·Jaji Kiongozi awaambia Mawakili wa Kujitegemea
·Awataka kutokuwa vikwazo kwenye mchakato wa usuluhishi
· Ashauri TLS kufanya utafiti ushiriki wa wananchama kwenye usuluhishi
Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewataka Mawakili wa
Kujitegemea kuwatumikiwa Watanzania kwanza wanapotekeleza majukumu yao katika mnyororo
mzima wa utoaji haki na kujiepusha kuwa vikwazo wakati wa utatuzi wa migogoro
kwa njia ya usuluhishi.
Mhe. Siyani ametoa wito huo
leo terehe 25 Januari, 2023 alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari baada ya
kutembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Sheria ya utoaji wa elimu na msaada
wa kisheria ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na wadau mbalimbali katika Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa.
“Nimezungumza mara
kadhaa, ni sauti inayozungumzwa na watu wengi kuhusu ushiriki wa Mawakili kwenye
usuluhishi. Mawakili wana nafasi kubwa, pengine kuliko Wasuluhishi wengine, wakiamua
mashauri yafanikiwe kwenye usuluhishi, hivyo msiwe vikwazo (katika kufanikisha utaratibu
huu),” Jaji Kiongozi amesema.
Mhe. Siyani amebainisha
kuwa Mawakili wa Kujitegemea ni muhimu katika mnyororo wa haki kwa vile wanayo
nafasi ya kusaidia upatikanaji wa haki kwa haraka, hivyo wanapaswa kutambua
kuwa pamoja na haki yao ya kupata kipato wanao kwanza wajibu kwa Watanzania.
“Natambua kila kazi ina
kipato lakini katika kazi hii ya sheria msingi wake wa kwanza siyo kipato, kipato
ni kitu kinachofuata baadaye. Bado Mawakili wanaweza kutumia
usuluhishi na kupata kipato kinachostahili kwa sababu sheria katika nchi yetu
zipo zinazoonyesha Wakili anastahili kupata nini kwa shauri la aina gani
litakaloshughulikiwa,” amesema.
Jaji Kiongozi ametoa
wito kwa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kufanya tafiti kuangalia ushiriki
wa Mawakili katika usuluhishi upo kwa kiwango gani na kupitia utafiti huo kuzungumza
na wanachama wake ili kuwahamasisha kushiriki moja kwa moja na kufanikisha
usuluhishi.
“Chama cha Mawakili ni
nguzo ya haki katika nchi yetu kwa sababu kinarahisisha kazi ya Mahakama katika
kutatua migogoro. TLS ifanye utafiti ili kujua mchango wa Mawakili kwenye
usuluhishi, sisi tunaamini utatuzi wa haraka wa migogoro utachochea ukuaji wa
uchumi na tungependa migogoro itatuliwe kwa usuluhishi,” amesema.
Kabla ya kuongea na
Vyombo vya Habari, Jaji Kiongozi alipata fursa ya kutembelea na kukagua mabanda
mbalimbali, ikiwemo lile la Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu, Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mkemia Mkuu
wa Serikali, Magereza, Taasisi ya Usuluhishi na Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja.
Ameelezea kufurahishwa
jinsi taasisi nyingi za kiserikali na binafsi zilivyojitokeza katika viwanja
hivyo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Kadhalika, Mhe. Siyani amejionea wananchi
ambao wamejitokeza kupata huduma ya elimu na ufahamu juu ya mambo mbalimbali
yanayohusu sheria na haki.
“Hii ni fursa ya wiki
nzima ambayo kwa upande wa Mahakama hupatikana mara moja kwa ajili ya wananchi
kutoa kero zao, kuuliza maswali na kupata majibu ambayo yatawasaidia
wanapotafuta haki zao kupitia vyombo vya sheria ambavyo vipo katika nchi yetu,”
amesema.
Jaji Kiongozi amebainisha
pia kuwa ameridhika, baada ya kukagua mabanda na kuona jinsi washiriki walivyojiandaa
na kujipanga, kuwa wananchi watakaofika katika viwanja hivyo watapata
elimu ya kutosha itakayowasaidia wanapoendelea na utatuzi wa migogoro.
“Naamini mwananchi
mwenye ufahamu juu ya jambo lolote lile anayo nafasi nzuri zaidi ya kulielezea
jambo hilo kuliko yule ambaye halifahamu. Tunapozungumza kuhusu haki ni vema
mwananchi aelewe anachokidai, asikimbilie mahakamani bila kujua angalau
viashiria au vyanzo muhimu vya kile anachokidai na wiki hii ya sheria ni fursa
ya kujifahamisha na kuuliza maswali,” Mhe. Siyani amesema.
Jaji Kiongozi ametumia
fursa hiyo kuwaalika wananchi wote kwa mara nyingine kufika katika viwanja
hivyo. Amewaomba Waandishi wa Habari kuwafikia wananchi kadri inavyowezekana ili
wafahamu uwepo wa maonesho hayo na watembelee viwanja hivyo au wafuatilie
vipindi katika vituo mbalimbali ili waweze kufahamu kinachoendelea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni