Alhamisi, 24 Novemba 2022

MACHO, MASIKIO KUELEKEA BUSEGA KESHO

Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania

Watanzania kote nchini kesho tarehe 25 Novemba, 2022 wanatarajia kushuhudia tukio kubwa na la kihistoria litakalofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye atazindua Mahakama za Wilaya 18 kwa mpigo kupitia Mahakama ya Wilaya Busega iliyopo mkoani Simiyu.

Tukio hilo litakaloonyeshwa mubashara na Televisheni ya Taifa ni mwendelezo wa mpango wa uongozi wa Mahakama ya Tanzania kuzindua jumla ya majengo ya Mahakama 26 hadi kufikia Disemba 2022.

Mahakama hizo 18 za Wilaya zitakazozinduliwa kwa pamoja zimejengwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kufuatia mkopo wa masharti nafuu uliotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mahakama.

Kati ya majengo hayo, 15 yalihusu ujenzi wa Mahakama mpya katika Wilaya ambazo hazikuwa na huduma za Mahakama ya Wilaya na tatu ni Mahakama za Wilaya zilizokuwa na majengo chakavu.

Mahakama za Wilaya zinazotarajiwa kuzindiliwa siku hiyo ni Nyang’ale, Mbongwe, Kaliua, Uvinza, Kakonko, Buhigwe, Kyerwa, Misenyi, Kilombero, Mvomero, Gairo, Songwe, Butiama, Rorya, Tanganyika, Itilima, Busega na Mkinga.

Ujenzi wa miradi hiyo mbayo ipo katika Mikoa tofauti hapa nchini umezingatia mahitaji ya kisasa kwa wadau wa mnyororo wa utoaji haki ambapo zipo ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii, miongoni mwao, huku watu wenye mahitaji maalum na watoto wakiwekewa vyumba maalumu vya kutumia wakiwa mahakamani.

Kuzinduliwa kwa majengo hayo katika Wilaya hizo 18 kutaongeza ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi kwani majengo hayo yana mzingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia. Huu ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano (5) wa 2020/21-2024/25 katika nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.

Halfa ya uzinduzi huo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi waandamizi mbalimbali wa Mahakama, Serikali na Bunge wakiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumaro, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt. Yahya Nawanda na Wabunge.

Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Wilaya ya Busega na Wilaya za jirani wanaombwa kujitokeza katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Busega kushuhudia uzinduzi huo ambao ni ishara ya kuwepo mabadiliko makubwa ya  uboreshaji wa utoaji huduma za Mahakama nchini.

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mahakama hizo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, atakuwepo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumaro, anatarajiwa kuhudhuria.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, atakuwepo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Mahakama, atakuwepo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni