Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Katika kuadhimisha Wiki
ya Sheria, Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro tarehe 24
Januari, 2023 walikutana na viongozi waandamizi wa Mkoa huo kutoa elimu ya sheria
na namna bora ya kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekithiri mkoani hapa.
Akizungumza katika Semina
iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Kanda hiyo, Mhe. Paul Ngwembe alisema kuwa viongozi katika Mkoa huo
wanamwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wapo kusimamia
amani na utulivu wa nchi.
Alisema kuwa viongozi
hao wana haki ya kuingilia mgogoro wowote unaoweza kuchangia uvunjifu wa amani
ili kufanya usuluhishi na kurejesha amani iliyotoweka na kama itashindikana
watapaswa kuupeleka mgogoro huo katika mamlaka inayohusika ili utatuliwe.
Jambo hilo liliungwa
mkono na Jaji Gabriel Malata ambaye alifafanua kuwa Serikali inauwezo wa
kutatua mgogoro wa ardhi kwa kuichukua ardhi husika na kuimiliki ikiwa mmiliki
wake amashindwa kuiendeleza kwa mujibu wa masharti yaliyopo kwenye hati ya
umiliki.
“Jukumu mama la kiongozi
yeyote ni kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika himaya yake,
hivyo nitoe rai yangu kuwa inapotokea migogoro yeyote tuwe mstari wa mbele
kuitatua kwa njia ya usuluhishi na itakaposhindikana tuifikishe katika vyombo
husika,” alisema Mhe. Malata.
Kwa upande wake, Jaji
Messe Chaba aliwaasa viongozi hao kuwashirikisha wanasheria waliopo katika
ofisi zao kwani watawasaidia kutatua changamoto nyingi zinazohitaji utatuzi wa
kisheria kwa kuwa wana uelewa wa kutosha.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa alitoa shukrani kwa Jaji Mfawidhi na timu yake kwa kuupokea
mwaliko na kutoa elimu kwenye mambo hayo ya msingi, hatua ambayo inaboresha mahusiano
mazuri kati ya Serikali na Mahakama na kuomba utaratibu huo kuendelea.
“Tunatambua kuwa
Mahakama ipo katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na sera kuu ni utatuzi wa migogoro
kwa njia ya usuluhishi, nasi tumeandaa mkutano huu ili tuweze kupata elimu.
Elimu hii tutaitoa vijijini ili nao wapate kujua haya tuliyojifunza,” alisema.
Semina hiyo
iliwakutanisha viongozi wa Mkoa huo, wakiwemo Wakuu wa Wilaya zote, Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashari zote, Wenyeviti
wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Wakuu wa idara,
taasisi na vitengo serikalini.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni