Alhamisi, 24 Novemba 2022

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA INATHAMINI KAZI ZINAZOFANYWA NA KAMATI ZA MAADILI

 Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Shinyanga

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof Ibrahim Hamis amesema Tume yake inathamini kazi inayofanywa na kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya za kusimamia maadili ya Maafisa wa Mahakama.

Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya mkoani Shinyanga, Jaji Mkuu alisema kamati hizo ni daraja kati ya wananchi na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa ziko karibu zaidi na wananachi.

“Ninyi ndiyo mko karibu zaidi na wananchi, mnapokea malalamiko yao kuhusu masuala ya nidhamu na maadili ya Maafisa wetu wa Mahakama hivyo mnapaswa pia kuzifahamu changamoto za utoaji haki kwenye maeneo yenu”, alisema Jaji Mkuu.

Aidha. Jaji Mkuu alitoa wito kwa wajumbe wa kamati za Maadili kuisemea vizuri Mahakama ya Tanzania kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wakijenga na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

“Mfumo wa masuala ya maadili wa Tume ni shirikishi, wajumbe wa Tume wengi wao wako Dar es salaam, hawakutani na wananchi moja kwa moja ili kupokea changamoto za kimaadili lakini kupitia ninyi mnawezesha wananchi kufikisha malalamiko yao mbele ya Tume”, alisema.

Jaji Mkuu alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama inathamini taarifa zinazowasilishwa kwake kuhusu hali ya kimaadili kutoka maeneo mbalimbli nchini kwa kuwa kipimo cha maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya hutokana na taarifa zinazowasilishwa na kamati hizo.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kishapu Bw. Joseph Mkude akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Sophia Mjema amesema Serikali mkoani humo itaendeleza ushirikiano mkubwa uliopo kati yake na Mhimili wa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof Ibrahim Hamis akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na wilaya mkoani Shinyanga.   


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni