·Wananchi wafurika mitaani wakiandamana
·Jaji Mfawidhi atoa ujumbe mzito kwa wananchi
Na Dillon Uisso-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi ametoa
wito kwa wananchi wa Kanda hiyo kutembelea mabanda ya Wiki ya Sheria ili kupata
elimu na ushauri wa kisheria na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuongeza
umakini na ubora katika Mhimili wa utoaji haki.
Mhe. Maghimbi ametoa wito
huo katika uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Kanda ya Dar es Salaam, tukio lililohudhuriwa
na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya
Ilala, Mhe. Ng’wilabuza Ludigija ambaye
alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mhe. Amos Makala.
Viongozi wengine
waliohudhuria hafla hiyo ni Majaji wa Kanda ya Dar-es-salaam pamoja na
Divisheni za Mahakama Kuu, Naibu Wasajili, Mahakimu, watumishi wa kada
mbalimbali pamoja na taasisi za kiserikali zinazohusika kwenye mnyororo wa
utoaji haki pamoja na wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha
mgeni rasmi, Mhe. Maghimbi alisema kuwa Mahakama ikiwa ndio chombo cha utoaji
haki imekuwa mstari wa mbele kutekeleza takwa la kikatiba la utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi chini ya Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisisitiza kuwa utatuzi
mbadala wa migogoro kwa njia ya usuluhishi umekuwa ni chombo kikuu duniani,
hivyo matumizi yake yaimarishwe ili kuleta ustawi wa jamii na kukuza uchumi
endelevu kwani wadaawa hutumia muda mfupi kutatua migogoro na kuwawezesha kujikita
katika shughuli za uzalishaji.
Kuhusiana na matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Jaji Mfawidhi huyo aliwasihi wananchi
kufika katika mabanda yaliyoandaliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kupata
elimu kwa kuwa mashauri yote sasa yanasajiliwa kwa njia ya matandao na pengine
kusikilizwa kwa njia ya Mkutano Mtandao.
Akizungumza katika
uzinduzi huo, Mhe Ludigija alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam
kutembelea viwanja hivyo ili kupata elimu na kujua dhima ya Mahakama kwa kauli
mbiu ya mwaka 2023 ambayo ni “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya
Usuluhishi katika Kukuza Uchumu Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.” Aliendelea
kusisitiza kwamba usuluhishi ni njia bora ya kuokoa muda, kukuza uchumi wa nchi
na kudumisha mahusiano ya wananchi.
Mkuu wa Wilaya huyo alifurahishwa
na kauli mbiu hiyo kwani Mahakama imetambua juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan, katika kukuza uwekezaji na juhudi za kukuza uchumi endelevu.
Aliahidi kuwa
wataendelea kuitangaza Mahakama kwa ujumla na hasa Kituo cha Usuluhishi ili
wananchi wakimbilie zaidi kusuluhishwa migogoro yao, hivyo kudumisha amani nchini.
Maandamano hayo
yaliyoanzia katika viwanja vya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, maarufu
Mwembeni yalihudhuriwa na mafuriko ya watu. Waandamanaji walipita katika mitaa
mbalimbali kabla ya maandamano hayo kuhitimishwa katika Mahakama ya Hakimu
Kisutu kwenye viwanja ambavyo vinatumika kutoa elimu na msaada wa kisheria katika
kipindi chote cha Wiki ya Sheria kupitia mabanda ambayo yameandaliwa na
Mahakama na wadau mbalimbali.
Moja ya mabanda yaliyoandaliwa na Mahakama kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwenye Wiki ya Sheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni