Alhamisi, 26 Januari 2023

WENYEVITI WA MABARAZA, MAHAKIMU WAJITOSA MITAANI KIBAHA KUTOA ELIMU YA SHERIA

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya Kibaha, Mhe. Sarah Mbunga ametoa wito kwa wananchi wa Kijiji cha Muheza, Kata ya Mailimoja kufanya usuluhishi wa migogoro katika Mabaraza ya Kata kwanza kabla ya kwenda kwenye Mabaraza ya Wilaya.

Mhe. Mbunga ametoa wito huo jana tarehe 25 Januari, 2023 katika mkutano na wanakijiji wa Kijiji hicho alipokuwa anatoa elimu katika Wiki ya Sheria nchini. Mwenyekiti huyo amesema kuwa katika Baraza la Ardhi Wilaya ya Kibaha kumekuwa na mashauri mengi yanayohusu ardhi.

Amewasihi wananchi hao kufanya suluhu katika ngazi za kaya kwanza kabla hata ya kufika katika Kata. Ameeleza kuwa migogoro mingine inahusu kugombea hatua tatu ambapo wahusika wawili pekee wanaweza kusuluhisha jambo hilo pasipo mtu wa tatu kuingilia.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi, Kata ya Mailimoja, Bi. Mosi Msiba amewaomba mabalozi wa mashina kutoa ushirikiano ili kupunguza migogoro maana utatuzi wake huanzia katika ngazi hiyo.  Aidha, mjumbe wa baraza hilo, Bw. Richard Mandi amesema katika kesi kumi zinazofika katika baraza hilo, nane zinatoka katika Kijiji cha Muheza.

Mwananchi wa Kijiji hicho, Bw. Vitus Mkoroma ameiomba Mahakama kuweka kambi kijijini hapo ili kutoa elimu ya kutosha na wala isiishie katika Wiki ya Sheria kwa kuwa eneo hilo ni makazi mapya ambalo lina migogoro ni mingi na wananchi hawajui haki zao.

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa wafanyabisha wadogowadogo wengi hawana uelewa wa sheria mbalimbali, hasa sheria ya mirathi kwa kuwa wapo katika harakati za kutafuta fedha muda wote. 

Hayo yamebaishwa na timu ya Mahakimu na Wanasheria kutoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Kibaha ambayo ilifika katika Soko la Mlandizi kutoa elimu ya kisheria kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kote nchini.

Akitoa elimu katika soko hilo, Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Maltrida Zakaria amesema kesi nyingi za ukatili dhidi ya watoto zinatoka na wazazi kutokupata muda wa kukaa nao kuongelea changamoto wanazopata wakiwa shuleni na hata nyumbani. Ametoa wito kwa wafanyabiashara hao, kwa kuwa nao ni wazazi, kutenga muda wa kuongea na watoto wao na kujenga urafiki.

Awali, akifungua mjadala katika soko hilo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Hamis Ally alielezea kuhusu suala la dhamana. Alisema   kuna makosa yanayodhaminika na kuna yale ambayo hayana dhamana. Alibainisha kuwa dhamana ni haki ya kikatiba ambayo mtu hupewa kwenye makosa yanayodhaminika japo kwa msharti.

Akijibu swali la mdau kuhusu ulinzi shirikishi, Hakimu huyo alisema suala la ulinzi ni wajibu wa kila raia, huku halmashauri zikipewa mamlaka ya kutunga sheria ndogo ndogo wanazoona zinafaa bila kukiuka sheria mama za nchi.

Akiongezea kwenye jibu hilo, Mwanfunzi wa Chuo cha Sheria kwa Vitendo, Bw. Amir Ramadhani alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na sheria ya polisi zimeruhusu wananchi kushiriki kwenye shughuli za ulinzi na usalama.

Mwenyekiti Baraza la Ardhi la Wilaya Kibaha, Mhe. Sarah Mbuga (juu) akitoa elimu katika Kijiji Cha Muheza Mailimoja Kibaha. Picha chini wananchi wa kijiji hicho wakimsikiliza.


Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama Hakimu Mkazi Kibaha, Mhe. Hamis Ally (aliyeshika kipaza sauti) akiongea na wafanyabiashara katika Soko la Mailimoja.
Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Maltrida Zakaria (juu) akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Mlandizi (chini) huku kazi za kupakua mizigo zikiendelea.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni