Jumatatu, 27 Machi 2023

WATUMISHI MAHAKAMA MOROGORO WAPATIWA ELIMU YA MATUMIZI YA FEDHA

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro 

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro hivi karibuni walipatiwa elimu ya matumizi ya fedha kutoka kwa wataalamu wa Benki ya CRDB. 

Elimu hiyo iliyotolewa ililenga kuwawezesha watumishi hao kujua namna ya kutumia vipato wanavyovipata katika uwekezaji na shughuli za kimaendeleo. 

Meneja wa   Benki hiyo toka soko la Chief Kingalu, Bw. Machaku Geni aliwaelekeza watumishi hao namna ambavyo wanaweza kuitumia fulsa ya mikopo ya watumishi toka taasisi za kifedha kufanikisha masuala yao, ikiwemo elimu, ujenzi na hata uwekezaji. 

Aidha, Bw. Machaku alionya juu ya watumishi ambao wanachukua mikopo bila kuwa na malengo kwani kitendo hicho hugeuza kuwa mizigo badala ya faida kama ilivyokusudiwa. 

Aliongeza kuwa mtumishi anaweza kuwekeza akiba yake kidogo kidogo ndani ya muda maalumu ambayo inaweza kumsaidia kutimiza malengo yake, badala ya kusubiri kuja kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja, jambo ambalo hutokea kwa nadra sana. 

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, akiongea katika tukio hilo alisema kuwa litakuwa jambo zuri kama itakapofika mwishoni wa mwaka 2023 kila mtumishi atakuwa na jambo lenye maendeleo la kujivunia baada ya kulifanikisha kutokana kipato chake. 

“Tusiogope kukopa fedha benki, mimi mwenyewe nilishawahi kukopa fedha na nikafanikisha nilichokuwa nawekeza katika kipindi hicho na kurejesha fedha niliyokuwa nadaiwa na Benki kwa uaminifu,” alisema Mhe. Ngwembe. 

Elimu hiyo ilionekana kukonga nyoyo za watumishi hao ambao walichangia hoja mbalimbali ikiwemo kuuliza maswali ambayo yalipatiwa majibu. Ikumbukwe kuwa elimu hii imefanikiwa kutolewa kutokana na Mahakama Kanda ya Morogoro kuendeleza mahusiano mazuri na wadau.

Meneja wa CRDB Tawi la Chief King Kingalu, Bw. Machaku Geni akitoa elimu ya masuala ya fedha kwa watumishi wa Mahakama. Waliokaa nyuma yake ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro wakiongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. Paul Ngwembe (katikati), Mhe. Messe Chaba (kushoto) na Mhe. Gabriel Malata (kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (katikati) akisisitiza jambo katika tukio hilo la utoaji wa elimu.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama (juu na chini) wakifuatilia tukio hilo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni