Na Faustine Kapama, Mahakama-Manyoni
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 30
Januari, 2023 amezindua Mahakama za Wilaya tano mpya kwa awamu moja, hivyo kuandika
historia nyingine kwenye utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama katika kusogeza
huduma za utoaji haki karibu na wananchi.
Akizungunza
katika tukio hilo la uzinduzi wa Mahakama za Wilaya Manyoni, Kilindi, Bunda,
Rungwe na Sikonge lililorushwa mubashara kupitia Vituo vya Channel 10 na ITV kutoka
katika Mahakama ya Wilaya Manyoni, Mhe. Siyani amewasihi watumishi wote nchini kuijengea
heshima Mahakama kwa kuchapa kazi na kuepuka viashiria vyote na harufu za
rushwa.
“Ni vyema
watumishi wa Mahakama mfahamu kuwa huduma mbaya au zilizo chini ya kiwango
ndizo zilizotufikisha mahali ambapo watu wanatutuhumu bila ushahidi. Matendo na
kauli zetu zimewafanya tunaopaswa kuwahudumia kuwa na hisia mbaya dhidi yetu.
Sasa ni wakati wa mabadiliko,” amesema.
Jaji
Kiongozi ameeleza kuwa wakati serikali na Mahakama zinaboresha miundombinu na
maslahi hatua kwa hatua, watumishi wanaowajibu wa kuwa mfano mzuri kwa umma na wanaoaminika,
wanaochapa kazi, wazalendo kwa nchi yao na wanaojua nini wanapaswa kufanya.
“Tunao
uwezo wa kuibadili hali yetu kutoka kwenye kutoaminiwa hadi kuaminiwa sana.
Niwaombe viongozi wa Mahakama kwenye kila ngazi ya Mahakama, kusimamia
mabadiliko haya yanayoanzia kwenye fikra na mitazamo yetu maana haya ndiyo
mabadiliko ya kweli,” amesema.
Mhe. Siyani
amebainisha kuwa uzinduzi wa majengo hayo matano ya Mahakama za Wilaya umetanguliwa
na uzinduzi mwingine wa majengo 24 ya Mahakama za Wilaya na matatu ya Mahakama
za Hakimu Mkazi katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
“Haya ni
mapinduzi makubwa ya kihistoria kwa Mahakama ya Tanzania na nchi yetu kwa
ujumla. Kwa hiyo uzinduzi wa majengo haya matano na mengine takribani 27 ni
wazi umesogeza huduma karibu zaidi na wananchi na hili ndilo lengo la Mahakama,”
amesema.
Jaji
Kiongozi amesema kuwa ujenzi wa majengo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango
Mkakati wa Mahakama kuimarisha upatikanaji haki kwa kuboresha miundo mbinu na katika
kutekeleza mkakati huo, Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya
Miundombinu ya Mahakama (2016-2021) uliandaliwa ili kuboresha mazingira ya
utoaji haki na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Kwa
mujibu wa Mhe. Siyani, Mpango uliainisha Wilaya 104 ambazo mwaka 2016, zilikuwa
zinahitaji ujenzi wa majengo mapya ya Mahakama za Wilaya zikiwemo hizo ambazo amezizindua.
Amesema katika utekelezaji wa Mpango huo, uboreshaji wa miundombinu ya majengo
ya Mahakama umeendelea kutekelezwa.
“Hadi
tarehe ya leo, tuna jumla ya majengo mapya 84 ambayo yamejengwa nchi nzima na
majengo matatu yaliyokarabatiwa. Majengo mapya 84 yaliyojengwa ni pamoja na Mahakama
Kuu saba, Mahakama za Hakimu Mkazi nane, Mahakama za Wilaya 46 na Mahakama za
Mwanzo 23, wakati majengo yaliyokarabatiwa ni Mahakama Kuu mbili na Mahakama ya
Hakimu Mkazi moja,” amesema.
Hafla
hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, Serikali na
Bunge. Baadhi ya viongozi wa Mahakama waliohudhuria hafla hiyo ni Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu, Jaji wa Mahakama
Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Adam Mambi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Prof. Elisante Ole Gabriel na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Wilbert Chuma.
Kwa upande
wa Serikali alikuwepo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geofrey Pinda, Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba na Wakuu wa Wilaya, huku Bunge likiwakilishwa
na Mbunge wa Manyoni Mashariki, Mhe. Dkt Pius Chaya, Mbunge wa Manyoni
Magharibi, Mhe. Yahana Masale na Mbunge wa Singida Mashariki, Mhe. Miraji Mtaturu.
Akizunguza
wakati anamkaribisha Jaji Kiongozi kuzungumza na Watanzania, Mhe. Mdemu alieleza
kuwa kabla ya ujenzi huo wananchi wa Manyoni walikuwa wanapata huduma za
kimahakama sehemu finyu na isiyoridhisha, hivyo wamefarijika na kujivunia uwepo
wa jengo hilo.
“Jengo
hili litahudumia wananchi takribani 495,016 kwa mujibu wa sensa ya watu na
makazi ya mwaka 2022 waliotawanyika katika Kata 32 na Vijiji 126 kwa Halmashauri
za Manyoni na Itigi. Jengo hili litatumiwa na Mahakama mbili, Mahakama ya
Wilaya Manyoni na Mahakama ya Mwanzo Manyoni Mjini,” alisema.
Jaji
Mfawidhi huyo alisema kuwa Mahakama itakuwa inafanya kazi katika mazingira
yanayolinda hadhi kama Mhimili. Alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi
kulitumia jengo hilo katika kutatua migogoro iliyoshindikana.
Kwa kufanya
hivyo, alisema, wataendeleza kauli mbiu ya maadhimishio ya Wiki na Siku ya Sheria
mwaka 2023 ambayo inahusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
katika kukuza uchumi endelevu; wajibu wa Mahakama na wadau.
“Hivyo,
siyo lazima kila mgogoro uletwe mahakamani kwa vile kuna jengo zuri, iletwe
migogoro pale tu njia za usuluhishi zinaposhindikana,” alisema na kuahidi kulitunza
jengo hilo ili lidumu kuweza kuhudumia vizazi na vizazi katika Wilaya hiyo.
Kwa upande
wake, Mhe. Pinda aliwaeleza wananchi kuwa Serikali imeelekeza ifikapo mwaka
2026 kujengwa Mahakama za Mwanzo katika makao makuu yote ya Tarafa na Wilaya
zote zitakuwa na majengo mapya ya
Mahakama za Wilaya kwa zile zenye uhitaji, huku kila Mkoa ukiwa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi.
Naibu
Waziri huyo aliwasihi wananchi wa Manyoni kulitumia jengo hilo kutafuta haki na
siyo vinginevyo, huku akiwahimiza watumishi wa Mahakama watakaohudumu mahakamani
hapo kulipenda na kulitunza.
Naye Mkuu
wa Mkoa wa Singida aliwasihi watumishi katika Mahakama hiyo kutoa huduma bora
kwa wananchi inayolingana na uzuri wa jengo hilo. “Tunapofanya kazi hii kubwa
ya kuboresha Mahakama na miundombinu iendanane na kutoa huduma bora kwa
wananchi wetu, wananchi wetu wapate haki kwa wakati,” alisema.
Jaji
Kiongozi aliwasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Manyoni majira ya saa
3.30 asubuhi hivi na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa Mahakama na baadae
kuelekea katika sehemu maalumu iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kupata taarifa
ya ujenzi wa majengo hayo matano.
Baada ya
kupokea taarifa hiyo kutoka kwa Mhandisi Fabiani Kwegilwa, Mtendaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha alimwongoza Jaji Kiongozi kwenda kukagua
jengo la Mahakama ya Wilaya Manyoni kabla ya kukata utepe maalumu na kufungua
pazia kuashiria uzinduzi wa Mahakama hizo tano za Wilaya.
Mhe. Siyani
baada ya uzinduzi huo alielekea jukwaa kuu pamoja na viongozi wengine na
baadaye Wimbo wa Taifa ulipigwa kabla ya mshereheshaji Mkuu wa shughuli hiyo,
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillar Sarwatt kuruhusu vikundi
mbalimbali vya burudani, ikiwemo kwaya ya Mahakama ya Tanzania, maarufu Ng’aring’ari,
kuwatumbuiza wananchi.
Baada ya shughuli ya uzinduzi huo, Jaji Kiongozi pamoja na viongozi wengine wa Meza Kuu walipata nafasi ya kupanda miti katika maeneo ya Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mahakama za Wilaya Manyoni, Kilindi, Bunda, Rungwe na Sikonge katika hafla iliyofanyika leo tarehe 30 Januari, 2023 katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Manyoni. Picha chini, Jaji Kiongozi (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wakipiga makofi baada ya kufunua pazia maalumu kwa ajili ya uzinduzi huo.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama wakifuatilia matukio katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama hizo.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama (juu) na wananchi (chini) wakifuatilia matukio mbalimbali katika hafla hiyo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akiwasili katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya Manyoni kwa ajili ya uzinduzi. Picha chini akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia).
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Mhandisi Fabiani Kwegilwa (aliyeshika kipaza sauti) kuhusu ujenzi wa Mahakama hizo. Picha chini Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (kulia) akimwongoza Jaji Kiongozi kwenda kukagua moja ya majengo ya Mahakama hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni