Na Faustine Kapama-Mahakama, Arusha
Mtaalamu wa Manunuzi kutoka Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE), Bw. Jackson Musiba ameisihi Kamati ya Tathmini iliyochaguliwa
kuchambua maombi ya Wazabuni 138 kwenye miradi mipya ya Mahakama ya Tanzania
kuzingatia uadilifu na usiri wa hali ya juu wanapotekeleza jukumu hilo ili
kufikia uamuzi sahihi.
Bw. Musiba
ametoa ushauri huo leo tarehe 4 Januari, 2023 katika Ukumbi wa Kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki jijini hapa alipokuwa anawasilisha mada katika siku ya pili ya
mafunzo ya siku tatu ya namna ya kufanya tathmini za zabuni za wataalam washauri
wa usanifu majengo na usimamimizi wa miradi ya ujenzi.
Amewaeleza
watumishi hao wa Mahakama kutoka maeneo kadhaa nchini wenye kada mbalimbali kuwa
kazi wanayoenda kuifanya ni muhimu ambayo itaacha alama katika historia nzima
ya Mahakama ya Tanzania, hivyo hawana budi kuongeza umakini wanapotekeleza jukumu
hilo waliloaminiwa kulifanya.
“Tujitahidi
kufanya uamuzi ambao ni sahihi. Tuongeze umakini kwenye kazi hii ili tuisaidie
nchi yetu. Kamati za Tathmini huwa zinatafutwa sana na makampuni, nawaomba
msiingie kwenye mtego wao wa aina yoyote. Tekelezeni wajibu wenu kwa kuzingatia
uadilifu na kutunza siri,” amesema.
Kadhalika,
Bw. Musiba amewaomba watumishi hao wanapotekeleza jukumu walilopewa kujiamini,
huku akiwakumbusha kuwa kuna gharama hasi kwa wao kuwa mawakala wa makampuni
kama wataamua kujiingiza kwenye mtego huo.
“Nawaomba
mzidishe umakini kwenye kazi hii, kama kuna ujanja ujanja hapa siyo mahali
pake. Naomba muelewe kuwa kuna maslahi ya nchi kwenye majengo yatakayojengwa.
Tuonyeshe ubora kwenye uamuzi tutakaofanya ili tuisaidie nchi yetu,” alisema.
Mtaalamu
huyo amewapitisha watumishi hao kwenye vipengele kadhaa muhimu wanavyoenda
kufanyia kazi, ikiwemo kuzingatia jukumu kuu na uzoefu wa miaka wa kampuni,
uwezo wa kiufundi na usimamizi wa kampuni na sifa na uzoefu wa wataalamu muhimu
katika kampuni inayohusika.
“Msije na
mawazo wengine, zingatieni vipengele hivi muhimu. Nyinyi ndio mnaoenda kutoa
uamuzi kwa Wazabuni walioomba kazi. Ebu fikiria utajisikiaje kama jengo ambalo wewe
umehusika kupitisha uamuzi likianguka baada ya miaka mitano, sita ijayo.
Tuongeze umakini,” alisema.
Mahakama
ya Tanzania, kupitia Kitengo cha Maboresho, imeandaa mafunzo maalumu kwa
watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo Wahandisi, Wasanifu majengo, Maafisa
Ugavi, Mahakimu, Wasajili, Wahasibu, Wachumi na Watakwimu kuwajengea uwezo
katika masuala yanayohusu ufanyaji wa tathmini za zabuni.
Hatua
hiyo inafuata baada ya kupata maombi 138 kutoka kwenye makampuni ambayo
yanataka kutoa ushauri kuhusu masuala ya usanifu majengo pamoja na usimamizi wa
miradi ya ujenzi.
Baada ya mafunzo hayo, Kamati hiyo ya Tathmini itajichimbia kwa siku kadhaa kufanya zoezi la tathmini kujua wazabuni wapi wanafaa kufanya kazi hizo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni