Na Festo Sanga-Mahakama, Kigoma
Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji katika Mkoa wa Kigoma hivi karibuni liliendesha mafunzo
kuwajengea uwezo kinadharia na kwa vitendo watumishi wa Mahakama ya Tanzania,
wateja na watoa huduma za ulinzi na usafi kuhusu uokoaji na uzimaji moto.
Akifungua
mafunzo hayo kwa washiriki 42 wakiwemo watumishi kutoka Mahakama Kuu, Mahakama
ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ya Kigoma, Mtendaji wa Mahakama Kuu
Kigoma Bw. Moses Mashaka alisema Jeshi hilo limelenga kuwapa ujuzi wa kujikinga
na kupambana na ajari za moto ili kuepusha au kupunguza athari zinazoweza
kutokea ikiwa janga hilo litatokea.
Aidha
aliwakumbusha washiriki wote kuzingatia mafunzo watakayoyapata na kuhakikisha
wanajisajili kila mara wanapokuwa ofisini
kwenye mashine maalumu ya kurekodi mahudhurio ili kuwa na taarifa sahihi
za idadi ya wanaokuwepo ndani ya jengo
ikiwa ni hatua za awali za uokoaji kama litatokea janga lolote.
“Tumeandaa
mafunzo haya kwa gharama ili muweze kutumia vyema vifaa na mifumo iliyopo
katika majengo kujikinga, kujiokoa na kuokoa mali za ofisi dhidi ya majanga ya
moto na mengine yanapotokea, hivyo kuepusha au kupunguza madhara yanayoweza
kutokea” alisema Bw. Mashaka.
Naye
Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji Bahati Salumu ambaye alikuwa mwezeshaji
wa mafunzo hayo aliwaeleza washiriki kuhusu mifumo mbalimbali iliyomo katika
jengo mahususi kwa ajili ya kujikinga na kujiokoa dhidi ya majanga ya moto na majanga mengine.
Alitaja
baadhi ya mifumo ikiwemo vigunduzi moshi, vizima moto, alama za njia za dharura
na eneo maarufu kama “Refugees Area”au kitaalamu likiitwa “Balcon” ambalo
hutumika kwa watu waliozingirwa na moto ili waokolewe.
Aidha,
katika mafunzo hayo, washiriki walikumbushwa juu ya namna ya kuukabili moto kwa
kutumia vifaa vya kuzimia moto vilivyopo katika mazingira mbalimbali vikiwemo mchanga
mkavu, matawi ya miti mibichi, mitungi ya gesi ya kuzima moto (fire
extinguishers), Blanketi maalum (fire blanket) na mfumo maji ya kuzima moto kwa
mpira (horse reel).
Mafunzo
hayo ni utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha usalama wa watumiaji wa jengo na
mali za ofisi na pia ni takwa la kisheria kupitia Kanuni Na.6 (1) (c) ya Kanuni
za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji za mwaka 2008 kuhusu kuwezeshwa kimafunzo juu
ya tahadhari za kuchukuliwa na watumiaji wote wa jengo katika jitihada za
kupambana na majanga ya moto.
Mshiriki wa Mafunzo kutoka Kampunzi ya Ulinzi ya Suma JKT, Bi Christa Samson akiwa tayari amefanikiwa kuzima moto kwa vitendo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni