·Waanza kazi kutoa elimu ya kisheria kwenye vyombo vya habari
Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe tarehe 23
Januari, 2023 amezindua utoaji elimu ya sheria kwenye Vyombo vya Habari huku
akisisitiza wananchi kuendeleza imani yao kwa Mahakama ili iweze kuwatatulia
migogoro waliyonayo.
Katika uzinduzi huo, Jaji
Ngwembe aliambatana kwenye Kituo cha Redio Abood na Majaji, Mhe. Messe Chaba na Mhe. Gabriel Malata
pamoja na viongozi wengine waandamizi, Naibu Msajili, Mhe. Augustina Mbando na
Mtendaji wa Mahakama Bw. Ahmed Ng’eni.
Akizungunza kupitia
Kituo hicho, Mhe. Ngwembe aliwasihi wananchi kujitokeza kufuatilia vipindi vya
elimu vitakavyokuwa vikiendelea kutolewa kupitia Radio na Televisheni mkoani
Morogoro kwani wameandaa mada zitakazowasaidi kuijua sheria na kuepuka makosa
yatokanayo na kutoijua sheria.
Aliendelea kusisitiza
wananchi kuishirikisha Mahakama ili kutatua migogoro yao kwakuwa watatumia
usuluhishi kwa kipindi chote, hoja ambayo iliungwa mkono na Jaji Malata ambaye
alielezea namna Kanda hiyo ilivyotumia usuluhishi kutatua mgogoro ulioendelea
ndani ya familia kwa zaidi ya miaka ishirini.
“Baada ya kuwasuluhisha
wote walitoka mahakamani wakiwa na furaha na kuahidi watakapofika nyumbani
watapika chakula na kula kwa pamoja, hivyo unaweza kuona namana usuluhishi
ulivyorejesha amani ndani ya familia hiyo,” alieleza Mhe. Malata.
Kwa upande wake, Mhe.
Chaba alienda mbali zaidi na kufafanua kuwa njia ya usuluhishi ikitumika
itampunguzia mwananchi gharama za kufika mahakamani na huokoa muda ambao
utamsaidia kujikita katika shughuli za uzalishaji. Jaji Chaba aliwasihi wananchi
kuendelea kuiamini Mahakama na kuleta mashauri yao ili yapatiwe ufumbuzi.
Majaji na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro wakiwa katika kipindi cha radio.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma.)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni