Na Tiganya Vincent-Mahakama -Manyoni
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Watumishi
wa Mahakama kufanya kazi kwa ushindani kama ilivyo kwenye sekta
binafsi wakati wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo tarehe 30 Januari 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama
za Bunda, Kilindi, Sikonge, Manyoni na Rugwe iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama
ya Wilaya Manyoni.
“Ni
lazima sasa hivi, kama Mahakama inataka kujenga imani kwa wananchi watumishi
wake washindane na sekta binafsi kwa utoaji wa huduma bora. Watumishi wa
Mahakama hawapaswi kujisifu kwa majengo mazuri yanayoanza kuonekana sasa hivi
kote nchini, bali wanapaswa kujisifu kwa kutoa huduma bora,” amesema.
Amewahimiza
watumishi katika majengo hayo mazuri kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia
uzalendo na weledi wakati wanapotoa huduma.
“Watumishi
wanapaswa kujisifu kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na hawapaswi kujisifu kwa
kuwa na majengo bora,” amesema na kuongeza kuwa watumishi wanatakiwa kuwa
kitovu cha utoaji wa huduma bora kwa umma,” amesisitiza.
Mhe.
Siyani amewataka watumishi wa Mahakama kutobweteka kwa kuona majengo mazuri
bali wasaidie katika kujenga imani kwa wananchi ili waweze kuondokana na fikra
ya changamoto walizokutana nazo siku za nyuma.
Ameongeza kuwa, ni vema wakahakikisha wanaokwenda mahakamani kutafuta haki, wanapata
haki kwa haraka, katika mazingira yasiyo na urasimu wala harufu ya
upendeleo ikiwa ni pamoja na wadaawa kuamini kuwa mchakato
mzima wa usikilizwaji wa mashauri umefuata sheria zilizopo,
kanuni na taratibu.
Mhe.
Siyani amesema kwa watumishi wa Mahakama, kazi kubwa iliyo mbele
yao baada ya kujengewa majengo hayo mazuri na ya kisasa, ni
kuwahudumia wananchi hata wakishindwa waamini kuwa wameshindwa kwa
haki.
Amesema
hilo linawezekana ikiwa kila mmoja wao atakuwepo sehemu yake ya kazi
kwa saa zote za kazi, atafungua uso wake na atatoa huduma bila
kunung’unika wala kuonyesha kutaka chochote cha ziada kutoka kwa wadaawa.
Aidha
Jaji Kiongozi huyo aliwaomba wadau wanaofanya kazi katika
majengo ya Mahakama nao kuweka kipaumbele katika utoaji huduma bora
kwani wananchi hawatatofautisha kazi za watumishi wa Mahakama na
wafanyakazi waliopo katika majengo hayo.
“Kwa hiyo
kwa wadau wetu naamini yapo mazuri mtakayojifunza kwa kuchangamana na watumishi
wa Mahakama katika jengo moja. Rai yangu kwenu ni kuwa igeni mazuri ya Mahakama
na inapobidi basi saidieni kufichua maovu kwa nia ya kujenga lakini na ninyi
wenyewe muwe vinara na mabalozi wazuri wa haki,” amesema.
Amesema majengo
mapya yamezinduliwa, lazima yawe kitovu cha utoaji huduma
bora kwa wananchi na kwamba hudumu zilizokusudiwa zitatolewa kwa weledi, uadilifu na wanataka
mabadiliko kwa mashauri yao kusikilizwa na haki kutolewa kwa haraka.
Mhe.
Siyani ameongeza kuwa wananchi wanataka mazingira yanayozunguka mfumo wa
kutolea haki yawe rafiki, yasiyogubikwa na urasimu wala harufu ya rushwa.
Katika picha ni sehemu ya Watumishi wa Mahakama, Wageni waalikwa pamoja na wananchi waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Wilaya Manyoni wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni