Jumatano, 25 Januari 2023

MAHAKAMA MAMBO SAFI MWANZA WIKI YA SHERIA

·Wananchi wamimina sifa lukuki kwa kuendeleza utaratibu huo

Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza

Zoezi la utoaji elimu ya kisheria limeendelea kushika kasi jijini hapa huku wananchi wakimiminika kwenye mabanda na kufurahia huduma wanayopokea kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.

Katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki vilivyopo katika eneo la Buswelu, elimu imeendelea kutolewa na wananchi wa eneo hilo wameitikia kwa furaha zoezi zima.

Akizungumza katika viwanja hivyo, Bi. Amina Jumbe aliyefika kupata msaada na elimu ya kisheria aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuleta Wiki ya Sheria nchini kwa wananchi.

“Kwa kweli nimefarijika sana kwa msaada na elimu niliyopata hapa kwani mara nyingi nimekuwa nikitumia gharama kwenda kwenye ofisi za Mawakili kila ninapopata changamoto za kisheria, lakini leo nimepewa njia rahisi kabisa ya kuweza kutatua changamoto iliyokuwa ikinikabili bila gharama zozote,” alisema.

Naye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ilemela, Mhe. Amani Sumari, ambaye ndie alikuwa mtoaji elimu kwa upande wa banda la Mahakama, alisema kuwa mwitikio wa wananchi unaridhisha.

“Wananchi wengi waliofika wana migogoro ya ardhi na tuliweza kuwaelekeza katika banda la Baraza la Ardhi na Nyumba. Wananchi waliofika kwenye banda letu wengi wao wanaulizia masuala ya dhamana, ndoa na talaka.Tumewaelimisha njia bora ambazo wanatakiwa kuzifuata ili kutatua changamoto hizo,” alisema.

Kwa upande wa Wilaya ya Nyamagana, elimu imeendelea kutolewa katika eneo la Kamanga na zoezi zima lilikuwa likisimimamiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Mhe. Veronica Mugendi na Hakimu Mkazi, Mhe. Cresensia Mushi.

Viongozi hao wa Mahakama walizungumzia zoezi zima katika kituo hicho kuwa linaendelea vizuri na wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu na msaada wa kisheria kama inavyotakiwa.

“Wananchi wengi waliojitokeza kwenye kituo chetu wamekuwa na changamaoto za ardhi, kwa hiyo elimu kubwa kuhusu suala hili inatakiwa kutolewa kwa wananchi,” Mhe. Mugendi alisema.

Zoezi la utoaji wa elimu linaendelea leo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza kwenye eneo la Buswelu na katika kituo cha mabasi Nyamhongolo kabla ya zoezi hilo kuhamia kwenye kituo cha Mabasi cha Nyegezi kwa siku ya Ijumaa na Jumamosi.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Ilemela, Mhe. Amani Sumari (wa pili kulia) akizungumza na wananchi waliofika katika banda la Mahakama.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Mhe. Cresensia Mushi (juu na chini) akiwahudumia wananchi.

Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Nyamagana, Bi. Irene Malamsha akieleza jambo kwa mteja (hayupo kwenye picha) aliyefika kwenye banda la Mahakama kupata huduma ya kisheria.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni