Jumamosi, 14 Januari 2023

MAHAKAMA YA MAKOSA YA RUSHWA, UHUJUMU UCHUMI YANUKIA ZANZIBAR

Na Faustine Kapama-Mahakama

Viongozi waandamizi wa Mahakama Kuu Zanzibar jana terehe 13 Januari, 2023 walifanya ziara katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi.

Katika ziara hiyo, viongozi hao ambao ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. Kai Mbaruk na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mhe.  Valentina Katema, walikutana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Divisheni hiyo, Mhe. Elinaza Luvanda, Naibu Msajili, Mhe. Magdalena Ntandu na Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Masalu Kisasila.

Viongozi hao walieleza lengo la ziara yao ambayo ni kujifunza mambo mbalimbali ili nao waweze kuanzisha Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi katika Mahakama Kuu ya Zanzibar. Baadaye viongozi hao walipokea taarifa fupi iliyokuwa imeandaliwa na Divisheni hiyo.

Katika taarifa hiyo, Mhe. Ntandu aliwaeleza viongozi hao kutoka Zanzibar kuwa Mahakama hiyo ni moja kati ya Divisheni nne maalum za Mahakama Kuu ya Tanzania zilizoanzishwa kwa sababu mahsusi za utoaji haki na mazingira bora ya kuvutia uwekezaji katika kukuza na kujenga uchumi nchini.

“Lengo kuu ni kuharakisha suala zima la utoaji wa haki ili kuvutia na kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji kiuchumi nchini, kuongeza imani kwa wawekezaji, kujenga na kuinua uchumi imara wenye kuhimili ushindani na hatimaye kuleta maendeleo ya jamii nchini,” alisema.

Naibu Msajili huyo alibainisha kuwa Divisheni hiyo ilianzishwa mwezi Julai 2016 chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Sheria Na.3 ya 1984, Sura ya 200 ya Sheria za Nchi kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Namba 3 ya 2016).

Alieleza kuwa Mahakama hiyo imepewa mamlaka ya kusikiliza mashauri ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi ambayo thamani yake au kiwango cha fedha ni kuanzia shilingi bilioni moja za Kitanzania na kuendelea na ina mamlaka pia ya kusikiliza makosa yote yaliyoorodheshwa katika Jedwali la Sheria ya Uhujumu Uchumi yanayoangukia katika vifungu vya sheria mbalimbali zilizopo kwenye jedwali hilo bila kujali thamani au kiwango cha fedha.

“Mahakama hii inayo Masijala Kuu moja iliyopo Dar es Salaam na Masijala zingine ndogo zilizoko kila penye Kanda ya Mahakama Kuu ambazo ni Dodoma, Morogoro, Tanga, Mwanza, Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma, Bukoba, Mbeya, Arusha, Moshi, Mtwara, Songea, Iringa, Musoma na Tabora,” Mhe. Ntandu alisema.

Naibu Msajili huyo wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwaeleza viongozi hao kutoka Zanzibar kuwa Mahakama hiyo inapokea na kuendesha mashauri nchi nzima kuanzia Masijala Kuu isipokuwa kwa mashauri ya maombi ya dhamana ambayo husikilizwa na kuamuliwa kwenye Kanda husika.

Alibainisha pia kuwa usajili wa mashauri yote katika Divisheni hiyo hufanyika kwa njia ya mtandao (Electronic filing) na taarifa zote za shauri huingizwa kwenye mfumo wa JSDS 2 na kuendelea kuhuishwa kila wakati. Hata hivyo, alisema, kufuatia maboresho yanayoendelea kufanyika katika uendeshaji wa shughuli za Mahakama, hivi sasa Divisheni imeanza kutumia mfumo wa kuendesha mashauri bila kutumia karatasi (Paperless Case Management System).

“Mashauri yanayosajiliwa katika Divisheni hii ya Mahakama Kuu yanaendeshwa kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na Gazeti la Serikali Namba 267 la Mwaka 2016. Kwa mujibu wa kanuni hizi ukomo wa muda wa kusikiliza mashauri katika Divisheni hii ni kipindi kisichozidi miezi tisa tu tangu kuwasilishwa kwa taarifa ya mashtaka,” Mhe. Ntandu alisema.

Alisema hadi sasa Divisheni imefanikiwa kumaliza mashauri 706 ya uhujumu uchumi na maombi ya dhamana, hivyo kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utatuzi wa migogoro kwenye jamii na kuleta utulivu na amani.

Viongozi waandamizi wa Mahakama Kuu Zanzibar ambao ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. Kai Mbaruk (wa pili kulia) na Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mhe.  Valentina Katema (wa kwanza kulia) wakiwa pamoja na wenyeji wao, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda (katikati), Naibu Msajili, Mhe. Magdalena Ntandu (wa pili kushoto) na Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Masalu Kisasila (wa kwanza kushoto).

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. Kai Mbaruk (kulia) akisalimiana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda.
Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mhe.  Valentina Katema akisalimiana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Bw. Kai Mbaruk akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kukukutana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda ofisini kwake. 
Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mhe.  Valentina Katema (kulia) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Elinaza Luvanda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni