Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Simiyu
Jaji
wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewataka watumishi wa
Mahakama ya Tanzania kuepukana na matendo yote yanayokiuka Maadili ili kuendelea
kujenga taswira nzuri ya Mhimili wa Mahakama.
Akitoa
mada kuhusu Muundo na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwenye Mkutano
wa Tume na Watumishi wa Mahakama jana mkoani Simiyu, Jaji Ndika alisema
Watumishi hao hawana budi kuepukana na matendo hayo kwa kuwa yatawaaibisha wao wenyewe
na pia yatachafua taswira ya Mahakama.
“Tuzingatie
pia kuwa jukumu tulilopewa la kutoa haki ni jukumu la kimungu na la kikatiba na
ni muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu,” alisema Jaji Ndika.
Aidha,
Jaji Ndika ametoa rai kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuzisoma, kuzielewa
na kuzifuata kanuni za maadili ya watumishi wa Mahakama ili wafahamu haki zao
na wajibu wao na kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisema kuna changamoto ya
watumishi kutofahamu haki na wajibu wao kwa kuwa hawasomi Sheria na kanuni za
maadili.
‘Natoa
rai kuwa ni vizuri kila mtumishi wa Mahakama asome kanuni za maadili na hasa
kanuni ya 45 mpaka 75 kwani kanuni hizi ndizo zina utaratibu mpya wa usimamizi
wa nidhamu. Utaratibu huu mpya ulianza kutumika Januari mwaka jana”,
alisisitiza.
Akizungumzia
kuhusu uamuzi unaotolewa na Tume kwa watumishi wanaokiuka maadili, Dkt. Ndika
alisema kwa upande wa Maafisa wa Mahakama/Mahakimu, uamuzi wa unaotolewa na
Tume ni wa mwisho na hakuna rufaa. Alisema kwa watumishi wengine wa Mahakama
wasio Maafisa wa Mahakama kama hawataridhika na uamuzi wa Tume wanayo nafasi ya
kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma na ngazi yao ya mwisho ni kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati
huo huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewataka
watumishi wa Mahakama kuzisoma kanuni za maadili na kuzizingatia kwa kuwa ni
kitu cha msingi katika maendeleo ya mtumishi yeyote wa Umma.
‘Nimesikitika
sana kuona watumishi hawazifahamu kanuni za maadili, huu ni ugonjwa ndani ya Utumishi wa Umma, usipopata
nafasi ya kuaminika na kuteuliwa unaanza kuwalaumu viongozi wako unasahau
kwamba ni lazima uzifahamu kanuni na kuzizingatia ili ufahamu haki na wajibu
wako ” alisema Mwanasheria Mkuu.
Kuhusu
kusimamia maadili, Kamishna Feleshi amewataka Mahakimu Wafawidhi kukutana na
watumishi walio chini yao mara kwa mara na kuwajengea uwezo wa kimaadili ili
kusaidia kuimarisha suala la maadili ndani ya Mhimili wa Mahakama.
Naye
Kamishna wa Tume hiyo, Wakili Msomi Mhe. Genoveva Kato
alihimiza watumishi wa Mahakama kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili
mema kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na nafasi kubwa ya kuendelea mbele zaidi
katika utumishi.
Aidha,
aliwataka watumishi wasio Maafisa wa Mahakama kutowakwaza Maafisa wa Mahakama
wanapotekeleza wajibu wao bali wawasaidie na kuwawezesha ili wananchi wapate
haki kwa wakati.
Kamishna
Kato pia alimpongeza Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Shinyanga Mhe. Matuma Kirati kwa
ubunifu wa kuunda kikosi maalum cha kushughulikia mlundikano wa mashauri na pia
watumishi wa kanda hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya utoaji haki.
Kwa
upande wake, Wakili Msomi Mhe. Kalolo Bundala amewataka
watumishi wa Mahakama kujilinda siku zote na kujiepusha na mambo yote yaliyo
kinyume na maadili mema ili kutoharibu taswira nzuri ya Mahakama.
“Kabla
ya kutenda jambo lolote, jiulize je litaendeleza taswira nzuri ya Mhimili wa
Mahakama?’. alisema Kamishna huyo.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara katika mkoa wa Simiyu ambapo wamekutana na watumishi wa Mahakama pamoja na wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya mkoa na wilaya.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika akitoa mada kuhusu Muundo na Majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wakati wa Mkutano wa Tume na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani Simiyu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni