Na Magreth Kinabo -Mahakama
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma
Maghimbi amesema kwamba utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
utawezekana pale ambapo wananchi wenyewe watakua tayari, kufuata taratibu za
kimahakama na wadau wengine nje ya Mahakama kwa kuhudhuria pale wanapohitajika.
Kauli hiyo imetolewa na Jaji Salma wakati akiwa mgeni rasmi wa kilele
cha Siku ya Sheria katika kanda hiyo, kilichofanyika leo tarehe 1 Februari,
mwaka 2023 kwenye Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es
Salaam, ambapo alisema hayo yote yatawezesha Mahakama na wadau hao kuwahudumia
kwa wakati, na kwa ubora zaidi.
“Napenda kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa
kila mwananchi, kufahamu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
una faida kubwa katika kukuza uchumi endelevu. Wananchi pia tujisomee sheria
ili tuwe na uelewa angalau kidogo wa sheria. Tusiwaachie mawakili na wanasheria
peke yao jukumu la kufahamu taratibu za sheria hizi za utatuzi wa migogoro kwa
njia ya usuluhishi.
“Tunapokuwa na jambo linalohusu sheria,
mathalan ya madai, ndoa, mwenendo wa makosa ya jinai, sheria ya usuluhishi nje
ya Mahakama hatua ya mwanzo kabisa ni mwananchi asome vifungu vya sheria husika
yeye mwenyewe na apate uelewa kabla ya kufungua shauri Mahakamani, mwananchi
ahakikishe kuwa anafahamu hatua zote kesi yake itapitia katika ngazi ya
Mahakama zote hadi Mahakama ya Rufani. Hauhitaji elimu ya Sheria kujua hatua
muhimu ambazo kesi zako zitapitia.
Aliongeza kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika kukuza
Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau”. Kazi ya kutatua migogoro inayohusisha wadau mbalimbali, wadau hao
wakitimiza wajibu wao kwa wakati, wataiwezesha Mahakama kumaliza mashauri na
wananchi kupata suluhu na haki zao kwa wakati.
Jaji Salma alisema utatuzi wa migogoro mahakamani na nje ya mahakama
kwa njia ya usuluhishi unafaida nyingi ikiwa ni pamoja na; Serikali ni mdau
muhimu na wezeshi kwa Mahakama katika kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi ili
kukuza uchumi endelevu, upatikanaji wa
haki kwa wakati kwa gharama nafuu, utatuzi wa migogro kwa njia ya ustaarabu,
amani na kwa muda mfupi bila kufungwa na masharti ya sheria na taratibu za
kiufundi.
Hivyo kuwawezesha wananchi kushiriki katika
shughuli za kukuza \uchumi ikilinganishwa na njia ya kawaida ya
usikilizaji/uendeshaji wa mashauri inayoweza kuchukua muda mrefu. Faida nyingine
ni huzingatia maslahi ya wadaawa ili kulinda mahusiano yao ya kijamii na
kiuchumi,Gharama hupungua kwa kila upande baina ya wadaawa na Mahakam na huhifadhi mahusiano ya kibiashara na ya kijamii
kwa wadaawa.
Aliushukuru uongozi ya mkoa wa Dar es Salaam
na Mkoa wa Pwani kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuleta maboresho
yanayosukumwa na dhana ya kupeleka huduma za haki kua karibu na wananchi.”Ninachukua
fursa hii kukushukuru wewe na uongozi wa serikali mnazoziongoza kwa kusaidia
kupata maeneo ya ujenzi wa Mahakama kwa Mahakama ya Mwanzo Madale Wilaya ya
Kinondoni, Mahakama ya Wilaya Ubungo, Mahakama za Mwanzo Gezaulole Wilaya ya
Kigamboni, Chamanzi wilaya ya Temeke na Lubakaya-Wilaya ya Ilala kwa mkoa wa
Dar es Salaam,” alisisitiza.
Kwa Mkoa wa Pwani umewezesha kupata maeneo ya
ujenzi wa Mahakama Kuu Kibaha na Mkamba-Kisarawe.ambapo aliomba salamu hizo zifikishwe
kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Akizungumza kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mhe. Mwema Punzi ambaye ni Mwanasheria
wa Serikali Mkuu, alisema katika jamii yoyote inayostawi utawala wa
sheria unabaki kuwa nguzo katika kukua na kuendeleza Taifa, Mahakama huru na thabiti
ni muhimu kwenye utawala wa maendeleo ya
kiuchumi kwa tafsiri adili na kwa wakati Pamoja na utekelezaji wa haki za uchumi
vinasaidia kujenga stahiki yanayohitajika katika uwekezaji na ukuaji wa uchumi
wetu.
“Ofisi yangu imewaidhinisha watoa huduma 494
za usuluhishi, majadiliano, na upatanishi wenye sifa. Idadi hiyo ni ndogo
ukilinganisha na mahitaji halisi yan chi. Migogoro yenye asili ya madai iliyopo kwenye Mabaraza ya
Ardhi na Nyumba na Mahakama za Mwanzo yapo zaidi ya mashauri 15.000 ya madai ya
aina mbalimbali hayajaisha katika Mahakama za Mahakimu na zile za juu,” alisema Mwema.
Mhe. Mwema alisema ofisi yake na Wakili Mkuu
wa Serikali wataendeleakusimamia kwa niaba ya Serikali matakwa ya kisheria ya
kutatua migogoro k wa njia ya usuluhishi.
Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika Kanda ya Mzizima, Bi. Tike Mwambipile alisema mawakili wa kujitegemea waanze kutumika
ipasavyo kwa kutoa huduma hiyo ya utatuzi wa migogoro mbalimbali kwa suluhu kwa kuwa wanawataalamu wa kutosha. Hivyo
kushiriki kwao katika suala hilo itasaidia kupunguza migogoro ya ardhi, mirathi
na ndoa.ikiwemo kuwapunguzia muda wanaoutumia wakuu wa mikoa na wilaya
kushughulikia migogoro mbalimbali.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe.Elizabeth
Nyembele alisema jumla ya wananchi 27,284 walipatiwa elimu ya sheria katika
maeneo mbalimbali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dares Salaam, Mhe. Amos
Makalla alisema yuko tayari kushirikiana na Mahakama katika kutatua migogoro
kwa njia ya usuluhishi ili kuweza kuwasaidia wananchi kupata haki zao gharama
nafuu na kuwawezesha kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mali na kujipatia
kipato.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na baadhi ya
viongozi wa dini, ambao waliiombea Mahakamma iendelee kutoa haki kwa uadilifu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe.
Salma Maghimbi(kulia) akiongoza maandamano ya wanataaluma ya sheria, kushoto ni
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla katika kilele cha Siku ya Sheria
Nchini iliyofanyika leo tarehe 01/02/2023 katika Viwanja vya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Sehemu
ya maandamano hiyo ikiendelea.
Gwaride maalum likiwa tayari kwa ajili ya ukaguzi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi
(mbele) akiwa Pamoja na majaji wengine wakipokea salamu kutoka kwa gwaride
hilo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma
Maghimbi(kulia) akikagua gwaride hilo.
Baadhi
ya watumishi wa Mahakama pamoja na wageni waalikwa wakiwa katika sherehe hiyo.Shehe
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhadj Mussa Salum akiomba sala maalumu kwa ajili
ya sherehe hiyo.
Wanafunzi kutoka shule ya Msingi Lioness Mibulani wakitoa burudani.
Wakili wa Serikali Mkuu Mhe. Mwema Punzi akitoa hotuba kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kiongozi
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Mzizima Bi. Tike Mwambipile akitoa hotuba kwa
niaba ya Rais wa TLS .
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos
Makalla akitoa hotuba yake katika sherehe hiyo.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Salma Maghimbi
akitoa hotuba yake.
. Meza
kuu ikiwa katika picha ya Pamoja.
Meza
kuu ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama. Mojawapo
ya Shauri la Usuluhishi likiendeshwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. (Picha
na Tumaini Malima- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni