·Amwaga sifa Majaji kuchapa kazi
·Kwaya ya Ng’aring’ari yamkosha, atoa zawadi ya millioni moja
Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 1 Februari, 2023
amewaongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Sheria na kuipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa uboreshaji mkubwa wa huduma za utoaji haki kwa wananchi unaoendelea.
Akizungumza katika
maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini hapa,
Rais Samia ameonyesha kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania
kupitia Mpango Mkakati ulioanza kutekelezwa toka mwaka 2015.
“Naipongeza sana Mahakama
kwa maboresho mnayoendelea nayo toka mwaka 2015 pale mlipoamua kuandaa Mpango
Mkakati wa Kwanza ambao umeleta mafanikio chanya,” alisema.
Mhe. Dkt. Samia alitoa
mfano kwa mwaka 2022 ambapo Mahakama ilifunga mwaka ikiwa na mashauri 64,001,
yakasajiliwa mengine 244,292 katika ngazi zote, hivyo kufanya mwaka huo kuwa na
mashauri 304, 293, lakini yaliyomalizika yalikuwa 253,495.
“Ni kazi kubwa sana
imefanyika, hongereni sana. Nakubaliana nanyi kuongezeka kwa idadi ya Majaji wa
Mahakama Kuu toka 78 hadi 100 Agosti 2022 imekuwa chachu ya mafanikio hayo. Hili
pia linachangiwa na dhamira ya dhati ya uongozi uliopo na Mahakimu wenyewe,”
alisema.
Rais Samia alibainisha
kuwa kwa sasa Majaji wamejielekeza kwenye utendaji wa haki na wanaendelea kutoa
haki jinsi nafsi na sheria zinavyowatuma. “Hongereni sana Majaji, tunawashukuru
sana. Naomba tuongeze kasi ili takwimu hizo zishuke lakini pia tujikite
kuangalia ubora wa uamuzi unaotoka kwa kila kesi ama shauri,” alisema.
Mhe. Dkt. Samia alieleza
kuwa Serikali itaendelea kufanyia kazi suala la upungufu wa watumishi na
maslahi na kuwahakikishia Majaji kuendelea kufanya kazi kwani maslahi yao yataendelea
kuboreshwa.
Aidha, Rais Samia ameipongeza
Mahakama kwa ujenzi wa miundombinu na kuendelea kusogeza huduma karibu na
wananchi. “Nimefurahi kukamilika kwa taratibu za upatikanaji wa huduma za Mahakama
Kuu katika Mikoa minane ya Singida, Pwani, Songwe, Katavi, Geita, Njombe,
Simiyu na Lindi na mpango wa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika maeneno
mengine, ikiwemo Pemba,” alisema.
Kadhalika, amewapongeza watendaji
wa Mahakama kwa kutumia vizuri fedha zilizotolewa kukamilisha miradi mbalimbali
itakayoimarisha utendaji.
Rais Samia ameeleza
kutambua uwepo wa fedha kutoka Benki ya Dunia ambazo zimeimarisha miundombinu
ya Mahakama, ikiwemo Mahakama za Mwanzo 60 na majengo mengine 18 ambapo kati ya
hayo, 11 ni Mahakama za Wilaya na saba ni Mahakama za Mwanzo.
“Hii ni ishara nyingine
ya azma ya Mahakama ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi. Rai yangu
kwa uongozi wa Mahakama ni kwamba miradi hiyo izingatie ubora unaoendana na
fedha. Serikali itaendelea kushirikiana na Mahakama kwa kuwezesha miradi hiyo ili
kuweka mazingira wezeshi ya kufanyia kazi na kusaidia wananchi kupunguza
gharama katika kutafuta haki,” alisema.
Rais Samia ameelezea azma
ya Serikali yake kuhakikisha taasisi zinazoshirikiana na Mahakama katika mnyororo
wa utoaji haki, ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zinapata pia miundombinu
wezeshi. Amesema azma yake ni kuona shauri linalofunguliwa polisi linasomeka hivyo
hivyo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na pia mahakamani ili kusiwe na hali ya kupindisha
haki.
Maadhimisho hayo
yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, ambaye ndiye aliyekuwa mwenyeji wa
Rais Samia, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, Majaji wa Mahakama Kuu, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert
Chuma pamoja na watumishi wengine.
Wageni wengine walikuwa Jaji
Mkuu wa Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki
Feleshi, Spika wa Bunge la Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri
wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro na Mawaziri wengine pamoja na
Naibu Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,
Wakuu wa Wilaya, Viongozi wastaafu wa Mahakama na Serikali, Rais wa Chama cha
Mawakili Tanganyika, Prof. Edward Hosea na wananchi kwa ujumla.
Rais Samia aliwasili
katika Viwanja vya Chinangali majira ya saa 3:10 hivi asubuhi na kupokelewa na
mwenyeji wake pamoja na viongozi wa Mahakama na Serikali. Baada ya kufika jukwaa
kuu Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki ulipigwa kabla ya Mshereheshaji Mkuu,
ambaye ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kuwakaribisha viongozi wa dini
kuyaweka maadhimisho hayo mbele za Mungu.
Baada ya sala hizo, Rais
wa TLS alikaribishwa kutoa salamu. Katika salamu zake, Prof. Hosea alisema kuwa
chama chake kimeweka dhana ya suluhu kwa vitendo kwa kuanzisha Kituo cha
Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro Tanzania.
“Tunaamini kwa
kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria Kituo hiki kitaiweka Tanzania katika
ramani ya Afrika na Dunia kwa kutekeleza dhana ya kutatua migogoro ya
kibiashara za kimataifa na ile inayohusu wawekezaji kwa njia ya suluhu. Hatua hii
itaimarisha kwa vitendo na kukuza mazingira Rafiki kwa wawekezaji na wananchi
wa Tanzania na kujenga imani katika mifumo ya utoaji haki na maendeleo,”
alisema.
Katika salamu zake,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kuanzishwa kwa Kituo cha Kimataifa cha
Usuluhishi kitafungua ukurasa mpya, hivyo kuwawezesha wadaawa na wanasheria kwenye
migogoro kuweza kuishughulikia na kuimaliza pasipo kulazimika kwenda kwenye
mabalaza ya nje katika mashauri hayo.
Mhe. Dkt. Feleshi alibainisha
kuwa wakati umefika wa kubadilisha Sheria ya Mwenendo wa Madai ili shauri la
madai lipate sifa ya kusajiliwa mahakamani mara baada ya kupata uthibitisho
kwamba zile ngazi za kupitia usuluhishi zimeshindikana.
Alimweleza Rais Samia kuwa
ofisi yake na ile ya Wakili Mkuu wataendelea kusimia vyema kwa niaba ya
Serikali matakwa ya sheria ya kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na
wataendelea kusimamia kwa karibu maelekezo aliyoyatoa kuhusu jambo hilo ili
kuhakikisha migogoro inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
“Nitoe rai kwa Majaji na
Mahakimu kuwa tayari kuwasilisha ofisini kwangu kwenye dawati linaloshughulikia
utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali, kuhusu Wakili yoyote au mtendaji yoyote
serikalini, ambaye kwa namna yoyote ile atathibitika kudhoofisha juhudi za
Serikali na Mahakama za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi,” alisema.
Kabla ya Jaji Mkuu wa
Tanzania kupanda jukwaani kuongea na Watanzania, Mhe. Chuma alikaribisha
kikundi cha Kwaya ya Mahakama, maarufu Ng’aring’ari ambacho kilikonga nyoyo za
wananchi waliokuwa wamefurika katika Viwanja vya Chinangali. Mawaziri na Naibu
Mawaziri na wananchi wengine walishindwa kujizuia, wakaamua kuachia viti vyao na
kujimwaga uwanjani kufuatia burudani safi ya nyimbo iliyokuwa inatolewa na kwaya
hiyo.
Wakati anazungumza na
Taifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa yanarushwa mubashara na vituo mbalimbali
vya runinga, Rais Samia aliwazawadia shilingi millioni moja Wanakwaya hao baada
ya kukoshwa na uimbaji murua katika hafla hiyo.
Katika kukamilisha
maadhimisho hayo ya Siku ya Sheria yanayoashiria mwaka mpya wa shughuli za kimahakama,
Jaji Mkuu wa Tanzania alikagua gwaride maalumu lililokuwa limeandaliwa na Jeshi
la Polisi kwa heshima yake na kwa ajili ya shughuli hiyo.
Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Prof. Edward Hosea akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (juu na chini) akiingia katika Viwanja vya Chinangali.
Meza Kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) ikiimba Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki. Picha chini ikifuatilia matukio mbalimbali katika maadhimisho hayo.
Sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania ikifuatilia matukio mbalimbali kwenye maadhimisho hayo. Chini ni viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali waliopo kazini na wastaafu (juu na chini) wakiwa kwenye viwanja vya Chinangali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiondoka katika viwanja vya Chinangali baada ya kukagua gwaride lililokuwa limeandaliwa kwa heshima yake katika maadhimisho ya Siku ya Sheria.
Gwaride la Jeshi la Polisi likiondoka katika viwanja vya Chinangali.
(Picha na Innocent Kansha na Faustine Kapama - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni