·Mahabusu wafunguka kuhusu dhamana, kukamatwa tena baada ya kuachiwa
Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Katika kutoa elimu wakati
wa Wiki ya Sheria nchini, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha imetembele Gereza la Mahabusu
Mkuza na kusikiliza kero zao, ikiwemo ukosefu wa dhamana kwenye makosa yanayodhaminika
na ucheleweshaji wa mashahidi kuletwa mahakamani.
Akizungumza katika Gereza hilo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce Mkhoi amesema kuna kesi nyingine zinazofikishwa mahakamani ambazo zinaweza kumalizika kwa njia ya usuluhishi.
“Kwa mfano polisi wanaweza
kufanya usuluhishi kama wakati mwingine wahusika wakikubaliana kulipana fidia
kwa makosa madogo kuliko kusubiri shauri lifike mahakamani, hii inapoteza muda,”
alisema.
Naye Mwendesha Mashtaka Kiongozi,
Bi. Auralia Makundi alibainisha kuwa kama mshtakiwa anataka kukiri kosa anaweza
kuandika barua kwa Mkuu wa Mashtaka wa Mkoa na kisha majadiliano hufanyika na
kama wakikubaliana shitala litaondolewa kwa kulipa kiasi fulani cha fedha.
“Kama majadiliano
yatashindikana basi nyaraka zote zilizokuwa zinatumika kwenye mchakato huo
zitateketezwa na jambo hilo litabaki kuwa siri na kesi itaendelea,” alisema.
Kwa upande wao, Mahabusu wa gereza hilo wameomba upande wa mashtaka kufungua dhamana kwa mashauri ambayo yanadhaminika na kuleta mashahidi mahakamani kwa wakati. Wamelalamikia pia suala la wao kukamatwa tena mara wanapoachiwa na Mahakama au pale upande wa mashtaka unapoamua kuondoa shitaka.
Katika hatua nyingine,
timu ya waelimishaji kutoka Mahakama hiyo imetembelea Kijiji cha Soga na kupokea
malalamiko kutoka kwa wananchi. Akiongea katika ofisi ya Mtendaji wa Kijiji hicho,
Mzee Kufa Kulala amesema wajumbe wa Mabaraza
ya Ardhi wengi hawajui taratibu na sheria za ardhi, hivyo husababisha migogoro
kuwa mikubwa zaidi.
Aidha amesema wananchi
wanalalamikia ada za ufunguaji wa mashauri kuwa kubwa ukilinganisha na hali ya
uchumi wa sasa, hivyo kupelekea juhudi zinazofanywa katika kutatua migogoro kutokuleta
matunda katika Kijiji hicho.
Mahakama ya Hakimu Mkazi
na Mahakama ya Wilaya Kibaha zimejikita kutoa elimu hasa katika Wilaya ya
Kibaha Vijijini maana ndio maeneo ambayo yamekuwa na mgogoro mkubwa wa ardhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni