Alhamisi, 2 Februari 2023

SIKU YA SHERIA NCHINI YAFANA; MAHAKAMA KANDA, MIKOA YAIADHIMISHA KWA BASHASHA

  • Usuluhishi wasisitizwa kwa nguvu zote

Na Waandishi wetu, Mahakama ya Tanzania

Tarehe 1 Februari, 2023 Mahakama ya Tanzania iliadhimisha kilele cha Siku ya Sheria nchini, siku hii muhimu huashiria uzinduzi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika. Sherehe za Siku ya Sheria nchini kitaifa imefanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mwandishi wetu Mayanga Someke anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru, amewashukuru wadau wote walioshiriki kutoa elimu katika wiki ya sheria, pia amewapongeza wananchi waliojitokeza kupata elimu hiyo adhimu.

 “Ndugu wageni waalikwa, leo ndio kilele cha maadhimisho na ndio siku ya sheria Nchini.Kauli mbiu ya mwaka huu ni; “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia kwa Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu Wa Mahakama Na Wadau.’’Kauli mbiu hii imebeba ujumbe mahsusi kuhusu wajibu wa mahakama na wadau wake kutumia njia ya usuluhishi kutatua migogoro kwa lengo la kukuza uchumi wa Nchi.

Ni vyema ikaeleweka kwamba usuluhishi na njia nyingine mbadala za utatuzi wa migogoro katika Nchi yetu ni takwa la kikatiba.Ibara ya 107A (2)(d) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 inahimiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.Kwa kuzingatia msingi huo wa kikatiba,sheria mbalimbali za Nchi zinatoa fursa kwa baadhi ya mashauri (siyo yote) kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi endapo wadaawa wataridhia.

Jaji Mfawidhi huyo alisema licha ya kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni suala la kikatiba bado eneo hili halipewi kipaumbele na wadaawa na wadau wa Mahakama.Bado ni mashauri machache sana yanaisha kwa njia ya usuluhishi.Mfano katika mkoa wa Rukwa pamoja na Mahakama Kuu mashauri yaliyoisha kwa njia hii mwaka jana 2022 ni kama ifuatavyo: Mahakama Kuu mashauri -3, Mahakama ya Hakimu mkazi Sumbawanga mashauri-0, Mahakama ya Wilaya Sumbawanga mashauri-4, Mahakama ya Wilaya Nkasi Mashauri-0, Mahakama ya Wilaya Kalambo mashauri-0 na kufanya jumla yake kuwa mashauri saba pekee yaliyoisha kwa njia ya usuluhishi.

Aliongeza kuwa katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, Mahakama ina wajibu wa kuongoza wadaawa kufikia makubaliano, kuandaa wataalam wa usuluhishi (Majaji na Mahakimu) kwa kuwaongezea ujuzi kwa njia ya mafunzo, kuweka mazingira rafiki ya usuluhishaji na kutoa elimu au hamasa kwa umma kuhusu umuhimu wa usuluhishi. Kwa upande wa Wadau wa Mahakama wanapaswa kutambua nafasi yao katika usuluhishi, kutoa ushirikiano kwa msuluhishi, kutokuwa na msimamo kuhusu jambo/mgogoro unaobishaniwa.

Jaji Mfawidhi alisema, tafiti zinaonesha kwamba Nchi nyingi zilizoendelea, Usuluhishi unamaliza zaidi ya asilimia 90 ya migogoro inayofikishwa Mahakamani. Sisi pia kama Nchi bado tunayo nafasi ya kuhimiza usuluhishi katika utatuzi wa mashauri tuliyonayo kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya uchumi wa Nchi yetu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Queen Sendiga alisema, kama ambavyo kauli mbiu inavyosema, itasaidia kutekelezeka kwa upana na usahihi migogoro na hivyo kuwezesha migogoro kupungua.

“Niwapongeze Mahakama na Wadau nikiamini kwamba tunakwenda kupeleka elimu kwa jamii inayotuzunguka, lakini pia katika suala hili ningependa kutoa wito wetu kwamba kama tutaenzi vizuri utatuzi huu wa migogoro na kama ambavyo pia maandiko matakatifu yametuonesha, viongozi wetu wa dini pia wametuambia, tutakwenda kufanya jambo kubwa sana.’’ Alisisitiza Mkuu wa Mkoa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Queen Sendiga wakiwasili tayari kwa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga akikagua gwaride maalum kuashiria uzinduzi wa shughuli za kimahakam kwa Kanda hiyo .

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dustan Ndunguru (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wananchi walihudhuria sherehe hizo katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga. Kushoto ni Jaji wa Kanda hiyo, Mhe.Abubakar Mrisha na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe Queen Sendiga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe Queen Sendiga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru na kulia ni Jaji wa Kanda hiyo, Mhe. Thadeo Mwenepanzi.

Kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mwandishi wetu Aidan Robert anaripoti kuwa, Kanda hiyo imejipanga kukabiliana na changamoto ya mwamko duni wa jamii wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi ili kuifanya jamii ya Mkoa huo kuona umalizwaji wa mashauri kwa njia ya usuluhishi kama njia nzuri ya kuwasaidia kumaliza mashauri yao haraka.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha ameeleza hayo wakati wa hafla ya Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu na kusema kuwa wananchi wengi wa Mkoa huo hawataki kesi zao kuisha kwa njia ya usuluhishi.

Mhe. Mlacha alisema kuwa mkoa wa Kigoma unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuamua mashauri kwa njia ya usuluhishi kutokana na wananchi wengi mkoani Kigoma kutotaka kesi zao kuisha kwa njia ya usuluhishi badala yake kutaka mashauri yao kutolewa hukumu na Hakimu au Jaji jambo ambalo kwa sasa linawapa kazi kubwa ya kufanya kukabiliana na hali hiyo.

Akitoa takwimu kuhusiana na hali hiyo Jaji Mlacha alisema kuwa mwaka jana jumla ya mashauri 5366 yalifunguliwa kwenye Mahakama za Mkoa Kigoma ikiwemo Mahakama Kuu hadi Mahakama za Mwanzo lakini ni mashauri 256 yaliyomalizika kwa njia ya usuluhishi sawa na asilimia 4.8 ya mashauri hayo na yaliyobaki yote yalimalizika kwa njia ya hukumu.

Alitaja sababu za kukwama kwa mashauri mengi kuamuliwa kwa njia ya usuluhishi kuwa ni pamoja na kukosena kwa utayari baina ya watu wanaohusika na shauri husika, kusuluhishwa bila kuwa na nia ya kutaka usuluhishi hivyo suala la usuluhishi  kushindikana.

Kwa upande wake Mgeni Rasmi wa Hafla, ambaye alikuwa Mkuu wa mkoa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye alisema kuwa utatuzi wa mashauri kwa njia ya usuluhishi ni muhimu katika kuleta nafuu pamoja na kukabiliana na muda, gharama lakini kurudisha amani kwa jamii husika.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wananchi na wadau wote wanaosimamia masuala ya kupata haki kutumia fursa ya kushughulikia mashauri yao kwa njia ya usuluhishi kutokana na faida zake kwa wananchi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) mkoa Kigoma, Eliutha Kivilyo alisema kuwa dhana ya kutatua mashauri kwa njia ya usuluhishi ni muhimu katika kushughulikia mashauri yakaisha kwa amani ambapo TLS inaunga mkono mpango huo kwani unafaida kubwa katika suala zima la utoaji haki kwa wananchi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akizungumza katika hafla ya kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama mkoani Kigoma. Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Kanda hiyo Bangwe Kigoma.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha  akikagua gwaride maalum la kikosi cha jeshi la kutuliza ghasia cha jeshi la polisi mkoani Kigoma  katika hafla ya kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama Kanda ya Kigoma.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye akizungumza katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, siku maalum ya kuanza kwa mwaka mpya wa shughuli za mahakama mkoa Kigoma zilizofanyika kwenye jengo la Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (kushoto) akiongoza maandamano ya kitaaluma (kushoto kwake) ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mh. Stephen Magoiga, na aliye nyuma yao ni Mkuu wa Mkoa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye wakiwa katika maandamano ya kilele cha Siku ya Sheria nchini. 


Kwa upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mwanahabari wetu Mohamed Kimungu anaripoti kuwa, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube amesisitiza matumizi ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro.

Akizungumza katika jana tarehe 01 Februari, 2023 katika hafla ya kilele cha Siku ya Sheria iliyofanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Makube alisema kuwa, ni muhimu na ni vyema kukimbilia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro mbalimbali inayotukabili.

Alieleza katika hotuba yake kwamba, utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ina manufaa mengi kama upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa gharama nafuu, kupunguza milundikano ya mashauri Mahakamani na kuimarisha Amani na ustawi wa jamii.

Mhe. Makube amepongeza juhudi za Mahakama za kuandaa Mahakimu kiujuzi ili kuweza kuendesha na kusimamia zoezi zima la usuluhishi kupitia mafunzo mbalimbali yanayotolewa na Chuo Cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), huku akikiri kuwa, mafunzo hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwapa uwezo Mahakimu wa kuendesha zoezi hilo kwa kufuata taratibu za sheria za usuluhishi na kusisitiza kuwa Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea na waendesha mashtaka wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri njia sahihi ya utatuzi wa migogoro ili kuweza kuwasaidia wadau wa Mahakama kumaliza mashauri mengi ndani ya muda mfupi.

Naye, Mhe Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba ameipongeza Mahakama kwa kufanikisha vyema Wiki ya Sheria  kwa kuwafikishia elimu ya sheria wananchi wa Mkoa huo ikiwa ni pamoja na kufahamu hatua za ufunguzi wa mashauri ya mirathi, haki jinai kwa watoto, mashauri ya ndoa na kufikia makundi ya wanafunzi Mashuleni, Hospitali na kufanya vipindi vya redio.

Mhe Kindamba ameeleza pia kupitia maadhimisho haya ni matumaini yake kuwa, Maafisa wa Mahakama wataweza kuwaongoza wananchi kutatua  migogoro kwa njia ya usuluhishi na kwa upande wa wadau wa Mahakama kutambua nafasi yao katika usuluhishi.

Kwa upande wake, Wakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Bw. Moses Mwampashi ameipongeza Mahakama kwa kuja na kauli mbiu hii ya “UMUHIMU WA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI KATIKA KUKUZA UCHUMI ENDELEVU: WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU” kwa kauli mbiu hiyo inawataka wadau wote  kutatua migogoro ya aina zote kwa njia ya usuluhishi. Aliongeza kuwa, kwa upande wao Mawakili kaulimbiu hiyo ni dhana pana lakini inatekelezeka kwa kuanza kubadili fikra na kuelimisha umma na jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa usuluhishi wa migogoro nje ya Mahakama.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube akizungumza wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 01 Februari katika Viwanja vya Mahakama hiyo.
Mkuu wa Mkoa-Songwe, Mhe. Waziri Kindamba akisisitiza jambo alipokuwa kwenye hafla ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama-Songwe wakiwa katika hafla hiyo.
Baadhi ya kundi la wageni waalikwa/Wana Songwe wakiwa katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini.

Meza kuu katika picha ya pamoja, katikati ni Mkuu wa Mkoa Songwe, Mhe. Waziri Kindamba, Kulia ni Mkuu wa Wilaya Momba na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube.


Tukiangazia, Mahakama Kuu-Kanda ya Tabora, Mwanahabari wetu Amani Mtinangi anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis amewapongeza watumishi wa Mahakama na wadau wote kwa namna ambavyo walishiriki katika maadhimisho ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka huu. Alieleza kuwa usuluhishi ni takwa la kikatiba, kisheria na kidini huku akinukuu Ibara, sheria, kesi na vifungu kadha wa kadha vya Biblia Takatifu na Kuran Tukufu, Sera pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Mhe. Amour alieleza faida za usuhishi kuwa, unasaidia pande zilizohitilafiana kusikilizana, kutafakari mawazo mbadala, uhifadhi wa siri za pande mbili kuhusu mgogoro mikubwa na midogo kwa haraka, kuondoa tofauti zao kwa ufanisi, unaokoa muda na fedha, na unapunguza Mlundikano wa mashauri Mahakamani.

Aidha, alitaja changamoto zinazofanya jamii yetu kutotoa kipaumbele  katika usuluhishi kuwa ni pamoja na kukosekana kwa mamlaka za kisheria za usuluhishi kwa baadhi ya wadaawa, kukosekana kwa mawasiliamo baina ya wadaawa au wawakilishi wao, wadau kutokubaliana na mambo msingi kuhusu mgogoro, wasuluhishi kutoelewa kwa kina sababu za mgogoro.

Naye Wakili Idd Mgeni, Mkuu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hotuba yake alimnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Chama cha Wanasheria wa Serikali 29/09/2022 ambapo alimnukuu akisema:- “Lazima wanasheria wawe makini kusikiliza migogoro na kuhakikisha inatatuliwa kabla ya kufikishwa Mahakamani”

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) alipongeza Mahakama kwa kazi kubwa ya utoaji elimu, jinsi inavyoshirikiana na wadau wengine pamoja na kuwaunganisha wadau na taasisis mbalimbali kati utendajikazi wake wa kila siku.

Katika picha ni Mgeni rasmi (katikati) ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Amour Khamis akiwa katika picha ya pamoja  na Kamati ya Ulizni na Usalama ya Mkoani Tabora.

Mwakilishi wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Lois Peter Bura akisema neno katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini.

Kwa upande wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mwandishi wetu Angel Meela anaripoti kuwa, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Joachim Tiganga ) alifafanua kauli mbiu ya mwaka huu na kueleza kuwa  kauli mbiu hii imejikita katika kuonyesha jamii ya watanzania na wapenda haki wote faida ya kutatuta migogoro kwa njia ya usuluhishi alifafanua kwa kutaja mambo manne.

Aliyataja mambo hayo ambayo ni pamoja na, Upatanishi kwa nia ya kurudisha mahusiano ya kirafiki kama ilivyo kwenye sheria ya ndoa; pili, Mazungumzo kufikia maafikiano, ambayo mara nyingi hufanyika kwenye migogoro ya kibiashara; tatu, Upatanishi kama ambavyo inakuwa kwenye mashauri yote ya madai, na nne, usuluhishi kama unavyoelekezwa kwenye Sheria ya kazi au kama inavyoelezwa kwenye Sheria ya Usuluhishi Sura No. 15 ya Sheria za Nchi.

“Ni wazi kwamba, kadri idadi ya watu inavyoongezeka inaenda sambamba na ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa muingiliano wa shughuli za kibinadamu, biashara, uchumi na kadhalika migogoro nayo huongezeka, kuongezeka kwa migogoro huhitaji mbinu bora za utatuzi, hivyo itoshe tu kusema kuwa, kwa wakati tulionao utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unahitaji kupewa kipaumbele zaidi leo kuliko jana, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi yetu na dunia kwa ujumla” alisema

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imehitimisha  kilele cha wiki ya sheria katika ikipambwa na burudani mbalimbali kutoka  kwaya ya Mahakama Kuu Arusha zilizobeba ujumbe/elimu  juu ya umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kama ilivyo kauli mbiu ya wiki na siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu 2023.

Akitoa takwimu za mashauri yaliyomalizika kwa Usuluhishi, Mhe Tiganga alisema kuwa, kwa mwaka 2022 ni wastani wa asilimia 13.3 pekee yalifanikiwa kwa njia ya usuluhishi na asilimia 86.7 yalishindwa.

Mheshimiwa Jaji Tiganga alitoa rai kwa  wadau wote wa Mahakama na sheria hasa  Mawakili wa Wadaawa,  kuhakikisha wanazingatia sheria  zinazohusiana na usuluhishi wa migogoro.  Pia alitoa wito kwa Mawakili wote kubadilika na kuingiwa na tahadhari ya Usuluhishi hasa kwa kuwashauri wateja wao ipasavyo kwani kwa kufanya hivyo watawezesha faida zitokanazo na kusuluhisha migogoro bila kwenda kwenye usikilizwaji kimahakama kuwa ndio udhahiri wa kumaliza shauri. Pia amewaomba wananchi kwamba wawe tayari kupokea na kuzitumia njia za usuluhishi kama njia mbadala za kutatua migogoro baina yao

Naye; Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela (mgeni maalum) alisema  kuwa Mahakama ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na watu kwa ujumla. Pia alisema Ofisi yake iko tayari kushirikiana ns Mahakama katika shughuli zote zinazochangia maendeleo ya nchi.

Nae Wakili wa Serikali Mkuu ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Veritasi Mlay alisema Ofisi yake itaendelea kusimamia vyema matakwa ya Serikali juu ya usuluhishi wa migogoro mbalimbali ikiwemo ya kibiashara na uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi na uchumi endelevu.

Naye, Mhe. George Njooka, Mwenyekiti wa ‘TLS-Chapter ya Arusha’ katika hotuba yake iliyosheheni vionjo elimu na mifano mbalimbali ya usuluhishi alisema wananchi wakielewa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi itasaidia kufikia malengo na nchi yetu kuwa na amani. Aliongezea kuwa TLS imedhamiria usuluhisho kwa vitendo na kutoa elimu kwa Mawakili wengi wa Arusha juu ya usuluhishi kwa vitendo .

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Joachim Tiganga-Mgeni Rasmi akizungumza wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini tarehe 01 Februari, 2023 iliyofanyika katika Viwanja vya 'IJC' Arusha.

    Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Mhe. Jaji Joachim Tiganga (mgeni rasmi), kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela (mgeni maalum).

Mwenyekiti wa TLS-'Chapter' ya Arusha, Bw. George Njooka akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika tarehe 01 Februari, 2023 katika Viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.


Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Veritas Mlay akizungumza katika hafla ya Siku ya Sheria iliyofanyika tarehe 01 Februari, 2023 katika Viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

    Baadhi ya Watumishi wa Mahakama  Kanda ya Arusha wakionyesha igizo linalohusu usuluhishi.

    Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela akizungumza wakati wa hafla hiyo.


Kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mwandishi wetu Emmanuel Oguda anaripoti kuwa MAWAKILI WAPEWA WITO KUSAIDIA WANANCHI KUFIKIA SULUHU; ambapo Jaji Mfawidhi wa  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Athuman Matuma ametoa rai kwa Mawakili wa Serikali na Kujitegemea kusaidia wananchi/wateja wao kufikia suluhu katika mashauri yao kuokoa muda na gharama.

Akizungumza wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama hiyo jana tarehe 1 Februari, 2023, Mhe. Matuma amesema kuwa, "Mawakili wasaidieni wananchi kutatua migogoro yao kwa usuluhishi, kwa kufanya hivyo, mtawasaidia wananchi kuokoa muda na gharama, ili wananchi hao waelekeze muda katika shughuli za uzalishaji mali kujenga uchumi wao binafsi na wa nchi pia.’’. Pia amewataka mawakili kutoirudisha tena Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwenye Mlundikano wa mashauri ambapo kwa sasa hakuna shauri hata moja la mlundikano ndani ya Kanda ya Shinyanga.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo ametoa rai kwa Viongozi katika ngazi za Shina, Vijiji na Kata kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kwani kwa kufanya hivyo Mahakama itamaliza Mlundikano wa mashauri kwa kuwa migogoro mingi sasa itatatuliwa kwa njia ya usuluhishi kuanzia ngazi za chini.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mfawidhi (M) Shinyanga, Bw. Solomon Lwenge, ameihakikishia Mahakama kuwa, kama Serikali wataendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuamua mashauri kwa njia ya usuluhishi. "Migogoro inafanya mitaji kukaa bila uzalishaji hivyo kukwamisha maendeleo yaliyokusudiwa na kuongeza uadui baina ya wananchi’’ alisema Bw. Lwenge.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Shinyanga (TLS), Bw. Shaban Mvungi  alisema kuwa, kama Mawakili wapo tayari kuelimisha umma kubadilisha mtazamo wa wananchi kwa kutoa elimu ya usuluhishi ili kumaliza tofauti zao pasipo kufikishana Mahakamani. ‘

Awali, akitoa salamu za Mkoa, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Bw. Moses Chila, ameihakikishia Mahakama kuwa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga itahakikisha inatekeleza dhana ya usuluhishi kwa vitendo na kushirikiana bega kwa bega na Mahakama katika kutekeleza dhana hiyo yenye lengo la kukuza uchumi endelevu.

(Habari hizi zimekusanywa na kuhaririwa na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni