Jumatano, 25 Januari 2023

WIKI YA SHERIA ISAIDIE KUPUNGUZA UKATILI WA KIJINSIA: JUDGE MLYAMBINA

Na Catherine Francis- Mahakama Kuu, Songea

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ametembelea mabanda ya maonyesho mjini hapa na kulishauri Dawati la Kijinsia la Jeshi la Polisi kujikita katika kuuelimisha umma kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia ili kupunguza uhalifu kwenye makosa hayo.

Mhe. Mlyambina alisema kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamiii, hivyo ni vyema wananchi watakaotembelea banda la Dawati hilo kuelimishwa umuhimu wa kuishi kwa upendo na amani na madhara yatokanayo na vitendo hivyo.

“Ninaamini mkifanya hivyo, Wiki hii ya Sheria itakapoisha itasaidia kupunguza vitendo hivi kwa kuwa elimu ya kutosha itakuwa imetolewa,” Jaji Mfawidhi huyo alisema.

Kadhalika Mhe. Dkt. Mlyambina ameshauri mbali na elimu kuhusu ukatili wa kijinsia pia ni vyema wakatoa elimu juu ya haki za watoto na matunzo yao kwa ujumla kutokana na uwepo wa wimbi kubwa la mashauri yanayohusu matunzo ya watoto.

Aliendelea kushauri kuwa ni vyema wazazi kushauriwa madhara yatokanayo na utelekezaji wa watoto, hasa wazazi wa kiume kuacha tabia hiyo kwani inaongeza idadi ya watoto wa mtaani, hivyo kuchochea vitendo vya uhalifu kama vile ubakaji na ukabaji pamoja na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya.

Mhe. Dkt. Mlyambina alipata nafasi pia ya kutembelea banda la Mawakili wa Kujitegemea (TLS) ambapo alipata ufafanuzi kuhusu maana na faida za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kama kauli mbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka 2023 inavyosema.

Wakili Naomi Ngoga alimweleza kuwa kama wadau muhimu wa Mahakama wanao wajibu wa kuwaelimisha na kuwashauri wateja wao kuhusu umuhimu wa kumaliza mashauri yao kwa njia ya usuluhishi.

Aidha Wakili huyo alisema kuwa amekuwa akiwashauri wananchi wanaofika kupata elimu ya sheria katika banda hilo kuwa ni vyema wakaacha kuwahusisha watoto kwenye matatizo au migogoro ya wazazi hususani ya ndoa kwani imekuwa ikiwaathiri kisaikolojia.

Akiwa katika banda la Mahakama, Jaji Mfawidhi alipokea maelezo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Songea Mjini, Mhe. Happiness Shelembi.

Alielezwa kuwa katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu wamekuwa wakiwaelimisha wananchi umuhimu wa kuandika wosia mapema ili kuepuka migogoro mingi inayosababishwa na mashauri ya mirathi ambayo huchukua muda mrefu mahakamani.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akizungumza na Mkaguzi wa Jeshi la Polisi Oscar Kitaly akiwa kwenye banda la Jeshi hilo.
Wakili Naomi Ngoga akifafanua jambo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (mwenye suti na tai nyekundu).
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Songea Mjini, Mhe. Happiness Shelembi akifafanua jambo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (mwenye suti na tai nyekundu) akipata elimu kutoka kwa Maafisa Uhamiaji kuhusiana na uhamiaji mtandaoni.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni