Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA),
Mhe. Dkt. Paul Kihwelo jana tarehe 30 Januari, 2023 alifungua mafunzo kwa
Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliteuliwa kushiriki kwenye programu ya majaribio
ya namna bora ya kujengeana uwezo wa kiushauri kwa Majaji na Mahakimu hasa
wakati wa kuamua mashauri bila kuathiri uhuru wa Mahakama “Pilot Mentorship
Programme”.
Akizungumza
katika hafla fupi ya ufunguzi wa mafunzo hayo uliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano ulipo jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma, Mhe. Dkt.
Kihwelo alisema mafunzo hayo yanatokana na matunda ya ushirikiano baina ya Mahakama
ya Tanzania na Mahakama ya Mzunguko ya Uingereza na Wales kubuni mpango wa
majaribio wa namna ya kujengeana uwezo kishauri ili kuboresha utendaji kazi na
kuongeza ufanisi wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri kwa Maafisa wa Mahakama.
“Kupitia
mafunzo haya ya na namna bora ya kujengeana uwezo wa kiushauri kwa Majaji na
Mahakimu tutakubaliana namna ya uandaaji kitabu cha Mwongozo utakao tumika
katika shughuli za namna ya kuanzisha mahusiano kushauriana kwa njia rasmi na
zisizo rasmi ‘Mentor & Mentee Relationship’ wakati wa kuamua mashauri na
migogoro inapowasilishwa Mahakamani” alisema Jaji Kihwelo
Mhe.
Dkt. Kihwelo alisema program hiyo itategemea zaidi ushirikishwaji wa uzoefu na
weledi mkubwa walionao Majaji hao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku
hasa katika eneo la kutatua migogoro ama mashauri yanayolenga kupambana na
rushwa kubwa zenye thamani ya kuanzia milioni 200 na kuendelea kwa ustawi wa
Taifa.
“Program
hii msingi wake utazingatia uhuru wa Mahakama kwa asilimia mia moja katika
kufanya maamuzi ‘Mentorship programme’ haitamaanisha mshauriwa anapaswa kufuata
yale yote aliyoelekezwa na mshauri katika kufikia maamuzi kama msingi wa
maamuzi yake juu ya jambo fulani lililopo mbele yake. Programu hii inalenga kuwajengea
uwezo Majaji na Mahakimu wa namna bora ya kuongeza ufanisi na weledi kupitia
uzoefu walionao wakati wa kutoa maamuzi ya kimahakama”, alisisitiza Jaji Dkt.
Kihwelo.
Mhe. Dkt. Kihwelo alisema kupitia Programu hiyo itakuwa ya msaada mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na kutoa matokeo chanya kwa maendeleo ya kazi kwa maafisa wa Mahakama. Kupitia forumu hiyo akawashauri Majaji kuchangia mawazo yao kwa kutumia uzoefu mkubwa walionao ili kufanikisha mwongozo bora wa programu ya ushauri.
Mafunzo
kama hayo shabaha yake kubwa ni kutoa msaada, kwatia moyo na kuwapatia mwongozo
Maafisa wa Mahakama wale ambao hawakupata bahati ya kushiriki moja kwa moja
programu ya mafunzo ya ‘Mentorship programme’. Majaji waliohudhuria mafunzo
watatumika kutoa elimu hiyo na kuwajengea uwezo Maafisa wengine katika maeneo
yao ya kiutawala
Programu
itaangazia maeneo ambayo yanaathirika na kugubikwa kwa kiwango kikubwa na
vitendo vya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kama vile Dar es salaam, Mwanza,
Dodoma, Arusha na Mbeya. Takwimu za mwezi mei, 2022 zinaonyesha kuwa mashauri 147 ya makosa
hayo yanayoendelea katika Mahakama za Hakimu Mkazi katika miji tajwa, makosa 21
ni ya mtandao mkubwa wa makosa ya rushwa na yamebainishwa na mtandao wa Programu
Endelevu wa Mapambano ya kuzuia Vitendo vya Rushwa Tanzania (BSAAT).
Jaji Dkt. Kihwelo alihitimisha kwa kuwashukuru wabia waliowezesha kufanikishwa kwa programu hiyo ambao ni Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania na Ofisi ya Maendeleo ya Jumuiya ya Madola, kupitia Programu yake endelevu ya kupambana na Vitendo vya Rushwa Tanzania “The British High Commission (Foreign, Commonwealth & Development Office – FCDO through the Building Sustainable Anti – Corruption Action in Tanzania (BSAAT)”.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (aliyesimama) jana tarehe 30 Januari, 2023 alifungua mafunzo kwa Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania (hawapo pichani) waliteuliwa kushiriki kwenye programu ya majaribio ya namna bora ya kujengeana uwezo wa kiushauri kwa Majaji na Mahakimu, kongamano hilo la siku 3 lilifanyika katika jijini Dodoma katika Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Shule ya Sheria kwa Vitendo ''Law School of Tanzania" Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (wa kwanza kushoto) na Mkufunzi na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Mzunguko ya Uingereza na Wales, Mhe. HH Nic Madge.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni