Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekutana na Rais wa Mahakama inayoshughulikia migogoro na Katiba, wa Uturuki , Mhe .Muammer Topal, ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa Mahakama mbalimbali za nchi hiyo na kubadilisha uzoefu wa mifumo ya uendeshaji wa shughuli za kimahakama baina ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao wamefanya mazungumzo hayo, tarehe 18 Novemba,
2022 katika ofisi ya Jaji Mkuu iliyopo jijini Dar es Salaam, ambapo
walizungumzia utendaji kazi wa shughuli za mahakama ikiwemo upatikanaji wa Majaji
na Mahakimu, muundo wa Mahakama,nidhamu za maafisa wa Mahakama, uendeshaji wa
mashauri kwa njia ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Muundo wa
Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Rais huyo, alitoa uzoefu wa mfumo wa kimahakama wa nchi yake ambao
umegawanyika katika ngazi mbalimbali ambazo ni Mahakama ya Katiba, Mahakama ya
Utawala, Mahakama Kuu, Mahakama ya Madai, Mahakama ya Jinai Mahakama ya Kesi nyinginezo.
Alisema katika nchi yake kila kitu kinaendeshwa kwa mtandaoni
na haimlazimu mtu kufika mahakamani, hivyo mtu hufungua kesi mahali popote
alipo.
Rais huyo alisema kwa upande wa nchi yao Jaji anateuliwa
kutoka Mahakama ya Utawala. Alisema pia kuwa katika nchi yake hutatua mashauri
kwa njia ya usuluhishi, mbinu ambayo ni ya lazima kabla ya mwananchi kupeleka
suala lake mahakamani.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Juma aliuelezea
ujumbe huo kuwa Tanzania ina Mahakama ya
Rufaa, Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya na Mahakama
ya Mwanzo.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya teknolojia, Jaji Mkuu alisema
Mahakama ya Tanzania imewekeza zaidi katika matumizi hayo‘’Hivi sasa kesi
zinazofunguliwa mahakamani asilimia 100 zinafunguliwa kwa njia ya mtandao, na
tulisikiliza kesi nyingi kwa kutumia TEHAMA wakati Covid 19 kuliko kipindi
kingine, vifaa vya TEHAMA vilifungwa magerezani ili kuwezesha utumiaji huo.”
alisema Jaji Mkuu.
Kuhusu upatikananji wa viongozi wa Mahakama, Prof. Juma
alisema kwa upande wa Tanzania, Jaji
anapatikana baada kufanya kazi za kisheria au
Hakimu kwa kipindi cha miaka 10. Pia jina lake liwe limepitishwa
kwenye Tume ya Utumishi wa Mahakama. Hivyo majina yao yanapelekwa Tume ya
Utumishi ya Mahakama kwa ajili ya kushauriana na Rais ambaye ndiye anayeteua
kulingana na idadi inayotakiwa.
Akizungumzia kuhusu suala ya kutumia usuluhishi katika
kutatua migogoro, Jaji Mkuu alisema kwa upande wa Tanzania si jambo lazima, ila
huwa wanapenda kuwashauri wananchi kutatua migogoro yao kwa njia hiyo ambayo
inamanufaa makubwa kwa pande zote mbili zinazohusika.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akizungumza jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam na
Rais wa wa Mahakama inayoshughulikia migogoro
na Katiba wa Uturuki , Mhe .Muammer Topal, ambaye aliambatana na ujumbe wa viongozi
waandamizi wa Mahakama mbalimbali za nchi hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani wa kwanza (kushoto) akiwa na viongozi waandamizi wa Mahakama mbalimbali za nchi ya Uturuki wakati wa mazungumzo hayo. |
Rais wa Mahakama inayoshughulikia migogoro na Katiba wa Uturuki, Mhe. Muammer Topal (wa kwanza kulia aliyenyoosha mkono) akizungumza jambo kwenye mazungumzo hayo, mwingine ni Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mhe. Dtk.Mehmer Gulluoglu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, akimkabidhi picha wanyama Rais wa Mahakama inayoshughulikia migogoro na Katiba wa Uturuki, Mhe .Muammer Topal (kulia) baada ya kufanya mazungumzo kuhusu shughuli za Mahakama jana.
(Picha na Innocent
Kansha- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni