Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Wananchi katika Wilaya 28
kati ya 139 Tanzania Bara wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma ya
Mahakama katika Wilaya zilizopo jirani.
Kauli hiyo imetolewa tarehe
15 Novemba, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati
wa hafla ya uzinduzi wa majengo mawili ya Mahakama ya Wilaya ya Mwanga na
Mahakama ya Wilaya ya Same.
Alisema kabla ya uzinduzi
huo Wilaya 111 za Tanzania bara zilikuwa zinapata huduma katika ngazi ya
Mahakama za Wilaya moja kwa moja.
Mhe. Prof. Juma aliongeza
kuwa katika Wilaya zote nchini, Wilaya zenye majengo yao ya Mahakama za Wilaya
zilikuwa ni 37, zilizobaki zimehifadhiwa katika majengo ya Serikali za Mitaa,
Ofisi za Wakuu wa Wilaya na nyingine zinatumia majengo ya kukodi.
Alisema juhudi zinazoendelea
kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania zitasaidia huduma za miundombinu
ya Mahakama za Wilaya kuwa bora hadi kufikia mwisho wa mwaka huu.
Mhe. Prof. Juma aliongeza
kuwa uzinduzi wa majengo ya Mahakama ya Same na Mwanga utafuatiwa na uzinduzi majengo
mengine 18 ya Mahakama za Wilaya ikiwemo jengo la Mahakama ya Wilaya ya Busega.
Alisema baada ya uzinduzi
huo Mwezi Desemba mwaka huu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania naye
atazindua majengo mapya ya Mahakama za Hakimu Mkazi Mpanda, Songwe na Lindi na
kumalizia na majengo ya Mahakama za Wilaya za Namtumbo (Ruvuma), Nanyumbu
(Mtwara) na Tandahimba (Mtwara).
Mhe. Prof. Juma alisema
pamoja na uboreshaji ndani ya Mahakama unaoendelea hapa nchini bado mahitaji ya
miundombinu ni makubwa ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Katika hatua nyingine,
Jaji Mkuu aliwataka maeneo yote ambayo yamepata bahati ya miundombinu hiyo
kuitunza ili yawe vitovu vya utoaji wa huduma bora kutoka kwa watumishi wa
Mahakama na kwa wadau katika mnyororo wa utoaji haki.
Mhe. Prof. Juma alisema hategemei
kuwa majengo hayo yajenge sifa ya ucheleweshwaji, mlundikano wa mashauri,
uahirishwaji wa mashauri pasipo sababu za msingi, vitendo vya rushwa au utovu
wa maadili.
Aidha Jaji Mkuu huyo
aliwataka wananchi kushiriki katika kulinda na kutunza miundombinu ya Mahakama
zilizopo na zinazojengwa kwa kuwa zimetokana na fedha kutoka katika kodi zao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(aliye piga magoti) akishiriki zoezi la upandaji miti mbalimbali mara baada ya hafla ya uzindizi wa majengo ya Mahakama za Wilaya ya Same na Mwanga.
(Picha na Tiganya Vincent).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni