Na Tiganya
Vincent-Mahakama –Katavi
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Siyani tarehe 18 Januari 2023 atakuwa mgeni rasmi katika hafla za
uzinduzi wa majengo matatu ya Mahakama za Hakimu Mkazi.
Uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya jengo
jipya la Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi. Majengo yatakayozinduliwa siku hiyo
ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Lindi na Songwe ambayo yamejengwa kwa
kutumia fedha za ndani. Ni mwendelezo wa uzinduzi wa miradi ya majengo ya
Mahakama yanayozinduliwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo katika mikoa
tofauti hapa nchini umezingatia mahitaji ya kisasa kwa wadau wa mnyororo wa
utoaji haki ambapo kuna ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii
ambapo maeneo kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum na watoto wamewekewa
vyumba vya kutumia wakiwa mahakamani.
Kuzinduliwa kwa majengo hayo katika Mikoa hiyo
mitatu kutaongeza ufanisi na utoaji huduma kwa wananchi kwani majengo hayo yana
mazingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Hafla ya uzinduzi inatarajiwa kuanza saa 3 asubuhi na itahudhuriwa na
Viongozi Waandamizi mbalimbali wa Mahakama, Serikali na Bunge. Wananchi wa Mkoa
wa Katavi, Lindi, Songwe na Mikoa mingine wanaalikwa kufuatilia matangazo ya
moja kwa moja ya tukio hilo yatakayorushwa kupitia vituo vya 'Channel Ten' na ITV.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni