Na Mwandishi wetu-Mahakama, Dodoma
Siku ya Sheria jana tarehe
1 Februari, 2023 imeazimishwa katika maeneo mbalimbali chini huku wananchi
wakihimizwa kutatua migogoro yao kwa njia za usuluhishi kabla ya kukimbilia
mahakamani, hatua ambayo itachangia ukuaji wa uchumi, amani na kupunguza
gharama na mlundikano wa mashauri.
Mwandishi wetu Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Bukoba, Mhe. Imakulata Banzi amewasihi wananchi kutumia njia mbadala katika
utatuzi wa migogoro ili kutumia muda mwingi katika shunguli za uzalishaji wa kipato.
Akizungumza katika
maadhimisho wa Siku ya Sheria, Mhe Banzi alielezea kauli mbiu ya mwaka 2023
inayohusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na kubainisha
kuwa ni jambo lisilopingika kwamba huwa hakuna suluhu kama shauli litamalizika
kwa njia ya kawaida kwa wadaawa kusikilizwa mahakamani.
“Mmoja kati ya wadaawa
hushinda na mwingine kushindwa, hivyo hakuna kutoka suluhu kama ilivyo katika
michezo, mfano mpira wa miguu. Matokeo hayo ya mdaawa kushinda na mwingine
kushindwa hupelekea chuki na kutokuelewana baina ya pande hizo mbili hasa
upande ulioshindwa,” alisema.
Amebainisha faida lukuki
zinazopatikana wakati wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika
kukuza uchumi endelevu zikiwemo, kimarisha
undugu na mshikamano katika jamii na kuongeza mshikamano katika jamii
kwa pande zilizokuwa zinahasimiana kwa muda marefu.
“Utatuzi wa migogoro kwa
njia ya kawaida huchelewesha kesi kumalizika kutokana na wingi wa mashauri,
lakinmi njia ya usuluhishi huwezesha migogoro kumalizika mapema kati ya pande
mbili na kuepusha Mahakama kulazimika kutumia taratibu za kiufundi ambazo
husababisha gharama kubwa,” alisema.
Mhe. Banzi alibainisha
kuwa njia ya usuluhishi husaidia pande zote kufikia muafaka kwa haraka na kumpa
mdaawa nafasi ya kufanya kazi na kuinua uchumi wake na uchumi wa nchi kwa
ujumla, huokoa gharama za uendeshaji wa mashauri na kupunguza mlundikano
mahakamani.
Kutoka Mahakama Mara, Kandana Lucas anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaasa wananchi wa Mkoa huo
kutumia njia ya usuluhishi ili kumaliza migogoro mbalimbali ya muda mrefu, hasa
ya ardhi na ndoa, inayopelekea watu kutumia muda mwingi kwenda mahakamani
kufuatilia mashauri yao huku wakiacha shughuli zao muhimu za uzalishaji mali.
“Utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni
mwarobaini wa migogoro yote, na basi la usuluhishi ni usafiri sahihi kuliko basi
la migogoro,” alisema. Kadhalika. Jaji Mtulya ametoa rai kwa wadau wa
Mahakama hasa, Mawakili wa Kujitegemea kuwa tayari na kuwashauri wateja wao
kufikia suluhu kwani upatanishi au suluhu ni maelekezo ya Mungu kwa dini zote
na kwamba kupitia upatanishi kazi hufanyika kwa amani na maendeleo hupatikana.
Kwa upande wake, mgeni
wa heshima, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele ambaye alimwakilisha
Mkuu wa Mkoa wa Mara kutoa salamu za serikali, alihimiza umma kutumia
usuluhishi ili kupunguza uwezekano wa visasi na uadui unaoweza kusababisha
makosa ya jinai kutendeka.
Katika hafla hiyo, Mwanasheria
wa Serikali na Chama cha Mawakili Tanganyika walipata nafasi ya kutoa salamu
ambapo wameiasa jamii kubadili fikra ili njia ya usuluhishi iweze kutumika
kutatua migogoro kwani lengo la kufanya hivyo ni kuimarisha upendo. Vilevile
viongozi hao walitoa rai kwa maafisa wote wa Mahakama kutokuwa chanzo cha ugumu
wa kutatua migogoro kwa njia ya suluhu.
Naye Catherine
Francis wa Mahakama Kuu- Songea anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Songea, Mhe. Dkt.Yose Mlyambina ametoa rai kwa wadau
wote wa Mahakama kuendelea kuelimisha jamii kwa usahihi juu ya matumizi ya
usuluhishi katika kutatua migogoro kabla haijafikishwa mahakamani ili kuendelea
na utaratibu wa kawaida wa usikilizai wa mashauri.
Alisema
kuwa mbali na umuhimu wa kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro,
Mhe. Mlyambina aliainisha baadhi ya changamoto wanazokutana nazo Mahakama
wakati wa usuluhishi ambapo mara nyingi wamekuwa wakitumwa wawakilishi wa
taasisi au kampuni ambao siyo wasemaji wa mwisho, jambo ambalo linapelekea
usuluhishi kuahirishwa na kuchukua muda mrefu.
Alishauri
inapotokea jambo kama hilo wakafika wasemaji wa mwisho kwa pande zote mbili za wadaawa
ili kuweza kuokoa muda. Mbali na hilo, Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa
changamoto nyingine ni mazingira ya kufanyia usuluhishi siyo rafiki.
Amefafanua
kuwa baadhi ya wadaawa hawavutiwi kwa kuwa mazingira yanayotumika ni yaleyale ambayo
huendeshea mashauri ya kila siku, hivyo jamii inapaswa kukubaliana na
changamoto hiyo iliyopo na kuendelea kufanya usuluhishi.
Mhe.
Mlyambina alinukuu usemi wa aliyekuwa mshauri wa masuala ya kiutawala na
mwandishi wa vitabu Peter Drucker usemao, “Jambo muhimu Zaidi katika
mawasiliano ni kusikia kile ambacho hakijasemwa”.
Alisema
kuwa katika usuluhishi wadaawa wanapojadiliana juu ya mgogoro wao ni rahisi
kugundua kile ambacho hakikusemwa na pengine ndiyo sababu ya mgogoro wao,
tofauti na kwenye taratibu za kawaida ambapo Mahakama hujikita katika yale
yaliyoainishwa.
Watumishi
na wadau wa Mahakama wakiandamana kuelekea viwanja vya Mahakama Kuu Songea
kusherehekea Siku ya Sheria nchini.
Kutoka Mahakama Mbeya, Ibrahim Mgallah anaripoti kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya leo tarehe 01 Februari 2023 imefanya maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwa mwaka 2023. Sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya. Siku ya sheria huadhimishwa kila mwaka kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama. Katika sherehe hizo
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe.Rose
Ebrahim ambaye alikuwa mgeni rasmi amewashauri wananchi kutumia usuluhishi kama
nyenzo muhimu ya utatuzi wa migogoro nje ya taratibu za kisheria za kimahakama
ili kuokoa muda na gharama.
“Iwapo watu wengi wataamua kumaliza migogoro yao kwa njia za usuluhishi
ni wazi zitasaidia Mahakama kupunguza mashauri ya mlundikano yaliyokaa kwa muda
mrefu na zitapunguza muda na gharama zitakazotumika katika kusikiliza mashauri
hayo. Badala yake muda huo utatumika katika uzalishaji jambo litakalopelekea
kuchochea ukuaji wa uchumi na kuvutia uwekezaji,” alisema.
Akitoa salamu zake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Juma Homera ambaye
alikuwa mgeni wa heshima ameipongeza Mahakama Kanda ya Mbeya kwa kazi nzuri
inayofanyika ya kusikiliza na kuamua mashauri kwa wakati.
Kdhalika, ameishauri Mahakama iendelee na utoaji wa elimu ya sheria kwa
wananchi ili kuwajengea uelewa zaidi wa masuala ya kisheria. “Ninakupongeza Jaji
Mfawidhi, Mahakimu na timu yako yote kwa kazi kubwa ya kushughulikia mashauri
kwa wakati,” alisema.
Baada ya hafla hiyo, wadau na viongozi mbalimbali walialikwa kusikiliza
shauri la uzinduzi lililofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Mbeya.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim akikagua gwaride la heshima katika maadhimisho ya Siku ya sheria nchini.
Naye Eunice Lugiana kutoka Mahakama-Kibaha
anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ameiomba Mahakama
ya Tanzania kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu usuluhishi bila kuhesabu
gharama kwa vile njia hiyo katika kutatua migogoro ina faida nyingi.
Amemshukuru Jaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuanza mchakato wa
ujenzi wa Mahakama Kuu katika Mkoa wake, hatua itakayowezesha upatikanaji wa
haki kwa urahisi. Amesema ujenzi huo pia utapamba Mji wa Kibaha kwakuwa jengo
hilo ni la ghorifa.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa
kuzungumza na wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson John alifurahishwa
na Mahakama ya Tanzani kuja na Kauli Mbiu ya mwaka 2023 kuhusu utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi na kubainisha kuwa imekuja muda muafaka ambapo
migogoro mingi ya Mkoa wa Pwani ianzie kwenye usuluhishi.
Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Kibaha, Mhe. Joyce Mkhoi, akizungumza katika maadhimishi
ya Siku ya Sheria alisema kukosa wataalamu wa usuluhishi katika Mahakama
kunasababisha mashauri mengi kutatuliwa kwa njia ya kawaida ya kusikiliza baada
ya kushindwa kufikia makubaliano kwa vile Wasuluhishi waliopo hawana mbinu za
usuluhishi.
Ameomba mafunzo
yafanyike kwa maafisa wa Mahakama ili mashauri yaishie kwenye usuluhishi.
Maandamano ya watumishi wa Mahakama na wadau wa Mahakama yaliyoanzia viwanja vya Mahakama ya Mwanzo Mailimoja na kuhitimishwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha.
Kwa
upande wake, Charles Philipo Ngusa
anaripoti kutoka Mahakama Geita kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Cleofas Waane amesema lengo la kauli
mbiu ya mwaka huu 2023 ni kuwakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi bila kufikisha mashauri yao mahakamani.
Amesema kauli mbiu hiyo inawakumbusha wadau wote na wananchi kwa ujumla
kuwa tayari kwa ajili ya usuluhishi na kuondokana na dhana ya kumaliza migogoro
yao mahakamani.
Aidha amesisitiza kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi
unasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa gharama nafuu zaidi, hivyo
kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kasi zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, ambaye
alikuwa mgeni rasmi aliipongeza Mahakama kwa kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya
kisheria ili kuwafikia wadau wengi zaidi, ikiwemo kutumia vyombo vya habari
kama redio.
Mkuu wa Mkoa ameomba kuwa elimu hiyo isiishie katika kipindi cha Wiki ya
Sheria bali uongozi wa Mahakama uweke utaratibu wakati wateja wakiwa wanasubiri
kuingia mahakamani waendelee kupewa elimu hiyo.
Aidha amevishauri vyombo vinavyohusika na usuluhishi kama vile Mawakili
kuweka utaratibu wa kujipima ili hadi kufikia mwakani waje na takwimu
zinazoonesha walitatua migogoro mingapi bila kufika mahakamani.
Katika hafla hiyo hotuba mbalimbali ziliwasilishwa kutoka katika taasisi
kadhaa zenye maudhui ya Siku ya Sheriam zikiwemo ofisi ya taifa ya mashtaka na
Mawakili wa Kujitegemea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni