Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Tume
ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na mikakati yake ya kujitangaza ambapo kesho
tarehe 21 Novemba, 2022 wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wataanza ziara katika mikoa
ya Shinyanga na Simiyu.
Katika
ziara hiyo itakayoanzia mkoani Shinyanga, wajumbe wa Tume watakutana na
watumishi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Shinyanga wakiwemo Mahakimu na
kufanya mazungumzo yanayohusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi na baadaye
watakutana na wadau wa utoaji haki wa mkoa huo kwa lengo la kuimarisha shughuli
za utoaji haki mkoani humo.
Aidha,
katika kutekeleza jukumu lake la usimamizi wa nidhamu na maadili ya watumishi
wa Mahakama ya Tanzania, Wajumbe ya Tume hiyo pia watapata nafasi ya kukutana na
wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya wakiwemo
wakuu mikoa na wilaya za mikoa ya Shinyanga na Simiyu ili kujadiliana namna ya
kuimarisha utendaji kazi wa kamati hizo.
Mkoani
Simiyu, wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pia watakutana na watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi, wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama
ngazi ya mkoa na wilaya pamoja na wadau wa utoaji haki mkoani humu katika
mikutano inayotarajiwa kufanyika Novemba 23 na 24 mwaka huu.
Wajumbe
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya
Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na
kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume
ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha Kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia
uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga mara baada ya kuwasili leo mkoani humo tayari kwa kuanza ziara ya Tume.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akisalimiana na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga mara baada ya kuwasili leo mkoani humo tayari kwa kuanza ziara ya Tume. Anayefuata ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mjumbe wa Tume Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akifuatiwa na Mjumbe wa Tume Mhe. Bundala Kalolo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni