Na Mwandishi wetu-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania tarehe 1 Februari, 2023 iliazimisha Siku ya Sheria kuashiria mwanzo mpya
wa shughuli za kimahakama. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wananchi nchini
kote, huku ujumbe mkuu ukiwahimiza wananchi kutatua migogoro kwa njia ya
usuluhishi kwanza badala ya kukimbilia mahakamani na kujiepusha na Mawakili
vishoka.
Mwandishi wetu
Stephen Kapiga kutoka Mahakama
Mwanza anaripoti kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mwanza, Mhe Dkt Ntemi Kilekamajenga amewaasa wananchi wa Mikoa ya Mwanza na
Geita kuepuka Mawakili wasio na sifa, yaani vishoka kwani ndio wamekuwa chanzo
cha mrundikano ya migogoro isiyofika mwisho mahakamani.
“Nawaomba sana wananchi
muweze kuwaepuka Mawakili vishoka kwani wao ndio wamekuwa wakisuka zaidi
migogoro ili kuona kuwa Mahakama inashindwa kumaliza migogoro hiyo. Ni muhimu
sasa kuanza kutumia Mawakili wanaotambulika,” alisema.
Akizungumza wakati wa
maadhimisho hayo, Jaji Kilekamajenga alisema kuwa amekaa na kuzungumza na Mawakili
wote wa Mkoa wa Mwanza kuhusu umuhimu wa kauli mbiu ya Siku ya Sheria, hivyo
kuwataka kabla ya kukimbilia kuleta kesi mahakamani waaze kutatua mgogoro kwa
njia ya usuluhishi.
Naye Mwenyekiti wa Chama
cha Mawakili Tanganyika Mkoa wa Mwanza, Wakili Lenin Njau aliishukuru Mahakama
ya Tanzania kwa kauli mbiu hiyo kwani imeamsha uelewa wa umuhimu wa utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi.
“TLS Mkoa wa Mwanza
tumejipanga kwani tunajua umuhimu huu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya
usuluhishi ndio maana kwa mwaka 2019 tulianzisha kituo cha kimataifa cha
utatuzi wa migogoro ya kimataifa na kituo hiki kimekuwa kikiendesha mafunzo kwa
Mawakili ili kuweza kuwa mahiri katika utatumizi wa migogoro,” alisema.
Kwa upande wake, Wakili
wa Serikali Mkoa wa Mwanza Mamti Sehewa alisema utatuzi wa migogoro kwa njia ya
usuluhishi unaokoa muda wa wadau, hivo kuweza kujikita kwenye shughuli zingine za
kiuchumi na kukuza uchumi wao.
Akiongea katika hafla
hiyo, mgeni mwalika ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala
aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuja
na kauli mbiu hiyo kwani itachangia kudumisha amani na mshikamano kwa wananchi
kwani katika usuluhishi huwa hakuna anayeshindwa au kushinda bali wote huwa ni
washindi.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na burudani mbali mbali kutoka katika vikundi vya kwaya, band na maigizo ambayo kwa ujumla yaliwavutia watu wote walihudhuria.
Akizungumza wakati wa
hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe.
Paul Ngwembe alisema kuwa wamefanikiwa kuwafikia wananchi 51,000 katika Wilaya
zote za Morogoro.
Idadi hiyo inajumlisha wanawake
27,730 na wanaume 23,858 na kwa upande wa Morogoro mjini jumla ya wananchi elfu
9, 178 wamefikiwa, ikiwa ni ongezeko la watu 2,490 kutoka mwaka 2022 ambapo
wananchi 6,731 ndio waliofikiwa.
Kazi hii imefanywa na
Mhakama kwa ushirikiano mkubwa toka kwa wadau. Idadi hii haijajumuisha Morogoro
Mjini,” alisema.
Aidha, Jaji Ngwembe
alisema kuwa kazi ya kutoa maamuzi inawataka Majaji na Mahakimu wawe na uadilifu
usio tia shaka kwani Mahakama ndio chombo pekee kilichokathimiwa majukumu ya
kutoa haki nchini, hivyo aliomba viongozi wa dini waendelee kuiombea Mahakama.
Naye Mgeni Maalum,ambaye
ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa alisema ni ukweli usiopingika
kuwa viongozi wa Mahakama wanashirikiana vizuri na Mihimili mingine hususani Mhimili
wa Serikali, huku akiamini utekelezaji wa kauli mbiu yam waka huu 2023 utapunguza
mzigo mkubwa wa kesi mahakamani.
Akitoa salamu toka kwa
Chama Cha Mawakili wa Kujitegemea (TLS), Wakili Azizi Mahenge alishukuru kwa ushirikiano mkubwa
wanaoupata kutoka mahakamani na kumpongeza Jaji Mfawidhi kwa kuasisi programu
ya msaada wa kisheriakwa wananchi.
Kwa upande wake, Richard Matasha kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara anaripoti kuwa maadhimisho ya Siku ya Sheria yameadhimishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu, ambapo shughuli hiyo ilitanguliwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Zainab Mruke kukagua gwaride lililokuwa limeandaliwa na kikosi cha Jeshi la Polisi.
Baada ya gwaride hilo, Msajili
wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara, Mhe. Amiri Msumi aliwakaribisha wawakilishi
kutoka dini mbalimbali ili kukabidhi shughuli nzima mikononi mwa Mungu.
Utambulisho ukafuata wa jukwaa kuu pamoja na wageni mbalimbali mashuhuri.
Kisha Naibu Msajili akaikaribisha
kwaya ya Mahakama Kanda ya Mtwara kutumbuiza kwa muziki mwanana uliokonga nyoyo
za kila aliyehudhuria. Baada ya hapo salamu kutoka kwa viongozi mbalimbali
zilifuata ambao kwa ujumla walisistiza umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia ya
usuluhishi.
Ikafuata hotuba ya Jaji
Mfawidhi ambaye naye alisisitiza kuhusu kauli mbiu ya mwaka 2023. Alitumia
fursa hiyo kuwaaga rasmi watumishi wa Mahakama Kanda ya Mtwara baada ya kuhamishiwa
kituo kingine cha kazi.
Kabla ya kuhitimisha
maadhimisho hayo, Naibu Msajili aliikaribisha kwaya ya Mahakama kwa mara
nyingine kuwasilisha shairi la kipekee lililotungwa na Jaji wa Mahakama Kuu
kutoka Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Eliamani Laitaika. Hakika shairi hilo liliteka
hisia za hadhira kutokana na utamu wa tenzi na ujumbe wake.
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi VETA ni moja kati ya wale walioshirika sherehe hiyo.
Naye
Paul Pascal kutoka Mahakama Kuu Moshi anaripoti kuwa Mahakama
Kuu Kanda ya Moshi imeadhimisha Siku ya Sheria nchini mwaka 2023 katika viwanja
vya Mahakama Kuu Moshi, ambapo mgeni rasmi alikuwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Juliana
Massabo ambaye ametanabaisha kuwa kauli mbiu ya kwa mwaka 2023 sio
utashi wakutungwa bali ni takwa la kikatiba ya Jamuhuri ya Muungani wa Tanzania
ya mwaka 1977 kupitia Ibara ya 107A (2) (d).
Alisema
Ibara hiyo inatamka bayana kuwa “katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na
jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo yaani kukuza
na kuendeleza usuluhishi baina ya
wanaohusika katika migogoro”.
Sambamba
na kuonyesha kuwa utatuzi wa migogoro ni suala la kikatiba Jaji Mfawidhi huyo aliwaeleza
wananchi baadhi ya sheria zilizotungwa kwa weledi kuwezesha usuluhishi wa
migogoro katika taifa, zikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Madai Sura ya 33, Sheria
ya Taasisi za Kazi na.7/2004 (The Labour Institution Act), Sheria ya Mahakama
za usuluhishi wa migogoro ya ardhi sura 216, Sheria ya Ndoa Sura ya 29 na Sheria
ya Bima na 10/2009 sura ya 394.
Alibainisha
faida kuu za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, ikiwemo upatikanaji wa
haki kwa wakati kwa kuondokana na milolongo ya kisheria katika shauri, upatikanaji
wa haki kwa gharama nafuu kutokana na kutokuwepo kwa gharama za uendeshaji wa
shauri, kudumisha umoja na mshikamano katika jamii ambapo njia hiyo huondoa
uhasabana baina ya wadaawa na kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani kwa
kuwa mengi yatamalizika kwa maridhiano.
Naye
Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Tamali Mndeme katika hotuba
yake alisema kauli mbiu yam waka huu wa 2023 ya Siku ya Sheria ina maana kubwa
katika kukuza uchumi wa nchi kama ikitumika kimamilifu kwenye kutatua migogoro
mbalimbali.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Chapta ya Kilimanjaro,
Wakili David Shilatu katika hotuba yake alibainisha kuwa dhima ya usuluhishi
imekuja wakati sahihi, hivyo akaomba juhudi zifanyike kuwaelimisha wananchi faida
za utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Akiwasilisha
salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu alimueleza Jaji
Mfawidhi kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Mkoa iko tayari kutoa ushirikiano utakaohitajika katika utekelezaji
wa kauli mbiu ya mwaka 2023.
Kutoka Mahakama Katavi, James Kapele anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Mwananvua
Mrindoka ambaye alikuwa mgeni maalum katika maadhimisho ya Siku ya Sheria amefurahishwa
na kauli mbiu ya mwaka huu wa 2023 ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
mrundikano wa mashauri mahakamani.
Akiwasilisha hotuba yake,
Mhe. Mrindoka amewasihi wadau wote wa haki mkoani hapa kuitumia kauli mbiu hiyo
kwa ufasaha kwa kuwa mashauri mengi yatamalizwa kwa usuluhishi isipokuwa yale
tu ambayo sheria za nchi haziruhusu kusikilizwa kwa njia hiyo.
“Utatuzi wa migogoro kwa
njia ya usuluhishi tena kwa wakati utazisaidia Mahakama zetu kumaliza kabisa
tatizo la mlundikano wa mashauri. Hii inatokana na ukweli kwamba wadaawa
wengine hupenda mashauri yao kusikizwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho hata kama
sheria zetu zinaruhusu migogoro hiyo kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi,” alisema.
Kwa upande wake, Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye amesisitiza
umuhimu wa kauli mbiu hiyo kuwa imekuja kwa wakati sahihi kwa kuwa sheria nchini
zinaruhusu utatuzi wa migogooro kwa njia ya usuluhishi.
“Katika
nchi yetu, mfumo wa utatuzi wa migogoro kwa upatanishi upo kwenye sharia zetu,
lakini bado nwananchi hawajui na hautumiki ipasavyo hasa kwa migogoro iliyopo mahakamani. Katika Mahakama
zetu miongoni mwa kesi zinazochukua muda mrefu ni mashauri ya madai na sababu
moja wapo ni kutojua sheria na manufaa yake,” alisema.
Awali wakisoma hotuba
zao, Mwenyekiti wa Maraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mpanda, Mkuu wa Ofisi
ya Mashtaka Mkoa wa Katavi na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika kwa
ujumla wao wameipongeza Mahakama kwa kauli mbiu hiyo na kuonyesha utayari wa
kuitekeleza kwa vitendo wakishirikiana na wadau wengine katika kada ya sheria.
Mtendaji wa Mahakama Katavi,Bw. Allan Mwela akitoa utambulisho wa wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni