·Yahimiza mchakamchaka kila kona kujiwinda na mashindano Mei Mosi
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Dar es Salaam
Kamati Tendaji ya Timu ya
Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) hivi karibuni ilikutana ili kujadili na
kutathmini maendeleo ya Timu hiyo na pia kujiandaa na kuweka mikakati namna
itakavyoshiriki katika mashindano ya Mei Mosi yanayotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro
kuanzia tarehe 14 Aprili, 2023 hadi tarehe 01 Mei, 2023.
Katika taarifa
iliyotolewa na Katibu wa Mahakama Sports Taifa Robert Tende iliwanukuu Mwenyekiti
Wilson Dede pamoja na Afisa Michezo Nkurumah Katagira wakiwahimiza viongozi
wawakilishi mikoani wahakikishe wanasimamia mazoezi ipasavyo kwa ajili ya
kupata timu nzuri itakayoiwakilisha Mahakama katika mashindano hayo.
“Washindi wa kwanza wote
hupewa zawadi siku ya kilele cha Mei Mosi ambayo mgeni rasmi hutoa vikombe na
mara nyingi huwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni heshima kubwa.
Wanamichezo wa Mahakama wachukulie mashindano haya kwa umuhimu unaostahili,
kwani ni sehemu pekee na kubwa ambayo Mahakama itajidhihirisha katika ukubwa
wake katika utoaji haki” sehemu ya taarifa hiyo ilieleza ikimnukuu Dede akisema.
Naye Katibu wa Mahakama
Sports alieleza katika taarifa hiyo kuwa kila mara watumishi wa Mahakama kwa
kushirikiana na wadau wengine wamekuwa wakishiriki katika mazoezi na kufanya
mabonanza mbalimbali ndani na nje ya Mahakama, hivyo kujenga mahusiano mazuri
na jamii inayowazunguka. Alisema mazoezi hayo pia yanajenga afya, kujikinga na
magonjwa yasiyoambukiza na kuleta hamasa kwenye akili, hivyo kupelekea uwepo wa
tija katika taasisi.
“Mei Mosi ni michezo ambayo inashirikisha wafanyakazi wa taasisi zote na washiriki wa michezo hii ni wafanyakazi halali wa taasisi, mashirika, wizara na makampuni binafsi, hivyo tunatakiwa kujiandaa vizuri na kuweka mikakati thabiti ya kuweza kuhimili mashindano hayo ili kuweza kuibuka washindi,” Katibu huyo alieleza kwenye taarifa hiyo.
Viongozi hao walitumia
nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano
wanaowapatia, kwani umekuwa chachu ya Timu hiyo katika kufanya vizuri kila
mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, mashindano hayo ya Mei Mosi yatashirikisha timu kutoka mashirikisho ya
SHIMIWI, SHIMUTA, SHIMISHEMITA na BAMMATA, ambayo huratibiwa na TUCTA, ambapo
timu shiriki zinatakiwa kufika kwenye kituo cha michezo kuanzia April 14,
2023.
Michezo itakayochezwa
kwenye mashindano hayo ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa wavu, riadha,
karata, baiskeli, drafti, bao, karata na mpira wa wavu.
Katika kilele cha
mashindano hayo ambayo pia ni Siku ya Wafanyakazi Duniani, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassan anatarajiwa kuwa mgenmi
rasmi na atatoa zawadi kwa washindi wa kwanza.
Viongozi wengine
waliohudhuria ni Fidelis Choka (Makamu Mwenyekiti), Theodosia Mwangoka (Naibu Ktibu
Mkuu), Shaibu Kanyochole (Mjumbe SHIMIWI), Rhoida Makasi (Mjumbe), Spear
Mbwembwe (Mwalimu wa Timu) na Joyce Nkoliala (Mwalimu wa Timu).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni