· Ni Mzee wa Kimakonde mwenye umri wa miaka 61
·Amerithi kipaji cha usuluhishi kutoka kwa babu yake
·Mbinu zake za utendaji zafananishwa na busara za Mfalme Suleiman
·Adai usuluhishi lazima ufanyike majira ya jioni kulinda usiri
Na Mwandishi Wetu
Wakati Wiki ya Sheria
nchini yenye kauli mbiu “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi:
Wajibu wa Mahakama na Wadau” ikizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mtwara imegundua uwepo wa mwananchi mwenye kipaji cha kipekee cha utatuzi wa
migogoro nje ya Mahakama.
Mwanachi huyu ni Issa
Mohamed Mkumba (61), Mkazi wa Kijiji cha Msimbati, Kata ya Msimbati katika Wilaya
ya Mtwara.
Akiongea na Mwandishi
wetu Mjini Mtwara, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara,
Mhe. Mh. Zainab Muruke anaeleza kuwa waligundua uwepo wa Mzee Mkumba baada ya
kufanya ziara katika Mahakama ya Mwanzo Msimbati ambapo alielezwa uwepo wa kesi
chache zilizofunguliwa mahakamani kutokana na migogoro mingi kusuluhishwa nje
ya vyombo rasmi vya dola.
“Ilikuwa mwaka jana.
Nilipotaka kujua zaidi kwa nini hali hii ipo hivyo ndipo nikatajiwa jina la
Issa Mohamed Mkumba. Watu wengi
walimsifu kuwa anafanya kazi yake vizuri,” anaeleza Jaji Muruke.
Kama njia mojawapo ya
kutambua mchango wake na kujifunza zaidi kuhusu kazi zake, Jaji Mfawidhi huyo anaeleza
kuwa alimwalika Mzee Mkumba ofisini kwake siku ya Jumamosi tarehe 21 Januari, 2023
kwa mazungumzo na kubadilishana uzoefu.
Katika mazungumzo hayo
yaliyohudhuriwa pia na Jaji wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe. Dkt.
Eliamani Laltaika, Naibu Msajili Amiri Msumi na Mtendaji wa Mahakama Kuu,
Kanda, Bw. Richard Mbamba, Jaji Mfawidhi anasema kuwa Mzee Mkumba alieleza kwa
kirefu kuhusu changamoto na mafanikio ya kazi zake.
Elimu na urithi
Jaji Mruke anamnukuu Mzee
Mkumba akieleza kuwa yeye ana elimu ya darasa la nne aliyoipata katika shule ya
Msingi Msimbati pamoja na elimu ya dini ya Kiislam (madrassa) aliyoipata
akiwana na umri mdogo. Anasisitiza kuwa mbali na elimu hizo, amerithishwa
maarifa mengi kutoka kwa wazee wake, hususan babu yake ambaye mara kwa mara
aliambatana naye katika shughuli za usuluhishi.
“Babu yangu alikuwa
akiamua migogoro. Baadaye alimuachia baba yangu nami nimerithi kwa baba,” Jaji
Mdawidhi anamnukuu Mzee Mkumba akieleza.
Hekima za Mfalme Suleiman
Mzee Mkumba
anabadilishana uzoefu na Viongozi Waandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara
kwa kusimulia kisa kimoja na namna alivyo kitolea unamuzi unofanana na simulizi
za Mfalme Suleiman katika mgogoro wa wanawake waliokuwa wakigombea mtoto.
Mwanamke Mwenye Kuku ni Yupi?
Katika simulizi hiyo,
Mzee Mkumba, kwa mujibu wa Mhe. Mruke, anaeleza kuwa wanawake wawili walifika
kwake wakigombania kuku ambaye mmoja wao alikuwa akienda kumuuza sokoni. Kila
mmoja kati ya wanawake hao aling’ang’ania kuwa ndiye mwenye kuku.
“Niliwaomba wakae nami
mpaka jioni. Ilipofika jioni nikawaambia turudi mtaani kwao. Tukifika
tutamuachia huyu kuku na kuona atakimbilia wapi. Mama mwenye nyumba
atakapoelekea kuku ndiye atakuwa mmiliki,” ananukuliwa Mzee Mkumba akisimulia huku
akionyesha kujiamini.
Huku akisisitiza, Mzee
Mkumba anaendelea kunukuliwa akieleza, “Tulipomuachia tu yule kuku alikwenda
moja kwa moja kwa yule mama aliyetaka kumuuza. Tukakubaliana kuwa yule mama
aliyesingiziwa kuwa kaiba kuku alipwe fidia ya shilingi elfu kumi.”
Kwanini Kusuluhisha Jioni?
Mzee Mkumba anasisitiza
kuwa kazi zake za usuluhishi hupendelea kuzifanya jioni kabisa mpaka saa sita
za usiku.
Jaji Mfawidhi anamnukuuu
Mzee Mkumba ambaye anasisitiza, “Kwa Kimakonde tunamsemo unaosema ‘Samaki
hanoni usiku’. Vitu vigumu vinaweza kufanyika kirahisi usiku kwani kunakuwa na
utulivu. Ni rahisi pia kuzungumzia mambo ya siri bila taarifa kuwafikia wasio
husika. Usiku hulinda usiri,” anasisitiza Mzee Mkumba huku akitumia Nahau na Semi
za busara za jamii yake ya Kimakonde.
Kumbukumbu ziandikwe
Akihitimisha mazungumzo
hayo yaliyodumu kwa takribani saa tatu, Jaji Muruke alitoa wito wa kutunza
kumbukumbu za busara za wazee kama Mzee Mkumba katika maandishi.
Mahakma Kuu Kanda ya
Mtwara imepanga kuwafikia watu wa rika mbalimbali na kutoa elimu ya sheria,
hususani suala la kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Wadau mbalimbali
wamejipanga kushirikiana na Mahakama kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo
redio za jamii, pamoja na kutembelea maeneo kadhaa, ikiwemo shule za sekondari
na msingi, magereza, utoaji wa msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na kusikiliza
malalamiko na kuyatafutia ufumbuzi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni