·Mahakimu wazama vijijini kutoa elimu ya sheria
·Mwitikio wa wananchi washangaza
Na Faustine Kapama-Mahakama
Mahakimu katika Mahakama
ya Wilaya Kisarawe wameamua kuzama vijijini kutoa elimu na msaada wa kisheria kama
sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayofanyika nchini kote.
Timu ya Mahakimu hao ikiongozwa
na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Devotha Kisoka tayari
imeshatembelea Kambi ya Jeshi ya Kisarawe na Shule ya Sekondari ya Wasichana Joketi
Mwegelo kabla ya kusambaa vijijini.
“Sisi tumeamua kwenda vijijini
kuelimisha wananchi kwenye masuala mbalimbali ya kisheria na tukiwa huko
tutatoa pia huduma za kisheria na bahati nzuri tumeambatana na Wakili Msomi wa
Kujitegemea, Mhe. Moses Chunga,” amesema.
Ameeleza kuwa timu yake
ambayo inajumuisha pia Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Frank Lukosi, Hakimu Mkazi
Manifred Sanga na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Zaituni Khatibu imeshatembelea
Kijiji cha Masaki kilichopo katika Kata ya Sungwi.
“Kote huko tulikopita
mwitikio wa wananchi ni mkubwa sana, hatukutegemea kwa kweli. Wananchi wanahamu
ya kujua masuala mbalimbali yakiwemo ya ardhi, miradhi, ndoa na taraka na
mengine mengi. Sisi tupo kwa ajili ya kuwatumikia na tumejipanga vizuri,” alisema
Mhe. Kisoka.
Amesema kwa sasa wapo katika
Kijiji cha Boga kilichopo Tarafa ya Manelumango kwa ajili ya kuendeleza zoezi
la utoaji elimu kwa wananchi. Mhe. Kisoka ameahidi kufika katika maeneo yote
ili elimu ya kisheria iweze kuwafikia wananchi wengi ambao hawana uelewa wa
kutosha kwenye masuala hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni