale,
basi ni lile lile na safari ni ile ile, ila tu dereva ndiyo amebadilika,”
alisema.
Naye Mhe.
Barthy alipokua akiwasalimu watumishi na wadau hao amesema amefurahi kufika
Manyara na anawashukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na kwa ahadi ya
ushirikiano waliyoitoa.
Pamoja na
makabidhiano hayo, viongozi hao walipata nafasi ya kutembelea jengo zima la
Mahakama Kuu Manyara ambalo linabeba Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na
Mahakama ya Wilaya Manyara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni