Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma leo tarehe 24 Januari, 2023 ametembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria
yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma huku
akitoa rai kwa wananchi kutembelea maonesho hayo ili kupata elimu ya usuluhishi
kufahamu kwa kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu inayohusu masuala ya
usuluhishi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya
kutembelea mabanda kadhaa ya Maonesho, Msajili Mkuu, Mhe. Chuma amesema kuwa
kaulimbiu ya mwaka huu imewekwa mahsusi lengo likiwa ni kutoa elimu kwa umma
ili kufahamu umuhimu wa suala ya usuluhishi ambalo lina faida nyingi ikiwa ni
pamoja na kuleta utengamano katika jamii.
“Maonesho haya yana umuhimu mkubwa kwa umma, moja ni kujenga
uelewa wa wananchi na wadau kuhusu masuala ya Mahakama tasnia ya Sheria kwa
ujumla. Mabanda haya yamesheheni wadau mbalimbali, hivyo ni muhimu wananchi kufika na kupata uelewa wa
masuala mbalimbali,” amesema Mhe. Chuma.
Aidha, baada ya kutembelea mabanda hayo, Msajili Mkuu
ameonesha kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa Wadau mbalimbali wa Mahakama
waliojitokeza kushiriki kwenye maonesho ya wiki ya Sheria pamoja na Mahakama ya
Tanzania.
Miongoni mwa mabanda yaliyotembelewa na Msajili Mkuu
ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Tume ya
Kurekebisha Sheria, Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Ofisi ya Taifa ya
Mashtaka (DPP), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (LST), Wakala wa
Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG), RITA
na Wakili Mkuu wa Serikali (OSG).
Maonesho haya ya Wiki ya Sheria yanaendelea kufanyika
nchi nzima hadi tarehe 29 Januari, 2023 ambapo kilele cha Siku ya Sheria nchini
itakuwa tarehe 01 Februari, 2023.
Kauli mbiu ya Wiki na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni; Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia
ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.
Maelezo kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni