Alhamisi, 17 Novemba 2022

MAJENGO MAPYA YA MAHAKAMA YAWE KITOVU CHA HUDUMA BORA KWA WANANCHI: JAJI MKUU

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Watumishi wa Mahakama nchini kuyatumia majengo mapya na ya kisasa ya Mahakama yanayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa kitovu cha huduma bora kwa wananchi.

Akizindua majengo ya Mahakama za wilaya za Mwanga na Same hivi karibuni, Jaji Mkuu aliwataka watumishi hao pamoja na wadau katika mnyororo wa utoaji haki kutotumia vituo hivyo kama sehemu ya ucheleweshwaji wa mashauri, mlundikano wa mashauri na vitendo vya rushwa na utovu wa maadili, badala yake watoe huduma bora kwa wananchi zinazolingana na uzuri wa majengo hayo.

“Ni maombi yangu kuwa wakati watumishi watakapokuwa wakifurahia mazingira bora ya kufanyia kazi za utoaji haki katika majengo haya, wakumbuke kuwa yametokana na fedha zilizotokana na kodi za wananchi hivyo, watoe huduma bora zinazolingana na ubora wa majengo hayo” alisema Jaji Mkuu.    

Aidha Jaji Mkuu aliwataka wananchi wanaofika mahakamani kutoogopa kuingia ndani ya majengo hayo mapya kutafuta haki zao kwa mujibu wa sheria. Alisema majengo hayo yanapaswa kuwa rafiki kwa wananchi wote na pia wananchi wategemee watumishi wa Mahakama wenye uchangamfu, bidii, weledi na wanaochukia vitendo vinavyokiuka maadili.

Kuhusu ushirikiano wa Mihimili katika shughuli za utoaji Haki, Jaji Mkuu alisema Mihimili yote mitatu ya dola haina budi kushirikiana na kuiwezesha Mahakama kutoa huduma ya utoaji haki iliyo bora, fanisi na iliyo karibu zaidi na wananchi.

Alisema Serikali ya Tanzania imetambua changamoto ya uhaba wa majengo ya Mahakama na imeazimia kuondoa upungufu huo. Aliongeza kuwa uthibitisho wa hilo ni kufanikiwa kwa mipango mikakati mizuri ya Mahakama na kuwa Serikali inatumia kodi inazokusanya na mikopo inayopata kusaidia kuboresha miundombinu ya Mahakama.

Jaji Mkuu alisema Serikali katika Mpango wake wa Maendeleo wa miaka mitano (2021/22-2025/26) imejumuisha ujenzi mkubwa wa miundombinu ya Mahakama ya Tanzania kama sehemu ya utekelezwaji wa Mpango huo. Alisema Mpango huo unatambua kuwa kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi ni sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi wa Tanzania

Alisema Mahakama kwa upande wake, kwa kutambua ukubwa wa changamoto za upatikanaji wa haki karibu na wananchi, iliandaa Mpango wa miaka mitano wa Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Mahakama wa mwaka 2016/17-2020/21) ulioweka vipaumbele na vigezo mahsusi vya kuhakikisha kuwa changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Hadi kufikia mwisho wa mwaka huu (2022) hali ya majengo yanayotoa huduma za Mahakama ya Wilaya itaimarika zaidi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa majengo 26 katika maeneo mbalimbali nchini. Baadhi ya majengo hayo ni pamoja na Mahakama za wilaya 23 zikiwemo za wilaya za Same, Mwanga, Busega, Namtumbo, Nanyumbu na Tandahimba, na Mahakama za Hakimu Mkazi tatu ambazo ni Katavi, Songwe na Lindi.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akihutubia wakati wa uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya za Same na Mwanga uliofanyika tarehe 15 Novemba, 2022 wilaya Mwanga mkoani Kilimanjaro.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni