Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amehimiza Mtaala ulioandaliwa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuboreshwa ili uweze kutumika kwenye
mafunzo yatakayotolewa kwa Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama katika
kushughulikia mashauri ya watoto.
Mhe.
Chuma alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anafungua Warsha ya siku moja
iliyowaleta pamoja baadhi ya Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu na Wasaidizi wa
Kumbukumbu ili kujadili Mtaala huo ambao Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF– Tanzania) lilishiriki pia katika kuuandaa.
Msajili
Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuwasihi washiriki wa Warsha hiyo kutoa maoni ambayo
yatasaidia kupata Mtaala unaozingatia mambo muhimu yatakayowawezesha Wasaidizi
wa Kumbukumbu wa Mahakama katika mashauri ya watoto kutekeleza majukumu yao kwa
ufanisi na uweledi.
“Natambua
makarani mliopo hapa ni wabobevu katika eneo hili. Hivyo, kuweni huru na wazi
katika kuchangia sababu mna uzoefu mkubwa. Hivyo, ninawatakia majadiliano mema
katika kufanikisha azma hii,” Mhe. Chuma alisema.
Niimani
yake kuwa mapendekezo yao yataboresha Mtaala huo na kuwezesha mafunzo
yatakayotolewa kuwajengea uwezo Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama katika mashauri
ya watoto na kufikia adhima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na
jumuiya ya kimataifa ya kuhakikisha haki ya mtoto inalindwa.
Mhe.
Chuma aliwahakikishia washiriki wa Warsha hiyo kuwa Mahakama ya Tanzania
itaendelea kutekeleza vema jukumu lake la utoaji haki ikiwepo utoaji wa haki
mtoto kwa kuzingatia kanuni, taratibu, sheria na miongozo iliyopo
Aliwakumbusha
kuwa Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ni wadau muhimu katika utunzaji wa kumbukumbu
mbalimbali za Mahakama, ikiwemo zinazohusu mashauri ya watoto na ndio wanaoita
mashauri na kupanga Mahakama na pengine hata kukutana na Watoto hawa kabla hata
shauri halijaanza mahakamani.
Alisema Wasaidizi wa
Kumbukukumbu za Mahakama ndio Wadau wa kwanza wanaopokea nyaraka zote
zinazohusu Mashauri ya Watoto zinazoletwa Mahakamani na kwamba wao ndio
wanaotunza Kumbukumbu hizo na kwa sehemu kubwa ndio wanaoandaa baadhi ya
nyaraka hizo.
Alibainisha pia kuwa Wasaidizi
wa Kumbukumbu ndio wanafanya kazi kwa karibu na wadau wa mashauri ya watoto wakiwepo
Majaji na Mahakimu katika mashauri ya watoto mahakamani, hivyo, ni muhimu
watumishi hao wakapewa mafunzo ya namna bora ya utekelezaji wa majukumu yao
katika mashauri ya watoto ili kuwa na ufanisi katika uendeshaji wake.
(Picha na Ofisi ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni